Na Anna Nkinda – Maelezo,
Kagera
Serikali imeombwa kuongeza
kiasi cha mkopo kinachotolewa kwa vijana kupitia mfuko wa maendeleo wa vijana na
Halmashauri za wilaya kwani kiwango kinachotolewa kwa sasa cha shilingi milioni
tano kwa vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) ni kidogo ukilinganisha na
mahitaji ya mkopo huo.
Ombi hilo limetolewa jana na
baadhi ya vijana waliopata mkopo huo kupitia SACCOS ya Ibwera na halmashauri ya
wilaya ya Bukoba wakati wakiongea kwa nyakati tofauti na Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara alipotembelea wilaya hiyo
ili kuona jinsi fedha hizo zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua
kiuchumi.
Vijana hao walisema kuwa fedha
za mkopo walizozipata zimewasaidia kujiinua kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuajiri
vijana wenzao, kupanua mitaji ya biashara zao, kulipa karo za shule za watoto
wao na kujikwamua kimaisha tofauti na ilvyokuwa awali kaba hawajapata mkopo na
kufanya shughuli za ujasiriamali.
Kwa upande wake mkazi wa
kijiji cha Ibwera Ibrahim Mulokozi ambaye alipata mkopo wa shilingi laki nne
kupitia SACCOS ya kijiji hicho alisema kuwa ameweza kununua matandazo na kulipa
wasaidizi wanaohudumia shamba lake la migimba na kahawa ambalo ni la mfano
kwa vijana na wazee wanaotoka kata ya Ibwera, Mikoni na Nyakibimbili na kwenda
kujifunza na kuchukua miche ya migomba.
Alisema kuwa anakabiliwa na
changamoto za kutokuwa na fedha za kuendeleza shughuli za kilimo, kutoka na
mbolea ya kutosha ya kurutubisha shamba, bei ya miche ya kahawa kupanda kutoka
shilingi 50 hadi 500 kwa mche mmoja, kuendelea kutumia jembe la mkono, kutokuwa
na masoko ya uhakika hasa soko la ndizi na magonjwa ya migomba.
Naye katibu wa kikundi cha
Msifuni Johanes Joel ambacho kilipata mkopo wa shilingi milioni moja na laki
tano kutoka Halmashauri ya wilaya ya Bukoba alisema kuwa kikundi chao
kinajishughulisha na kazi ya ukulima wa samaki na walianza na bwawa moja na
hivi sasa wana mabwawa matatu na wanampango wa kuhakikisha kuwa kila
mwanakikundi anakuwa na bwawa lake.
“Changamoto zinazotukabili ni
kutokuwa na mtaji wa kutosha, wanachama kutokuwa na elimu ya kuendesha na
kusimamia au kutunza miradi na kufanyiwa hujuma kwa mradi wetu wa samaki ikiwa
ni pamoja na kuibiwa na kuharibiwa kwa mabwawa hasa nyakati za usiku na watu
wasiopenda kufanya kazi za maendeleo”, allisema Joel.
Kwa upande wake waziri Dk.
Mukangara aliwataka vijana wa kijiji hicho kufanya kazi kwa kujituma na kujiunga
katika vikundi vya maendeleo jambo ambalo litawafanya waweze kupata mikopo
kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana na halmashauri ya wilaya na hivyo kuweza
kujishughulisha na kazi za upandaji wa miti, kilimo cha samaki na ufugaji wa
ng’ombe wa maziwa na nyuki.
Dk. Mukangara alisema, “Vijana
ni lazima mfanye kazi na kuachana na tabia ya uvivu, kufanya kazi si lazima
uajiriwe bali unaweza kujiajiri wewe mwenyewe kama hapa Ibwera kunahali ya hewa
nzuri na milima mingi haina miti mnaweza kuwa na mradi wa kupanda miti na kufuga
nyuki ambao watawapatia asali na mkiiuza mtapata fedha nahivyo kujikwamua
kiuchumi”.
Kwa upande wa mafunzo ya
ujasiriamali waziri Dk. Mukangara alisema kuwa wizara yake inavituo vya
kuwajenge uwezo vijana hivyo basi kama wahusika ambao ni vijana watakuwa tayari
kupata mafunzo ya ushirika na mafunzo mengine kama ya uongozi, stadi za maisha
watayapata na yatawasaidia katika maisha yao.
Waziri Dk. Mukangara alikuwa
mkoani Kagera kwa ajili ya kukagua SACCOS na vikundi vya vijana vilivyopata
mkopo kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana ili kuona fedha hizo zimewasaidiaje
vijana kujikwamua kiuchumi. Katika wilaya ya Bukoba alilitembelea shamba la
mfano la kahawa na migomba, kikundi cha burudani cha Rugazi na shamba la
samaki la kikundi cha Msifuni.
Post a Comment