Baada ya kunusurika kufa ndani ya uwanja, hali iliyompelekea kustaafu Kucheza mpira katika Umri mdogo, Fabrice Muamba ameonesha kipaji chake kwa sanaa ya kucheza Muziki katika kipindi maalumu cha dansi ‘Strictly Come Dancing’ kinachorushwa na Televisheni ya BBC Entertainment.
Ikiwa ni miezi kadhaa tangu kustaafu Mpira wa miguu, Muamba mwenye miaka 24 alicheza wimbo maalum wa Christmass ‘The Waitresses’ katika mtindo wa Salsa huku akipewa sapoti na dansa wa kike maarufu kama Vilani.
Mchezaji huyo wa zamani wa Bolton Wanderers na mzaliwa wa Zaire, aliwambia waandishi wa habari kuwa lengo la yeye kushiriki ni kutaka kufurahi na kupata faraja, Muamba aliongezea “ ulikuwa ni uzoefu mzuri sana kwangu na nimefurahia, nilitaka kuonesha ulimwengu upande mwingine kuhusu mimi, pia ni jukwaa la kuonesha kuwa sasa nafanya vingine”.
Muamba alimalizia kwa kusema “ Ndio! nakumbuka sana kucheza mpira lakini ipo wazi sababu ya kwanini sitocheza tena, na kitu muhimu zaidi katika maisha yangu ni Mke wangu na mwanangu”.