Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Chato (CCM) Dk. John Magufuli
****************Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Chato (CCM) Dk. John Magufuli amemuomba radhi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Said Mwema, kufuatia uharibifu wa mali za jeshi hilo uliofanywa na wananchi wa Wilaya ya Chato mkoani Geita.
Dk. Magufuli aliomba radhi kwa niaba ya wananchi
wake kufuatia, kujeruhi, kuchoma moto na kuharibu mali za jeshi hilo uliofanywa
na baadhi ya wananchi wilayani humo Julai 10, 2007.
Aliomba radhi wakati alipopewa fursa ya kuzungumza
kwenye uzinduzi wa kituo kipya cha polisi uliofanywa na IGP Mwema, baada kile
kiichokuwepo kuteketezwa kwa madai ya kumsaka mwanamke aliyetuhumiwa kukutwa na
ngozi ya binadamu.
Waziri Magufuli alisema ana kila sababu ya
kuwaombea radhi wananchi wake kwa Jeshi la Polisi kwa kitendo cha kuwajeruhi
askari watano ambapo mmoja alivunjwa taya, mwingine kutobolewa jicho na kuchoma
moto kituo cha polisi.
“Hata hivyo namshukuru IGP Mwema kwa kushiriki
kikamilifu katika ujenzi wa kituo kipya cha polisi na nyumba za askari wetu
katika Wilaya ya Chato… Jamani lakini wananchi wasingeyafanya yale hiki kituo
cha kisasa tungekipata wapi?... Sifurahii waliyoyatenda ila nafurahia ujenzi wa
kituo kipya kukamilika na leo kinazinduliwa.” Alisema Magufuli.
Aidha aliwataka wananchi kulithamini Jeshi la
Polisi na kushirikiana kuimarisha usalama wa raia na mali zao kwa kutoa taarifa
za uhalifu unapojitokeza.
Katika uzinduzi huo wa kituo kipya cha polisi na
nyumba za askari Waziri Magufuli aliikabidhi hospitali ya Wilaya ya Chato shuka
200 za wagonjwa .
Alisema hafurahishwi na kuwalaza wagonjwa kwenye
mashuka machafu na kutishia kuwa atafanya ziara za ghafla kuangalia usafi wa
hospitali hiyo akisisitiza kuwa usafi ni muhimu ili kuzuia magonjwa ya milipuko.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Post a Comment