Nia ya Mbunge wa Kigoma
Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, kuwania urais mwaka 2015, imezidi kujionesha,
baada ya kupendekeza umri wa mgombea nafasi hiyo kuwa miaka 35.
Zitto ametoa rai hiyo
wakati akichangia maoni kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipokutana na wabunge
mjini hapa jana.
Mbunge huyo ambaye hadi
kufikia mwaka 2015 atakuwa na miaka 38, ameshatangaza nia ya kuwania urais
ingawa suala la umri linaonekana kuwa kikwazo kwake, kwa mujibu wa
Katiba.
Akichangia maoni yake jana,
alisema umri wa mtu kuruhusiwa kugombea urais uanzie miaka 35 kama ilivyo katika
nchi nyingine.
Alitoa mfano wa nchi za
Rwanda, Burundi, Afrika Kusini, Kenya, Uganda, Marekani ambapo umri uliowekwa
katika katiba zao ni kuanzia miaka hiyo.
Aidha, alipendekeza muda wa
rais kukaa madarakani uwe kipindi kimoja cha miaka saba na akimaliza asiruhusiwe
kugombea tena.
Wengine waliopendekeza umri
wa miaka 35 ni pamoja na Mbunge wa Tarime Chacha Nyangwine, Hamis Kigwangala na
Ali Kessi.
Walisema umri huo ndio
unaotumika na nchi nyingi duniani na hata kuwekwa kwenye katiba za nchi
zao.
MAONI
TOFAUTI
Suala kuwepo kwa kipindi
maalumu cha Rais kuwepo madarakani, umri wa kugombea urais, vyombo vya habari
kuwa mhimili wa nne na serikali tatu, miongoni mwa masuala yaliyoibuka katika
michango ya wabunge.
Aidha, haki ya mgombea
binafsi na mawaziri wasitokane na wabunge na uraia wa nchi mbili ni mambo
yaliyotawala katika michango hiyo.
Tume hiyo inayoongozwa na
Jaji Joseph Warioba, ilianza kazi hiyo tangu Julai mwaka huu kwa kukusanya maoni
ya mtu mmoja mmoja, baadaye itaingia kwenye awamu ya pili ya kukusanya maoni ya
vikundi.
Kuhusu kipindi cha mtu
kukaa bungeni, Kessi alipendekeza awe na awamu mbili na viongozi wastaafu
wasiruhusiwe kuchukua fomu za ubunge . “Haiwezekani wastaafu waje bungeni
kusinzia,” alisema.
Alitaka ukubwa wa baraza la
mawaziri upunguzwe na ubaki na mawaziri 14 na manaibu 14.
Aidha, alisema majimbo
yapunguzwe kwa kuwa yamekuwa mzigo kwa taifa na kutoa mfano wa Pemba na Unguja
ambako kuna wabunge zaidi ya 60 na kutaka majimbo yapimwe kwa
ukubwa.
Mchungaji Peter Msigwa
(Iringa Mjini), alipendekeza suala la Viti Maalum lifutwe na mtu aingie kwenye
ushindani na kuchaguliwa kwa uwezo wake.
Hoja hiyo iliungwa mkono na
Diana Chilolo (Viti Maalum) aliyesema kuwa wabunge wa Viti Maalumu
wanadharauliwa hata wageni wanapokwenda kwenye wilaya zao wanasahauliwa
kutambulishwa.
Suala la Muungano na kuwepo
kwa serikali tatu lilionyesha kuchukua maoni ya wabunge wengi ambapo
walipendekeza kuwe na Serikali ya Muungano, Serikali ya Tanganyika na Serikali
ya Zanzibar.
Hoja hiyo ilichangiwa pia
na Musa Haji Komba, Mariam Msabaha, Ester Bulaya, Mohamed Mnyaa, Zitto Kabwe,
ambapo baadhi walipendekeza kuwepo kwa muungano wa mkataba ili kuangalia masuala
waliyokubaliana kwenye muungano kama yanatakelezeka.
Kombo alisema muungano wa
sasa ni muungano wa sehemu moja kutawala upande mwingine wa muungano na kutaka
katika iangalie katika suala hilo. Aidha, Zitto alipendekeza kuwe na nchi moja,
dola moja na serikali tatu.
Suala la mbunge wa baraza
la wawakilishi kuingia kwenye Bunge la Muungano na wa Bunge la Muungano
kutoingia kwenye Baraza la Wawakilishi lilitakiwa liangaliwe ili kutoa haki kwa
pande zote mbili za muungano.
Hamad Rashid, alipendekeza
katiba mpya ieleze mawaziri wanaoteuliwa nje ya Bunge wathibitishwe bungeni
badala ya ilivyo sasa kwa kuteuliwa na Rais.
Aidha, alisema katiba ya
sasa iweke wazi kuwepo kwa mahakama ya katiba ili kuepuka uvunjwaji unaoweza
kutokea.
Cesilia Pareso (Viti
Maalum-Chadema), alisema katiba ya sasa iweke mhimili wa nne wa vyombo vya
habari ambao utakuwa na jukumu la kukosoa mihimili mingine ambayo ni Serikali,
Mahakama na Bunge.
Spika wa Bunge, Anne
Makinda, aliwasifu wabunge kwa kujitokeza kwa wingi kuchangia maoni hayo na
kueleza umuhimu wa Katiba kuwa ni uhai wananchi. “Mmeonyesha hali ya uwajibikaji
mbele ya umma,” alisema.
habari NA BEATRICE
BANDAWE
CHANZO: NIPASHE
JUMAPILI
Post a Comment