MJUMBE wa Halmashauri
Kuu ya CCM (NEC) wa Wilaya ya Karatu, Daniel Awakie, amewataka vijana wilayani
Karatu, kuungana na kuanzisha vikundi vya ujasiriamali na uchimbaji madini, ili
iwe rahisi kusaidiwa na Serikali.
Akizungumza katika
mkutano wa hadhara katika Kata za Karatu mjini na Qasai, katika mfululizo wa
mikutano yake ya kukagua uhai wa chama hicho, Awakie alisema ili vijana waweze
kupata usaidizi ni vyema wakaungana.
“Serikali ya Chama Cha
Mapinduzi, imejipanga kuwasaidia vijana lakini haiwezekani kusaidia mtu mmoja
mmoja hivyo mnapaswa kuunda vikundi na tutashirikiana mpate maeneo ya
ujasiriamali na pia vitalu vya kuchimba madini ya dhahabu ambayo yamegundulika
hapa Karatu,”alisema Awakie
Awakie alisema Serikali
ya CCM imejipanga kutatua kero za wananchi wa Karatu, ili kuhakikisha pia kuwa
wanalirejesha CCM Jimbo la Karatu ambalo kwa sasa linashikiliwa na
Chadema.
“Ndugu zangu tumewapa
Chadema jimbo na halmashauri, lakini wameshindwa kutatua matatizo yetu, sasa
wapo katika mgogoro, tumekuja hapa kuwaeleza kuwa CCM inakusudia kuondoa kero
zetu,”alisema Awakie.
Alisema CCM sasa
imepania kurejesha heshima yake Karatu, kwa kuwa karibu na wananchi na kupokea
kero zao na kuzipatia ufumbuzi wa haraka.
Mwenyekiti wa CCM wa
Wilaya ya Karatu, Mustapha Kassimu ,alisema katika kuhakikisha kuwa wanarejesha
jimbo hilo, wanatarajia kushinda katika uchaguzi wa mji mdogo
Karatu.
“Tunataka tuanze na
uchaguzi wa mji mdogo, kwani hapa mjini kuna matatizo ya vijana kukosa maeneo
kwa wajasiriamali na viongozi wa Chadema wameshindwa kuwasaidia na kuamua
kuwaondoa mjini. Sasa CCM tumesema wasiondoke mpaka wapewe maeneo,”alisema
Kassim.
Katika mikutano hiyo,
baadhi ya vijana waliutaka uongozi wa CCM kusaidia kupata maeneo ya kufanya
biashara zao hasa baada ya kutakiwa kuondoka katikati ya mji wa
Karatu/
Pia walitaka wasaidiwe
kupata leseni za kuchimba madini ya dhahabu yaliyogundulika katika Kata ya
Endabash, wilayani humo.
Post a Comment