TAARIFA
YA MHE. JANUARY Y. MAKAMBA (MB), NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO, SAYANSI NA
TEKNOLOJIA KUHUSU USITISHAJI WA MATANGAZO YA ANALOJIA NA KWENDA KATIKA MFUMO WA
DIJITALI
Ndugu
Wananchi,
Mtakumbuka
kuwa hapo tarehe 23 Februari 2012 tuliwatangazia kupitia vyombo vya habari juu
ya usitishwaji wa matangazo ya televisheni kwa kutumia teknolojia ya analojia
kwenda katika mfumo mpya unaotumia teknolojia ya dijitali.
Napenda
kuwaleleza kuwa, maandalizi ya kuzima mitambo ya analojia kuanzia tarehe 31
Desemba 2012 yamekamilika kwa mujibu wa makubaliano ya nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hata
hivyo, napenda sasa kutoa taarifa kuwa uzimaji wa mitambo ya analojia
utafanyika kwa awamu kama ifuatavyo:-
(1) Dar
Es Salaam-31 Desemba, 2012;
(2)
Dodoma & Tanga- 31 Januari, 2013;
(3)
Mwanza-28 Februari, 2013;
(4)
Moshi & Arusha-31 Machi, 2013;
(5)
Mbeya-30 Aprili, 2013.
Tumeamua
kuanza kuzima mitambo hiyo kwa Jiji la Dar es Salaam kwanza ili kutoa fursa kwa
makampuni yenye leseni kusimika mitambo ya utangazaji wa dijitali katika mikoa
mingine. Makampuni haya yamejipanga kukamilisha usimikaji wa mitambo hiyo
katika mikoa minane katika miezi minane ijayo.
Mitambo
ya analojia itakayozimwa kesho ni ile iliyopo Kisarawe na Makongo. Vituo
ambavyo siku ya tarehe 1 Januari 2013, vitapaswa kuanza kutangaza matangazo kwa
mfumo wa dijitali ni TBC1, ITV, EATV, Channel 10, StarTV, DTV, CapitalTV,
TumainiTV, ATN, MlimaniTV, C2C, CTN, CloudsTV na Efatha.
Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inafanya jitihada za kutosha kuhakikisha kwamba
makampuni yenye leseni za kusambaza ving’amuzi yanakuwa na ving’amuzi vya
kutosha na vingine vimeagizwa ili kukidhi mahitaji ya baadaye na vile vilivyopo
sokoni vina ubora unaokubalika.
Vilevile,
Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itahakikisha
kwamba zoezi la uhamaji linafanyika bila usumbufu na kero kwa wananchi.
Makampuni yanayouza ving’amuzi yameagizwa yaimarishe huduma kwa wateja wakati
wa kuuza ving’amuzi na hata baada ya ununuzi iwapo wananchi watakuwa na
matatizo na ving’amuzi.
Zoezi
hili la uhamaji ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Tutakapokuwa
tumekamilisha uhamaji, huduma za mawasiliano na utangazaji zitapanuka na kuwa bora
zaidi. Kwa mfano, itawezekana sasa kuangalia televisheni kupitia simu zetu za
mikononi. Vilevile, itawezekana, kwa bei nafuu kabisa, kwa mtu mwenye uwezo wa
kutengeneza vipindi kukodisha chaneli yake na kutangaza vipindi vyake.
Vilevile, bei za mawasiliano na utangazaji zitashuka, na tutakuwa tumepiga
hatua kubwa kwenye mapinduzi ya teknolojia duniani, ambayo nchi yetu haiwezi
kubaki nyuma.
Ndugu
Wananchi,
Serikali
kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itaendelea kutoa elimu kwa
wananchi kuhusu uhamaji huu. Serikali inatarajia kupata ushirikiano wa karibu
kutoka kwa wadau wa sekta ya utangazaji na wananchi kwa ujumla katika kipindi
cha uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa televisheni ili kufanikisha zoezi la
uzimaji wa mitambo ya utangazaji ya teknolojia ya analojia.
Uhamaji
huu hautahusu televisheni za wananchi zinazopata matangazo kupitia madishi
(nyungo) (satellite) au nyaya (cables). Hivyo, wananchi wanaopata matangazo
kupitia DStv, Zuku, na nyinginezo wataendelea kupata matangazo yao kama
kawaida.
Ndugu
Wananchi
Kama
kuna mwananchi yoyote ana kero, malalamiko, swali au anahitaji maelekezo kuhusu
uhamaji, awasiliane na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia namba
0784-558270; 0784558271 au barua pepe: malalamiko@tcra.go.tz
Ndugu
Wananchi,
Nawashukuru
kwa kunisikiliza
Post a Comment