Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam,
imetuma timu ya Makachero kuja Zanzibar kuungana na wenzao wengine wa Polisi
Zanzibar katika Upelelezi wa tukio la kushambuliwa kwa Paroko wa Parokia ya
Mpendae Amrose Nkenda (pichani).
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya
Jinai Zanzibar ACP Yusuf Ilembo, amesema kuwa timu hiyo ambayo inaongozwa na
Afisa mmoja wa ngazi ya juu (hakumtaja jina) ina jumla ya Makachero watano
waliobobea katika masuala ya upelelezi hapa
nchini.
Amesema kuwa nia ya Mkuu wa Jeshi la Polisi
nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, kuituma timu hiyo kuja hapa Zanzibar, ni
kutaka kuengeza nguvu katika tukio hili ambalo linatazamwa kwa aina tofauti hasa
ikizingatiwa kuwa aliyeshambuliwa ni Kiongozi mkubwa wa dini na limetokea katika
kipindi cha siku kuu ya Krismas.
Amesema Jeshi la Polisi limeamua tukio hili
kupelelezwa kwa pamoja kati ya wenzao wa makao makuu ya Polisi Dar es salaam na
wa hapa Zanzibar ili kuhakikisha kuwa wale wote waliohusika katika kumshambulia
Paroko huyo wanakamatwa.
Hata hivyo kamanda Ilembo amesema kuwabado
Polisi wanaendelea na Upelelezi wa kubaini sababu za kushambuliwa kwa Paroko
huyo bila ya kuibwa kwa kitu chochote kutoka kwa
mshambuliwa.
Amesema kuna uwezekana kuwa watuhumiwa
wameshindwa kuchukua kitu chochote baada ya kubaini kuwa eneo la tukio
lisingekuwa salama kwao kwa vile kulikuwa na walinzi na ni eneo ambalo ni karibu
kabisa na makazi ya viongozi wengine wa dhehebu
hilo.
Akizungumzia siku kuu ya mwisho wa mwaka 2012
na mwanzoni mwa mwaka 2013, Kamanda Ilembo amewahimiza wananchi kuendelea kutoa
ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa pale wanapobaini kuwepo kwa
wahalifu ili wachukuliwe hatua.
Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi
Zanzibar ACP Aziz Juma Mohammed, amewatahadharisha wazazi na walezi kutowaruhusu
watoto wadogo kuranda barabarani ama kwenda katika fukwe za bahari kuogelea
pasipo uangalizi wa watu wazima.
Kamanda Aziz amesema kuwa uzoefu unaonyesha
kuwa watoto wengi wamekuwa wakigongwa na magari ama kuzama na kufa maji katika
siku hizi za siku kuu za mwisho wa mwaka kwa kukosa uwangalizi wa watu
wazima.
Aidha amewataka wananchi kutoziacha nyumba zao wazi ama bila ya kuwa na uwangalizi wa kutosha ili kutowapa nafasi kwa wahalifu kupata fursa ya kuwaiba.
Post a Comment