Kikosi cha timu ya Simba
kikiwa katika picha ya pamoja
Simba imetwaa nafasi ya tatu
katika michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu zenye umri chini ya miaka
20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya kuitandika Mtibwa Sugar ya Morogoro
mabao 3-0.
Hadi mapumziko katika mechi
hiyo iliyochezwa leo asubuhi (Desemba 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu
ya Karume, Dar es Salaam, Simba ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
Mabao yote ya washindi katika
mechi hiyo yalifungwa na Ramadhan Mkipalamoto. Mfungaji alifunga bao la kwanza
dakika ya 43 wakati mengine alipachika dakika za 57 na 70. Kwa kunyakua nafasi
ya tatu, Simba imeondoka na kitita cha sh. 500,000.
Mechi ya fainali ya michuano
hiyo kati ya Azam ya Dar es Salaam na Coastal Union ya Tanga itachezwa leo
(Desemba 23 mwaka huu) saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume.
Mbali ya kombe, bingwa wa
michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji Uhai
atapata sh. milioni 1.5 wakati makamu bingwa atazawadiwa sh. milioni
1.
Timu iliyoonesha zaidi mchezo
wa kiungwana (fair play) itapata sh. 400,000, mchezaji bora wa mashindano sh.
350,000, mfungaji bora sh. 300,000 na kipa bora sh. 300,000. Naye kocha bora
katika mashindano hayo atazawadiwa sh. 300,000 kama itakavyokuwa kwa refa
bora.
RAMBIRAMBI MSIBA WA MCHEZAJI
MUSA RICO
Shrikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya
Coastal Union, Musa Rico kilichotokea jana (Desemba 22 mwaka huu) jijini
Tanga.
Msiba huo ni mkubwa kwa wadau
wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti akiwa mchezaji Rico, na baadaye
kocha alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezea na kufundisha
ikiwemo Coastal Union, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF inatoa pole kwa familia
ya marehemu Rico, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga (TRFA) na klabu ya
Coastal Union na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu
cha msiba huo mzito.
Maziko yanatarajiwa kufanyika
leo (Desemba 23 mwaka huu) mkoani Tanga. Mungu aiweke roho ya marehemu Rico
mahali pema peponi. Amina
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA
TAREFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Tabora (TAREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana (Desemba 22
mwaka huu).
Ushindi waliopata viongozi
waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa
TAREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani
Tabora.
TFF inaahidi kuendeleza
ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya TAREFA chini ya uenyekiti wa Yusuf
Kitumbo aliyeshinda kwa kura 16 dhidi ya nane za Musa Ntimizi, na Paul Werema
ambaye hakupata kura.
Uongozi huo mpya una
changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa
miguu mkoani Tabora kwa kuzingatia katiba ya TAREFA pamoja na vyombo vya mpira
wa miguu vilivyo juu yake.
Pia tunatoa pongezi kwa
Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha
uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa
TFF.
Viongozi waliochaguliwa
katika uchaguzi huo ni Yusuf Kitumbo (Mwenyekiti), Fate Remtulla (Katibu), Dick
Mlimuka (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Razak Irumba (Mwakilishi wa Klabu TFF) na
wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao ni Eric Kabepele na Mwalimu
Sizya.
TWFA YAWATUZA TENGA, FURAHA
FRANCIS
Chama cha Mpira wa Miguu
Wanawake Tanzania (TWFA) kimetoa tuzo kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Leodegar Tenga na Meneja wa timu ya Taifa (Twiga Stars), Furaha
Francis kutokana na mchango wao katika kuendeleza mchezo huo.
Tuzo hizo zilitolewa katika
Mkutano wa Uchaguzi wa TWFA uliofanyika Desemba 19 mwaka huu mjini Morogoro
kutokana na mchango wao katika kuendeleza mpira wa miguu kwa wanawake
nchini.
“Ni dhahiri kazi ya
kuendeleza soka ya wanawake ni wajibu wa Shirikisho (TFF), lakini Rais wa TFF
alitoa kipaumbele zaidi na alijitoa kuhakikisha misingi imara ya kuendeleza soka
ya wanawake inawekwa,” alisema Mwenyekiti wa TWFA, Lina
Kessy.
Pia Mkutano huo ulitambua na
kumpa tuzo Furaha Francis ambaye amekuwa Meneja wa Twiga Stars kwa miaka minane
mfululizo. Licha ya kuwa Meneja wa Twiga Stars, ametumia muda wake na kujitoa
katika kuendeleza mpira wa miguu kwa wanawake.
TWFA itaendelea kutumia
michango yao katika mpira wa miguu kwa wanawake nchini.
Boniface
Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF)
Post a Comment