Tatizo hilo na mengine, limegundilika kufuatia utafiti uliofanywa na Mtafiti, ambaye ni Mhitimu wa Stashahada ya Juu ya Mawasiliano ya Umma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ally Kileo.
Utafiti huo, ambao matokeo yake yalitangazwa na Kileo katika mkutano wake na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, ulifanywa kwa lengo la kuchunguza matatizo ya msingi yanayoikabili bodi hiyo hasa katika eneo la mawasiliano kupitia teknolojia ya ‘intaneti’ katika kuwahudumia wadau wake wakuu, ambao ni wanafunzi.
Pia ulilenga kutoa mapendekezo ya kitaalamu ili kuiwezesha bodi hiyo kutoa huduma bora zaidi.
Kileo alisema matatizo yaliyochunguzwa zaidi katika utafiti huo, yalikuwa katika mawasiliano wakati wa maombi ya mikopo ya karo na gharama za shughuli za kimasomo, hasa pesa kwa ajili ya kufanyia utafiti na mafunzo kwa vitendo.
Alisema katika utafiti huo, asilimia 55 ya washiriki wote 45 walisema matumizi ya intaneti, vipeperushi, matangazo ya kubandikwa, matangazo ya redioni na katika televisheni kama njia za mawasiliano, bado hazijaiwezesha bodi kutoa au kufanya shughuli za mawasiliano vizuri na kwa wakati baina yake na wadau wake katika kutoa huduma sahihi na kwa haraka.
Kileo alisema katika kuchunguza matumizi ya mtandao wa intaneti kama chombo kikuu cha mawasiliano, upungufu mkubwa zaidi umegundulika; mmojawapo ikiwa ni kukosekana kwa ubunifu na matumizi madogo ya njia ya mawasiliano ya intaneti.
Mwingine ni urasimu usio wa lazima, kuchelewa kwa majibu ya maswali au maelezo yanayotokana na zoezi la usajili, kukosekana kwa uwazi na ukweli katika mchakato wa kupanga mikopo na kukosekana kwa ushirikiano katika mawasiliano katika mawasiliano kati ya bodi na wadau wake.
Alisema katika nchi zilizoendelea kwenye teknolojia ya utoaji wa mikopo ya elimu kwa kutumia mtandao wa intaneti, kama vile Afrika Kusini na Botswana, shughuli zinazochukua siku mbili Tanzania, huko huwachukua saa chache kuzikamilisha.
Kileo alisema utafiti huo ulibaini pia kuwa siyo tu uzembe wa watendaji katika vitengo vya bodi kufanya huduma za bodi kuwa duni na mbaya, lakini pia kukosekana kwa nia ya dhati ya kuboresha huduma za bodi kunafanya zoezi lote la matumizi ya mtandao wa intaneti kutoa huduma kuwa kama mchezo wa kuigiza usio na waigizaji wala watazamaji sahihi.
Alipendekeza bodi kuimarisha na kuboresha huduma za mawasiliano ya mtandao wa intaneti kwa kuongeza taaluma ya mawasiliano ya umma kwa watendaji wake katika zama hizi za utandawazi na kujenga kituo cha mawasiliano ya huduma kwa wateja kwa njia ya simu na inataneti itakayopatikana kwa saa 24 kwa gharama za mtumiaji wa hudumac hiyo.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment