Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Usanifu Majenzi (Architectural) na nadharia ya Freemasonary



Usanifu majengo umekuwa mstari wa mbele kulinda utamaduni wa mahali fulani. Wanajamii wenye maono ya aina fulani ambao hupata uthubutu wa kuyaainisha maono hayo na kuyaweka katika mipango. Kwa kiasi fulani hupata baraka za viongozi wao katika kukamilisha maono au mipango hiyo. Ikumbukwe Usanifu Majenzi (Architecture) ni ‘Sayansi na pia ni sanaa.’ Yaani zipo kanuni za kufanya usanifu (Sayansi) na kwa upande mwingine kuna jinsi au namna ya kutekeleza hizo kanuni (Sanaa). Utamaduni kama uhalisia wa desturi na mazingira ya sehemu fulani huwa ni utambulisho unaotofautiana kabisa na tamaduni zingine. Na walinzi wake ni viongozi. Kwa sasa wengi wa viongozi hao ni wanasiasa.
Historia inatuambia kati ya miaka ya 3000 hadi 2119 KK-(BC); inasemekana kulikuwa na ukuaji wa miji ulio sababishwa hasa na uimara wa mifumo ya kiuchumi na hata katika siasa. Miongoni mwa matunda ya kuimarika kwa vitu hivi viwili yalikuwa ni ukuaji Ngome ya AKKADIANI mwaka wa 2350 KK na ukuaji wa haraka haraka wa miji miwili ule wa Akkad na Mari. Lakini uimarikaji wa vitu hivi ulisababisha kile kilichoonekana uharibifu wa Mila na Desturi. Hasa ukizingatia maeneo haya yalikuwa ni maeneo yenye rutuba hivyo yalikuwa yanapata wahamiaji wengi siku baada ya siku. Hivyo watawala wa nyakati hizo waliamua kuchukua njia za haraka haraka ili kuwezesha utunzaji wa mila na Desturi za maeneo hayo. Kwa mantiki hiyo, wasanifu majenzi walitakiwa kufanya kazi bega kwa bega na watawala hao.
Hata hivyo jibu la swali uliloweka juu ya meza ni pana sana si tu ‘usanifu una uhusiano na siasa.’ Lakini badala yake tunaweza kusema usanifu una uhusiano na Utawala. Ni dhahiri kuwa Ujenzi wa majengo unahitaji kiasi kikubwa cha rasilimali: yaani; vifaa, fedha, muda, nguvu kazi, ardhi, na mengineyo mengi. Kwa hiyo, usanifu majenzi na wasanifu majenzi wamekuwa kile wazungu wanaita ‘bedfellows’ kwa tawala za mahali fulani.
Kwa lugha nyingine, mara nyingi sera ambazo tafsiri nyepesi ni maamuzi mbali mbali katika jamii, aghalabu huwekwa na Wanasiasa au watawala. Au mchango wa Wanasiasa huwa mkubwa sana. Kama Hayati Baba wa Taifa letu (Tanzania) Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyowahi kusema ‘kupanga ni kuchagua!’ Mipango inayotekelezeka hutegemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa mpangaji na mtekelezaji kwa upande wa pili. Wote wakitegemea upatikanaji wa raslimali zinazohitajika katika kuutekeleza mradi husika. Madhali mipango mingi ya maendeleo inaakisi sera za mamlaka husika. Hivyo basi mifumo mbali mbali ya kijamii hutoa taswira ya mamlaka hayo na zaidi uwezo katika raslimali za kuutekeleza mradi huo.
Kwa upande mwingine utaona au utakubaliana na mimi kuwa ‘Usanifu Majenzi’ unaakisi kwa sehemu kubwa namna imani za eneo hilo zilivyo. Ndiyo maana ukiangalia katika mfumo wa ujenzi wa Mji wa Roma utakuwa unaakisi mazingira ya imani ya pale zaidi. Lakini ukiingia Vatican utaona ina ujenzi tofauti kabisa ambao unaonesha dhahiri kuwa umeingia katika eneo jingine ingawa katika ujumla wake unakuwa upo ndani ya Roma. Hapa Tanzania utaona ujenzi wa Kanisa Kuu la Manispaa ya Zanzibar halifanani na Msikiti wa kwanza wa Manispaa hiyo hiyo.
Ukiwa kwenye ndege ukapita juu ya nchi ya Omani au Saudi Arabia mbali na utaona moja kwa moja jinsi ujenzi wa maeneo hayo unavyoshabiana na Imani kuu ya maeneo haya kwa kuwa nchi hizi ni nchi za Kiislam na hivyo aina za ujenzi ni lazima ziheshimu mamlaka za kiserikali na imani husika.
Lakini nichukue mfano mmoja pengine miongoni mwa mingi wa ujenzi wa Hekalu la Kwanza huko Yerusalemu. Utaona kuwa pamoja na mgawanyo wa majukumu kati ya Mtawala wa wakati huo –Mfalme Daudi Mwana wa Yese ambaye ni wa mbari ya Yuda. Na Kuhani ambaye ni wa mbari (ukoo) wa Lawi. Bado Mfalme Daudi alichukua nafasi kubwa katika kubuni mradi huo mkubwa wa ujenzi wa Hekalu. Mfalme Daudi anasema hivi; ‘‘Enyi ndugu zangu na watu wangu nisikilizeni. Nilikusudia moyoni mwangu kujenga nyumba kwa ajili ya sanduku la agano la Mwenyezi Mungu, …..; na nilifanya maandalizi ya kujenga.’’- (1 Mambo ya Nyakati 28:2b-d). Anaendelea kusema ‘‘Sulemani mwanangu aliyechaguliwa na Mungu, bado yungali mdogo, na hana uzoefu mwingi, na kazi hii ni kubwa……Basi nimejitahidi kwa kadri ya uwezo wangu wote kuiwekea nyumba ya Mungu wangu akiba ya dhahabu ya kutengeneza vitu vya dhahabu…..’’-(1 Mambo ya Nyakati 29 :1b na kuendelea). Kwa ujumla utaona palipo na dhamira/utashi wa Kisiasa (political will) miradi mikubwa sana (mega projects) huzaa matunda makubwa yaliyotarajiwa. Kwa upande mwingine utaona kwenye kubomoa miundo mbinu pia ni hawa hawa wanasiasa kwa kutumia majeshi na vifaa vyao hubomoa. Mfano halisi ni vita iliyokuwa Libya na hata yale yanayoendelea kule Syria sasa. Aidha utaona hata Mfalme Sulemani alipoanza kutawala na kushughulikia mradi wa ujenzi wa Hekalu utashi wa kukamilisha mradi huo ulikuwapo. Mwingine anaweza kusema pengine ilikuwa miongoni mwa hadidu zake za rejea wakati anakabidhiwa madaraka. Lakini vipi kama angeamua kuelekeza raslimali hizo katika mradi mwingine? Tafadhali endelea kusoma mwenyewe 2 Mambo ya Nyakati sura ya 2 – 9 na 1 Wafalme 5:1-18, – 10). Miongoni mwa majukumu ya Mfalme ilikuwa kutafuta vifaa vya ujenzi ambavyo havikupatikana katika ufalme wake. Alilazimika kuwasiliana na Viongozi wenzake nje ya Israeli.
Ningependa kumalizia kujibu swali lako kwa kusema, usanifu majengo utabaki kuwa sehemu ya siasa hasa ukizingatia makazi ni sehemu ya haki za binadamu. Hata hivyo ili kujenga jamii iliyo tofauti na nyingine lazima mipango ya ujenzi itofautiane na ya sehemu nyingine. Na hivyo kutoa utambulisho usio na tashwishi wa jamii husika. Kwa kuwa aina ya utawala na imani za jamii duniani hutofautiana.
Bwana Alex Chezi Kutoka Tanzania akauliza Kwanini tunasema Ustaarabu wa kwanza Ulianzia huko Mesopotamia na si sehemu nyingine ya Dunia?
Bwana Alex Tofauti na vipindi vingine vya mapokeo ya ustaarabu kwa mfano kule Misri na hata kule Ugiriki, Mesopotamia ulikuwa sehemu ambayo ilikaribisha mchanganyiko wa mila na desturi Mbalimbali ambazo kiunganishi cha pekee miongoni mwao kilikuwa Fasihi andishi. Namna walivyokuwa wanaabudu miungu na nafasi ya mwanamke katika jamii. Mila, sheria na hata Lugha ziliendelea kutofautiana kipindi kimoja hadi kingine. Kwa mfano watu Akkadi hawakuzungumza Lugha sawa sawa na ile iliyokuja kuzungumzwa na watu wa Babiloni (Babeli). Hata hivyo haki za wanawake na umuhimu wa fasihi andishi na miungu iliyokuwa inaabudiwa kipindi kimoja baada ya kingine viliendelea kushabihiana kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo, Mesopotamia inajulikana pia kama “Cradle of Civilization” kwenye lugha yetu ya Kiswahili tunaweza kusema “chimbuko la ustaarabu.” Bwana Alex ustaarabu unasemekana kuanzia hapa kwa sababu nilizokupa hapo juu moja ikiwa ni ugunduzi wa fahisi andishi lakini pia ile hali kukua kwa miji sambamba na mipango miji yote hii ilifanyika katika karne ya 4 KK hii ni tofauti kidogo na vipindi vingine. Kwa mfano ustaarabu wa Warumi na hata kule Ugiriki.
