Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

YA MNYIKA NA UDHAIFU ANAOUSEMA

Na Emmanuel J. Shilatu
Hakika sie Binadamu tumeumbwa na mapungufu mengi yanayotutofautisha sisi (Binadamu) na Malaika. Mapungufu haya tuliyonayo yanawafanya Wanaadamu wengi kutokuweka kumbukumbu vizuri na hata wale wenye kumbukumbu yenye uhauheni wamejikuta wakiingia kwenye mtego huu wa mapungufu ya Mwanaadamu.
Usijipe shida sana ya kutafakuri kwani sipo mbali sana na wakati tulionao ambapo baadhi yetu ndani ya jamii tumefikia hatua ya kunena “hakuna hata jambo jema ambalo Jakaya Kikwete amelifanyia Taifa hili”.Lahaula!
Inanibidi nipatwe na mshangao usio na mfanowe. Jakaya Mrisho Kikwete ninaye mzungumzia ndio huyu huyu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Amekuwa Rais kwa vipindi viwili na huu ni mwaka wake was aba tangu awe Rais.
Huku mitaani tunamoishi walio wengi wanamuona Rais Kikwete kama kiongozi anayewapoteza muda Watanzania kutokana na wao kuhisi ajafanya lolote lile tangu awe Rais. Watu wengineo waliovuka mipaka ya kiupungufu wanamuona Jakaya Mrisho kikwete (JK) kama Rais dhaifu na mzembe kiutendaji.
Hapa sina haja ya kumpiga mtu fumbo wala kijembe na mfano dhahiri wa kauli zilizojaa mapungufu ya hali ya juu ni ile iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Ubungo kupitia tiketi ya Chadema, Mhe John John Mnyika.
Mnyika alisema, “tumefika hapa kwa sababu ya udhaifu wa Rais Kikwete, kwa uzembe wa Bunge, na kwa sababu ya upuuzi wa CCM”. Lahaula!
Watanzania walio wengi walishtushwa sana na kauli hii ya Mnyika inayoonyesha kujaa mapungufu mengi sana ya kimtazamo. Sitakwenda mbali sana bali nitagusia juu ya kile alichokisema “udhaifu wa Rais Kikwete”
Wakati akiisema kauli hii nikapata picha ya haraka haraka ya labda Mnyika alikuwa akizungumzia Udhaifu wa Rais Kikwete katika mapambano dhidi ya ufisadi nchini. Nikaonelea ni bora nimkumbushe haraka za mapambano ya kiufisadi nchini yaliyofanywa na Rais Kikwete tangu aingie madarakani.
Ni kwa kupitia Serikali inayoongozwa na Rais Kikwete tumeshuhudia utekelezaji wa dhahiri wa mapigano dhidi ya ufisadi bila ya kuangalia hadhi, umaarufu wala wadhifa wake. Pia tumeshuhudia viongozi waandamizi na makada wakubwa wa chama wakijiuzulu na wengine kulala rumande na hata kupelekwa mahakamani.
Mnyika aendelee kukumbuka jinsi gani watuhumiwa wa EPA wanavyoendeshwa mahakamani pia tu mashuhuda wa jinsi gani vigogo wa BOT wanavyosota rumande kwa ajili ya kashfa za majengo pacha, uzidishaji wa utengenezaji wa noti EPA.
Jamii pia imeshuhudia watuhumiwa wa nyara za Serikali za kontena lililokuwa na meno ya tembo waliburuzwa mahakamani. Hayo yote yamefanyika ndani ya utawala wa Rais Kikwete huo udhaifu aliokuwa anausema Mnyika unatoka wapi kwa Rais Kikwete? Hapa Mnyika alipotoka kutokana na kushindwa kuweka kumbukumbu zake sawa.
Lakini wakati mie nikiyafikiria hayo, kumbe mitaani walim”passive” (walimtafsiri) Mnyika na kauli yake kuwa Rais Kikwete ni dhaifu katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi. Nikaonelea hapa kuna haja ya kuwakumbusha kipindi cha kwanza cha kuanzia 2005 hadi 2010 cha awamu ya nne ya Rais Kikwete kilivyopiga mzigo wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa chama chao (CCM).
Mwaka 2005 Rais Jakaya Mrisho Kikwete, alikabidhiwa ilani ya uchaguzi, ya CCM ili akainadi kwa watu kupitia ahadi na mara baada ya kushinda urais kwa ushindi wa zaidi ya asimilia 80 alianza kuwatumikia Watanzania wote bila ya kujali itikadi zao za kisiasa. Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa anapambana vilivyo na ujinga, maradhi na umaskini.
Ili Taifa lolote lile Duniani liitwe lina maendeleo ni lazima liwe na watu wenye elimu bora, afya bora na uchumi imara wenye mapato na matumizi y a kuridhisha. Hayo pia yamebainishwa hata kwenye ilani ya uchaguzi ya mwaka 2005.
