Kocha Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Kim Poulsen (pichani) ametangaza kikosi cha wachezaji 24 kitakachoingia kambini tayari kuvaana na timu ya Zambia (Chipolopolo) Disemba 22 mwaka huu.
Katika uteuzi huo kocha Poulsen amemtema kipa wa Azam Deogratius Munishi ‘Dida’ na badala yake amemuita kipa wa kikosi cha chini ya umri wa miaka 20 cha Azam Aishi Mangula, huku akimrejesha kikosini nahodha wa Yanga na timu ya soka ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) Nadir Haroub, ‘Canavaro’.
Katika orodha hiyo Kim amewaita kwa mara ya kwanza kiungo mshambuliaji wa Zanzibar Heroes na timu ya Azam Mcha Khamisi na beki wa kushoto wa Heroes na Azam Samii Haji Nuhu kutokana na uwezo mkubwa waliouonesha kwenye michuano ya Kombe la Chalenji iliyomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita, Kampala, Uganda.
Wengine waliotemwa na Kim kwenye kikosi hicho ni mshambuliaji chipukizi wa Simba Ramadhani Singano na Edward Christopher kutokana na kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye timu ya Simba.
Akizungumza na waandishi wa habari Kim amesema kwamba kikosi hicho kitaingia kambini leo na kesho kitaanza mazoezi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume kujiandaa na mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Zambia itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Desemba 22.
Aliwataja wachezaji hao kuwa ni makipa Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ally (Azam) na Aishi Mangula (Azam U-20 ).
Mabeki ni Nassoro Masoud ‘Cholo’, Shomari Kapombe, Amiri Maftah (Simba), Erasto Nyoni, Agrey Moris, Samii Haji Nuhu (Azam), Issa Rashidi (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani, na Nadir Haroub ‘Cannavaro’(Yanga).
Viungo ni Shaabani Nditi (Mtibwa Sugar), Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba (Simba), Salumu Abubakari (Azam), Frank Domayo, Athumani Idd ‘Chuji’(Yanga), Mcha Khamisi (Azam).
Washambuliaji ni Simon Msuva (Yanga), Thomasi Ulimwengu, Mbwana Samatta (TP Mazembe), John Bocco (Azam) na Mrisho Ngassa (Simba).
Post a Comment