RAIS wa Misri Mohamed
Morsi ameagiza jeshi nchini humo kuchukua mamlaka ya polisi kuwakamata wale wote
wanaoandamana kupinga kufanyika kwa zoezi la kura ya maoni kupitisha rasimu ya
katiba mpya siku ya Jumamosi, uamuzi ambao serikali inasema unaanza kutekelezwa
mara moja.
Wakati uamuzi huo
ukitolewa, maandamano makubwa yamepangwa kufanyika siku ya Jumanne jijini Cairo
nchini Misri, yatakayoongozwa na kundi moja linalomuunga mkono rais Mohammed
Morsi na lingine la upinzani.
Upinzani unasema
unatumia maandamano hayo kupinga kufanyika kwa kura ya maoni kupitisha rasimu ya
katiba mpya wakati wafuasi wa rais Morsi wakisema maandamano yao yatakuwa ni ya
kumuunga mkono kiongozi wao.
Muungano wa vyama vya
kiislamu nchini humo vinasema vinapinga wito wa upinzani wa kutaka zoezi la kura
ya maoni kuahirishwa kwa kile wanachokidai kuwa huo ndio wakati wa nchi hiyo
kupata katiba mpya na ni sharti zoezi hilo liendelee kama ilivyopangwa.
Upinzani kwa upande wao
unaona kuwa katiba hiyo mpya ikipita itawabagua pamoja na makundi ya wanawake
na pia inagandamiza haki za wakiristo na wanawake.
Wiki iliyiopita, maelfu
ya wapinzani waliandamana katika maeneo mbalimbali nchini humo kumshinikiza
rais Mohammed Morsi kuondoa madaraka aliyojioongezea suala ambalo alisalimu amri
na kuyaondoa lakini akasisitiza kuwa zoezi la kura ya maoni kuhusu katiba mpya
litaendelea kama ilivyopangwa.
Jeshi nchini humo
limetangaza kuwa halitaruhusu waandamanaji kuligawa tena taifa hilo na
watatumia mbinu zote kuhakikisha kuwa wanalinda amani na kuepusha ghasia
zilizosababisha watu saba kupoteza maisha na mamia kujeruhiwa wiki
iliyopita.
Post a Comment