Nanukuu aya ndani ya ilani hiyo inayosema: “ Chama Cha Mapinduzi kinatambua kuwa rasilimali watu ndiyo nyenzo ku ya maendeleo yote ya nchi , watu walioelimika na wenye afya ndio chombo na lengo la harakati za kukuza uchumi na kuutokomeza umaskini”.
Katika upambanaji dhidi ya adui “ maradhi” kupitia katika sekta muhimu ya afya nchini kuna mengi yamefanyika na yanaonekana waziwazi. Mathalani kulikuwa na ujenzi wa Zahanati mpya ambapo mwaka 2006 kulikuwa na zahanati 4,679 hadi kufika 2009 zilifika 5,422, huku vituo vya afya vikitoka 526 na kuwa 663, pia makazi ya waganga hayakuasahaulika kwani jumla ya nyumba 394 za waganga zilijengwa.
Ongezeko hilo la zahanati na vituo vya afya limekwenda sanjari na ongezeko la madaktari wauguzi na wakunga. Wakati Kikwete akiingia madarakani 2005 kulikuwa na madaktari 3,528 na mpaka leo hii kuna jumla ya 4,502, pia madaktari wasaidizi nao wakiongezeka kutoka 9,028 hadi kufikia 14,017 kwa sasa.
Akina mama nao hawajasahaulika kwani napo kuna ongezeko la idadi ya wauguzi na wakunga kutoka 18,123 hadi kufikia 23,886. Ongezeko hilo na uwepo wa jitihada za dhati toka kwa serikali imeabibisha vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano vimepungua ambapo mwaka 2005 kulikuwa na vifo 158 kwa kila watoto, 1000 na kushuka hadi kufikia 75.
Kwa upande wa mapambano dhidi ya adui “ujinga” napo harakati hazikuwa za kitoto kwani Wanafunzi wa shule za awali wameongezeka kutoka 638,591 kwaka 2005 hadi 825,465 mwaka 2010. Lile wazo la kuwa na shule ya msingi kwa kila kijiji limetimia kwani shule za msingi zimeongezeka kutoka 14,257 mwaka 2005 hadi 15,816 mwaka 2010 ambalo ni sawa na ongezeko la wastani wa shule 1559 hadi iliyopelekea wanafunzi kuongezeka kutoka 7,541,208 hadi 8,419,305.
Upanuzi huu umewezesha asilimia 97 ya watoto wanaostahili kupata elimu ya msingi kuandikishwa na uwiano wa kijinsia wa 1:1 umezingatiwa. Kupitia utawala wa Rais Kikwete umefaulu kuleta mafanikio ya elimu ya msingi nchini. Mathalani mwaka 2004 ni asilimia 36 tu ndizo waliofanikiwa kupata elimu ya msingi ambapo mwaka 2010 zaidi ya asilimia 96 ya watoto wanapata elimu ya msingi. Kwa hili JK, amefanikiwa enzi ya utawala wake.
Mafanikio hayakuishia hapo kwani hata kwa upande wa elimu ya sekondari kimasomaso bado kinaendelea mwaka 2005 kulikuwa na shule 1,202 zilizojengwa tangu uhuru ambapo leo hii kuna jumla ya shule 2,171. Lile lengo la kuwa na sekondari moja kwa kila kata limetimia ambapo pia kuna baadhi ya kata zina shule zaidi ya moja. Ongezeko hilo la shule limewezesha idadi ya wanafunzi wanaosoma sekondari kuongezeka kutoka 524,325 mwaka 2005 hadi 1,638,669.
Idadi ya wanafunzi wanaosoma kidato cha tano imeongezeka kutoka 9,710 kwaka 2005 hadi 33,169 mwaka 2010. Leo hii ukienda vijijini kwenda kusaka wafanyakazi wa ndani (Ma-house girl) hawapo kwani wote wapo mashuleni. Haya ni mafanikio ya dhahiri yasiyostahili kubezwa.
Ila wapo wale magwiji wa upangaji maneno wanaozibeza shule za kata kuwa ni takataka ni muhimu wakatambua ya kwamba wale walioingia elimu ya asilimia 50.1 wanatoka shule za kata na asilimia 10 shule za serikali. Huku asilimia 38.1 ni shule za watu binafsi. Hii ni sehemu tu ya mfano tosha unaodhihirisha umuhimu wa shule za kata kwa jamii.
Idadi ya wanafunzi ni wengi ambao ongezeko hili linabidi liende sambamba na ongezeko la walimu kwa kipindi cha mika mitano serikali imeajari walimu wapya wa sekondari 14,329. Pia nyumba za walimu nazo zimeongezeka ambapo kipindi cha mwaka 2006 hadi 2010 jumla ya nyumba 15,343 za walimu zimejengwa katika hizo nyumba za walimu wa shule za msingi ni 9,910 na nyumba za walimu wa sekondari ni 5,424.
