
Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya
Binadamu (NIMR) Kituo cha Tanga, Dk. Mercy Chiduo akiwasilisha utafiti
uliofannywa na kikundi cha watafiti wa NIMR nchini, juu ya uwezo wa dawa ya
Ciprofloxacin kutibu ugonjwa wa Kisonono. Taarifa hiyo ya utafiti huo wa awali
ilitolewa mbele ya Waandishi wa habari na Watafiti mbalimbali jijini Dar es
Salaam leo Desemba 2012.
**********
Na Mroki Mroki, FK Blog
UGONJWA wa zinaa wa
Kisonono umekuwa sugu kutibika kwa kutumia dawa ya Ciprofloxacin na kusababisha
wagonjwa kutokukopona.
Kutokufanya kazi kwa dawa
hiyo kutibu ugonjwa wa Kisonono kumegunduliwa na kundi la watafiti wa Kitanzania
kutoka Taaisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Kuongozwa na
Mr. John Changalucha, wa NIMR Mwanza na kufanya utafiti juu ya ufanyaji kazi wa
dawa hiyo kwa kutibu kisonono katika wilaya za Tanga, Moshi mjini, Dar es
Salaam.
Akiwasilisha taarifa ya
awali ya utafiti huo uliofanyika kuanzia Oktoba mwaka 2011 na kumalizika Aprili
mwaka huu kwa hizo tatu kabla ya watafiti hao kumalizia Wilaya ya Mbeya Mjini,
Dk. Mercy Chiduo kwa niaba ya Watafiti wenzake amesema Wilaya ya Moshi mjini
ndio tatizo limebainika kuwa kubwa zaidi.
Dk. Mercy ameeleza kuwa
Wilayani Moshi wagonjwa wote waliofanyiwa utafiti walionesha kutokupona kwa dawa
hiyo ya Ciprofloxacin sawa na asilimia 100, huku Wilaya ya Tanga ulikuwa kwa
asilimia 25 na Dar es Salaam ikiwa ni kwa asilimia 71.4.
Aidha mtafiti huyo anasema
uwezo wa dawa hiyo kutibu Kisonono kwa utafiti huo ni sawa na asilimia 40 hivyo
kuwa kinyume na sheria ya Shirika la Afya Duniani ambalo linagiza kuwa dawa ili
iwepo katika orodha ya kutibu magonjwa husika ni lazima iwe na uwezo wa kutibu
kwa asilimia 95.
Watafiti hao wamependekeza
dawa za ceftriaxone, cefixime, azithromycin na spectinomycin zitumike kwa sasa
kutibu ugonjwa wa Kisonono huku Ciprofloxacin ikibaki kutibu magonjwa mengine
isipokuwa Kisonono.
Wagonjwa wapatao 353
walijitokeza katika utafiti huo katika vitengo vya Magonjwa ya Zinaa kwenye
vituo vya afya vya Ngamiani jijini Tanga, Majengo mjini Moshi, na Zahanati ya
IDC Jijini Dar es Salaam.
Kushindwa kwa dawa hiyo
kutibu kunatokana na ugonjwa huo kuwa sugu kufuatia tabia ya wagonjwa wengi
kujinunulia dawa bila kupatiwa vipimo vya daktari na hili linadaiwa kutokana na
kuwepo kwa maduka ya dawa ambayo huwauzia wagonjwa dawa bila kuwa na vyeti vya
daktari.
Utafiti huo wa uwezo wa dawa
hiyo kutokutibu unakaribia kuendana na ule uliowahi kufanyika katika nchi za
Israel (61%), Urusi (68%) Kanda ya Magharibi ya WHO (62%-70%), Afrika Kusini
(42%), Japan (24.4%) na China (34.3%), huku Jiji la Mwanza-Tanzania, likionesha
dawa hiyo kutokufanya kazi kwa asilimia 71 katika utafiti uliofanyika mapema.


Post a Comment