Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisoma hotuba yake wakati wa
sherehe za kuupokea Mwaka mpya wa Kiislamu 1434 Hijriyya, zilizofanyika katika
Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, leo Desemba 16, 2012. Picha na
OMR
Sherehe
hizo za kuukaribisha mwaka mpya wa Kiislamu 1434 Hijriyya ambazo zilifanyika leo
katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam zilihudhuriwa na waumini wa
Kiislamu kutoka nchi mbalimbali pamoja na mabalozi wa Sudan, Oman na Iran nchini
Tanzania.
Akizungumza na waumini hao
Dk. Bilal aliwataka Waislamu kuuanza mwaka mpya wa Kiislamu kwa kuepuka
machafuko na kudumisha amani ambao ndio msingi mkuu wa dini ya
Kiislamu.
Makamu wa Rais alisema
katika serikali wameanza kuingia wasi wasi kutokana na vurugu za hivi karibuni
ambazo zimeashiria kuvunjika kwa amani nchini.
“Mimi na wenzangu
Serikalini tumeanza kuingia wasi wasi. Hivi karibuni katika nchi yetu kumetokea
vurugu ambazo hatimaye zimeashiria kuvunjika kwa amani ya nchi yetu. Mali
zimepotea na wengine wamepoteza maisha kwa kisingizio cha dini,” alisema Dk.
Bilal na kuongeza
“Machafuko hayo
yametufanya tujiulize hawa watu wanafuata misingi ipi ya Dini ambayo imewafanya
wao wawe na jazba kiasi cha kushindwa kuwa na busara katika maamuzi yao. Je ni
vipimo vipi vya msingi wa Dini ambavyo wao wanavifuata. Tunashindwa kupata
jawabu”.
Makamu wa Rais aliwaeleza
waumini hao kuwa kwa mawazo yake anaona matatizo mengi yanayolenga Uislam ni
ukosefu wa elimu, ile ya Uislam wenyewe, na elimu ya dunia na kuwataka Waislamu
kusoma kwa dhati jambo ambalo anaamini linaweza kusaidia mambo ya jazba
yakapungua na hatimaye kutokomea kabisa.
“Tukiendeleza jazba ndio
ziwe na nguvu kuliko mafunzo ya Quran tukadhani kuwa mwenye jazba ndiye Muislamu
wa kweli tutaharibikiwa,” alibainisha.
Akisoma risala ya Jumuiya
hiyo, Sheikh Juma Nassor Alhinai aliiomba serikali kuifanya siku ya kwanza ya
mwaka mpya wa Kiislamu kuwa ni ya mapumziko
Naye Sheikh Mkuu wa Mkoa
wa Dar es salaam, AlhajiMussa Salum alikubaliana na wazo hilo lakini aliwataka
Waislamu wenyewe kubadilika kwa kuitangaza tarehe hiyo ya kwanza ya mwaka mpya
kwa kuipa nafasi katika maisha yao ya Kiislamu ili iweze kutambulika
ipasavyo.


Post a Comment