Hali kadhalika serikali imefanikiwa kupanua mafunzo ya walimu katika vyuo vikuu kutoka wahitimu 500 mwaka 2005 hadi jumla ya wahitimu 5,339 hadi kufikia mwaka jana (2009) .
Pia Rais Kikwete alihaidi kujenga chuo kikuu kipya, ameteleza. Leo hii tunajivunia uwepo wa chuo kikuu kipya cha Dodoma almaarufu kama “U-Dom” chuo hiki ni fahari kubwa sana hapa nchini kwani kimebuniwa na kujengwa kwa kutumia fedha zetu wenyewe bila ya msaada kutoka nje. Chuo hiki kitakuwa na uwezo wa kuchukua takribani wanafunzi 40,000 kitakapokamilika ambapo mpaka hivi sasa kina wanafunzi 15,000.
Elimu yetu imekuwa ikitolewa kisayansi zaidi kwani wakati huku chini kwenye ngazi za elimu ya awali, msingi halikadhalika sekondari huku huu (Ngazi ya chuo) napo kumepatiwa ufumbuzi wa hali ya juu kutokana na uwepo wa chuo kikuu hiki kipya cha U-Dom.
Vijana nchini wameendelea kunufaika na mpango wa serikali kugharamia elimu ya juu. Utawala wa Rais Kikwete umefanikiwa kuongeza kiwango cha mkopo nchini, Mathalani mwaka 2005/2006 wanafunzi 42,729 walimufaika kwa kupata mkopo wenye thamani ya Tsh. 56.1 bilioni ambapo mwaka 2009/2010 wanafunzi 69.442 walikopeshwa zaidi ya Tsh. 190 bilioni. Na mwaka huu (2010/2011) kiwango cha mkopo kimeongezeka hadi kufikia Tsh. 237 bilioni. Licha ya changamoto kubwa ya kiwango cha pesa za mikopo lakini kiwango kilichopo ni kikubwa mno na ambacho hakiwezi kufikiwa na nchi yoyote ile ya Afrika Mashariki na Kati. Kama haya siyo mafanikio ni kitu gani hasa?
Pia tumeshuhudia ujenzi wa maktaba mpya takribani 30 za kisasa ukikamilika na hili sasa wanafunzi wanajifunza kwa vitendo zaidi. Pia kuna ongezeko la vyuo kutoka vyuo 24 kwa mwaka 2005 hadi vyuo 34 kwa mwaka 2010.
Hayo yote yamewezekana kutokana na kuenenda sanjari kwa bajeti ya elimu kutoka shilingi 669.5 bilioni mwaka 2005/2006 hadi shilingi 2,045.3 bilioni (zaidi ya Trioni 2) kwa mwaka 2010/2011. Hizi ni jitihada na harakati za kutosha kabisa ambazo zinapaswa kuungwa mkono kwa kuipongeza serikali ya Kikwete kwa ukuaji huu wenye kuleta tija.
Nchi haiwezi kuwa na mazingira mazuri ya kiuchumi iwapo miundombinu ya uchukuzi na usafirishaji itakuwa duni na isiyotosheleza mahitaji.
Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005, serikali iliagaizwa ifikapo mwaka 2010, iwe imekamilsha miradi 17 ya barabara kuu. Kati ya miradi hiyo, 12 imekamilishwa na mitano iliyosalia ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Tangu Rais Kikwete aingie madarakani mnamo Desemba 21, 2005 alikuta barabara zilizojengwa Tanzania tangu iumbwe zilikuwa za urefu wa kilomita 6,000 tu. Lakini alipoingia alikamilisha miradi mipya 54 ya ujenzi wa barabara kadhaa wa kadha kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 11,000 kwa kipindi cha awamu ya kwanza tu. Baadhi yake na urefu wake ni kama ambavyo unavyoonyeshwa kwenye mabano.
Barabara hizo ni ya kuanzia Buzirayombo – Geita (Kilometa 100) , Burizayombo – Kyamyorwa ( kilometa 120) , Singida – Shelui ( Kilometa 110) , Shelui - Igunga – Nzega ( kilometa 108), Nzega – Ilula ( Kilometa 138), Pugu - Kisarawe ( kilometa 3.6) , Dodoma –Manyoni ( kilometa 127), Dodoma - Morogoro ( kilometa 256) .
Barabara nyingine ni kutoka Muhutwe –Kigoma ( kilometa 24) , Nangurukuru - Mbwemkuru – Mingoyo ( kilometa 190), Kyabakari – Butiama ( kilometa 11.4) , Tunduma – Songwe ( kilometa 71), Mkuranga - Kibiti (Kilomita 121 ), na Morogoro - Melela (Kilometa 129).
