Rais Francois Bozize wa Jamhuri ya Afrika ya
Kati amemfukuza kazi Waziri wa Ulinzi nchini humo pamoja na Mkuu wa majeshi
kutokana na kushindwa kuwadhibiti waasi wa Seleka.
Katika tangazo lililotolewa kupitia kituo cha
radio cha taifa nchini humo, Rais Bozize amelikosoa jeshi kwa kushindwa
kukomesha harakati za waasi kuukaribia mji mkuu wa nchi hiyo Bangui kiasi cha
kufikia umbali wa kilometa 75 karibu na mji huo.
Waziri wa ulinzi aliyefukuzwa kazi ni mtoto wa
kiume wa rais Bozize anayeitwa Jean Francis Bozize. Hatua hiyo inachukuliwa
wakati waasi wa kundi la Seleka wakiwa wametangaza kusitisha harakati zao za
kuelekea Bangui.
Kutokana na kuendelea kwa mzozo nchini humo
Umoja wa Mataifa umetoa mwito kwa pande zote mbili kukaa katika meza ya
majadiliano na kutafuta suluhu ya matatizo yao ukisema kuwa uko tayari
kuyaratibu mazungumzo hayo.
Msemaji wa umoja huo, Martin Nesirky,
ameliambia shirikia la habari la AFP kuwa wanaendelea kufuatilia hali ya mambo
katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa umakini mkubwa.
Post a Comment