Ingawa sikudhamiria kuingia kwa kuhalalisha jibu langu kwa kutumia Biblia. Ninajikuta nikilazimika kufanya hivyo katika swali kama hili. Aidha eneo hili la Mesopotamia linaonekana katika mipaka ya ile iitwayo ‘Bustani ya Edeni.’ Kwa maana hiyo siyo jambo la kushangaza kuona hapa panakuwa kitalu cha ustaarabu duniani. Ukisoma kwenye Biblia yako hasa ile ya Kiingereza tangu Mwanzo sura ya pili mstari wa kumi hadi kumi na nne (Mwanzo 2:10-14) Utaona kunatajwa mto ulioinyweshea bustani hiyo kuwa uligawanyika vijito vine. Kati yavyo kuna mito Tigris na Euphrates-(Mwanzo 2:14).
Kwa mazingira hayo kijografia, yenye mandhari nzuri na akiba ya dhahabu kama inavyosomeka. Yamkini vilikuwa vichocheo vya ubunifu kama huo. Tutakapokuwa tunahitimisha mfululizo wa makala hizi tutaongeza maelezo mengine. Lakini pengine unaweza kukubaliana na mimi kuwa pale palipo na Imani huwa pana ustaarabu wa aina fulani. Mchungaji Kateti anaweza kutusaidia zaidi kuhusiana na hoja hii. Kwani pia hili ndilo eneo (Mesopotamia) anakotokea Baba wa Imani Ibrahimu kabla ya kuhamia Kaanani.
Bibi Happiness Mtua kutoka Kenya yeye angependa kupata maelezo kwa kifupi kuhusu mfalme Hammurabi au Hammurapi.
Mfalme Hammurabi alikuwa mfalme wa Babeli, aliyeishi kati ya miaka (1850 – 1750 KK), Inasadikiwa aliitawala Babeli kati ya mwaka 1786-1728 KK). Historia inatuambia mfalme huyu alisifika kwa kuwa na jeshi na lenye nguvu na imara. Na pengine ndiye muasisi wa upangaji kimkakati (strategic planning). Kwa kuwa alichodhamiria kukitenda sasa alikipanga miaka kadhaa kabla. Lakini kubwa zaidi aliwezesha uanzishwaji wa sheria na Mahakama. Ingawa inasemekana kulikuwepo na sheria kadhaa kabla ya Mfalme huyu. Hammurabi alikuwa mfalme wa kwanza kuandika sheria mbalimbali kwa ajili ya kurahisisha kazi ya kiutawala. Hata hivyo ni mwaka 1901 sheria hizo ziligunduliwa katika mji wa Susa Elamu, nchini Iran.
Inasadikiwa kuwa kwa kutumia diplomasia na nguvu za kijeshi alipanua himaya yake. Utawala wake unajulikana kama zama za dhahabu za Babeli (The golden age of Babylonia).
Ukweli ni kwamba sheria hizi zilifungua njia za uwajibikaji na kutekeleza juhudi za nyakati hizo za kukabiliana na uhalifu. Ingawa kisasa kuna baadhi ya sheria ukisoma unacheka kwa mfano Kanuni ya Hammurabi iliyokuwa inampa haki mtuhumiwa kujirusha mtoni na kama atafanikiwa kufika kwenye ukingo wa pili bila shaka madai yake yakuwa yametupiliwa mbali. Kulikuwa na wazo kuwa miungu imemuokoa mtu asiye na hatia. (Inaonekana dhahiri kwamba Mfalme Hammurabi hakuwa na uelewa wowote kuhusu dhana ya kuogelea!)
Wanahistoria wanamuona mfalme Hammurabi kama mfunguzi njia ya uadilifu. Utawala wake uliutambulisha vema ustaarabu wa Kibabeli. Aliusaidia ufalme wake kuwa na bei elekezi (maximum prices) na pia viwango vya mishahara. Na pia kuwa na kanuni za utoaji kodi. Kanuni hizi ziliwekwa katika lugha ya Kiakadi-(Akkadian). Sheria na kanuni hizi zililenga pia kusaidia yafuatayo– kudhibiti ubambikizaji wa vyesi (false accusation), ushirikina, huduma za jeshi, biashara na ardhi, sheria za familia, tozo kwa huduma mbali mbali (tariffs), mikopo na madeni. Shabaha ya kuwepo mifumo hii ilikuwa kuwasaidia watu wenye nguvu katika ufalme wake kutowadhulumu wasio na nguvu au uwezo. (The strong shall not injure the weak). Lakini miaka takribani hamsini (50) ya utawala wake iliisha kwa himaya yake kupasuka vipande vipande.
Kuna maswali mengine zaidi nimepokea kwa barua pepe. Ninaendelea kufanya utafiti na majibu yako mpendwa msomaji nitakutumia mara tu nitakapomaliza kufanya utafiti huo. Makala ijayo nitajaribu kuchimba kiundani kidogo kuhusu maajabu saba ya dunia. Ambayo kwa sehemu kubwa nafasi ya sanaa na sayansi ya Usanifu majenzi inadhihirika zaidi. Miongoni mwake ikiwa ni Bustani iliyoelea ya Babeli!
Zigurate ni moja ya majengo ya ibada nyakati za Mesapotamia
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top