Hizo ni baadhi tu ya zile barabara ambazo zimekamilika ujenzi wake kwa kiwango cha lami pia kuna barabara ambazo zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Barabara hizo ni ile ya kuanzia Ndungu - Somanga ( kilometa 60) , Tabora - Malagarasi - Uvinza ( kilomeita 364), Masasi - Mangaka ( Kilomita 54) , Arusha – Namanga ( Kilomita 105) , Kagoma –Lusahunga ( Kilomita 154)
Sio hizo nit u bali pia kuna barabara zinazoanzia Mwandinga – Manyovu ( kilomita 60 kila moja ) Singida –Babuti – Minjigu, ( Kilometa 224 ) Tanga – Horohoro ( Kilometa 65) na Manyoni isuna ( kilomita 54)
Katika barabara za mikoa, kilomita 121 zimejengwa kwa kiwango cha lami, kilomita 1,979.4 zimefanyiwa matengenezo katika kiwango cha lami, na kilomita 3,114 zimefanyiwa ukarabati kwa kiwango cha changarawe.
Madaraja 8,385 yalifanyiwa matengenezo ya kuzuia uharibifu, na madaraja 660 kufanyiwa matengenezo makubwa. Madaraja 53 yamejengwa likiwemo Daraja la Mpiji, Daraja la Ruvu na Daraja la Umoja linalounganisha Tanzania na Msumbiji. Mnaotoka maeneo tajwa yalinufaika na miradi hiyo, ni mashahidi wa haya niyasemayo.
Hakika huu ni uthibitisho tosha wa utekelezaji wa ahadi ya ilani ya uchaguzi ambao umefanywa na DK. Kikwete na wale wanaobwabwaja eti serikali ya awamu ya nne yake JK haijafanya lolote, tuwaelewaje? Hawana macho ya kuona ama masikio ya kusikia yaliyotekelezwa ? ama wana lao jambo?
Bado tunaangazia mapambano dhidi ya adui “ umaskini” makusanyo ya ndani katika utawala wa awamu ya nne yaliimarika, ambapo mapato ya Serikali katika kipindi cha miaka mitano iliyopita yameongezeka kutoka shilingi 2,124.8 Bilioni (zaidi ya Triioni 2) kwa mwaka 2005 hadi kufikia Shilingi 4,979.3 Bilioni (zaidi ya Trilioni 4) mwaka 2009, ongezeko ambalo ni sawa na asilimia 134.3.
Hali hiyo imesababisha ule utegemezi wa fedha za kigeni ( misaada) kutoka nje kutoka nje nayo pia kupungua. Mathalani mwaka 2005 Taifa letu katika bajeti yetu ilikuwa tegemezi kwa asilimia 49 ambapo kwenye bajeti iliyopita 2009/2010 utegemezi ule wa awali ulipungua hadi kufikia asilimia 28. haya ni mafanikio ya dhahiri kabisa yanayoonyesha jinsi gani uongozi uliopo ulivyo makini na unatambua kazi na wajibu wao.
Ndani ya utawala wa DK. Kikwete tumeshuhudia mfuko wa udhamini wa wafanyabiashara wadogo na wa kati umeongeza mitaji kutoka shilingi milioni 500 mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 6 mwaka 2010. Hii ina maana ya kuwa kutakuwa na ongezeko kubwa la wafanyabiashara wadogo wadogo almaarufu kama wamachinga na wa kati watakaonufaika na mikopo ya kibishara kwa ajili ya kuanzisha biashara mpya ama kuimarisha zile walizonazo. Kwa kufanya hivyo kwa namna moja ama nyingine atakuwa ameupa kisogo umaskini.
Hapo awali haijawahi kutokea kwa mfuko huu wa wadhamini wa mitaji kwa wafanyabiashara kutuna ( kuongezeka ) kwa kiasi hiki, ila kwa uwepo wa utawala wa Rais Kikwete imewezekana hilo.
Katika utawala wa awamu ya nne kumekuwa na ongezeko la upatikanaji na utumiaji wa pembejeo za kilimo, hususan mbolea, mbegu, miche bora na kuweka mfumo utakaohakikisha upatikanaji wa pembejeo hizo kwa mkulima.
Mathalani katika kipindi cha miaka ya 2005-2010 serikali ya CCM imewezesha idadi ya wakulima wanaopata ruzuku ya mbolea kuongezeka kutoka 750,000 hadi kufikia 2,076,710, asilimia kubwa ya wakulima wamenufaika kwa hili.
Ndugu zangu, ya Ngoswe tumpe Ngoswe mwenyewe na ya Kikwete apewe Kikwete. Kwa mifano hii michache tu imedhihirisha kuwa Rais Kikwete si kiongozi dhaifu kama wanavyomdhani bali ni kiongozi shupavu, mchapakazi na mtekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama chake.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top