Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haji Omar Kheir akizindua Bodi ya Utumishi ya Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar huko Maisara.
Picha ya Pamoja ya Wajumbe wa Bodi ya Utumishi ya Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar pamoja na Waziri Haji Omar Kheir akiyekaa pamoja na Katibu Mkuu wake Joseph Meza kuliani kwake huko Maisara.
Na: Maelezo Zanziba
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haji Omar Kheir ameishauri Bodi ya Utumishi ya Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar kufuata misingi ya sheria,busara na hekima ili Bodi hiyo iweze kufanya kazi zake vyema na kufikia lengo lake.
Waziri Kheri ameyasema hayo leo wakati alipokuwa akizindua Bodi hiyo katika Afisi ya Bodi hiyo iliyopo Maisara mjini Zanzibar.
Amesema ana matumaini makubwa kuwa Wajumbe wa Bodi hiyo watafanya kazi zao kwa uzalendo mkubwa bila ya upendeleo wala kumuonea Mtumishi yeyote katika kazi zao.
Ameongeza kuwa za msingi za Bodi hiyo ni kuwashughulikia watumishi wa Afisi hiyo ambao wanatakiwa kuwaita na kuwasikiliza na kujua uhalisia wa upotevu wa nidhamu kutokana na makosa mbalimbali waliyonayo na hatimaye kuishauri Serikali.
Amesema Bodi iliyopita ilikuwa na tatizo la kutokukutana kwa mujibu wa Ratiba na Kalenda ya Vikao vyake kisheria na kuisihi Bodi hiyo iweke utaratibu wa kukutana ili kuepukana na tatizo hilo kutorejewa tena.
Amewataka Wajumbe wa Bodi kuzikabili changamoto zinazoikabili Bodi hiyo kwa kufuata misingi ya sheria namba 11 ya mwaka 2003 na kupitia Sheria ya Utumishi wa Umma namba 2 ya mwaka 2011.
Aidha Waziri Kheir amewahakikishia mashrikiano ya karibu Wajumbe wa Bodi hiyo na kuongeza kuwa milango iko wazi kwa Bodi kukutana naye ili kushauriana juu ya mambo yanayohusu utendaji wao wa kazi zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo Amina Juma Zidi Kheir amemuhakikishia Waziri huyo mashirikiano ya kutosha kutoka kwao ili waweze kutimiza malengo yao na kufanikisha kazi hiyo waliyopewa.
Amesema licha ya changamoto ambazo zinaweza kuikabili Bodi hiyo lakini watajitahidi kuzifuata sheria na kanuni ziliopo ili kuondoa uonevu kwa mtumishi yeyote.
Bodi hiyo ambayo imezinduliwa na Waziri huyo wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na mambo mengine inakusudiwa kuchochea uwazi na uwajibikaji wa wafanyakazi juu ya kulinda na kusimamia mali za Serikali pamoja na matumizi ya Fedha.
Picha zote na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
Post a Comment