RAIS wa Jamhuriya Muungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete (pichani) anaanza ziara rasmi ya
Kiserikali nchini Ufaransa leo, Jumamosi, Januari 19, 2013, kwa mwaliko wa Rais
wa Ufaransa, Mheshimiwa Francois Hollande.
Rais Kikwete na ujumbe wake
aliondoka nchini usiku wa kuamkia leo, Jumamosi, kwa ndege ya Shirika la Ndege
la Uswisi kuelekea Ulaya kwa ajili ya ziara hiyo.
Mara baada ya kuwasili
kwenye Uwanja waNdege wa Charles De Gaul mjini Paris leo jioni, Rais Kikwete
ambaye anafuatana na Mama Salma Kikwete atapokelewa rasmi katika Ufaransa kwa
gwaride na kupokelewa na Waziri wa Misaada ya Maendeleo wa Ufaransa, Mheshimiwa
Paschal Canfin.
Kwa mujibu wa ratiba,
kesho, Rais Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na Mama Frannie Leautiera
mbaye ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko Private Fund na baadaye atakutana na Mama Marie
Christine Saragosse, Mtendaji Mkuu wa Redio France International (RFI). Mkutano
huo utafuatiwa na kikao kati ya Rais Kikwete na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi
nchini Ufaransa.
Keshokutwa, Jumatatu, Rais
Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Francois Hollande, Rais wa
Ufaransa kwenye Kasri ya nchi hiyo ya Elysee Palace.
Mazungumzo kati ya Rais
Kikwete na Rais Hollande yatafuatiwa na chakula cha mchana ambako Rais Kikwete
atakaribishwa naWaziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Mheshimiwa Laurent Fabius.
Baada ya chakula hicho cha mchana, Rais Kikwete atakutana na kuzungumza na Bwana
Yves Louis Darricarere, Rais wa Kampuni ya Mafuta ya Kimataifa ya
Total.
Mazungumzo hayo yatafuatiwa
na mazungumzo mengine kati ya Rais Kikwete na Kiongozi wa Madhehebu ya Ismailia
Duniani H.H The Aga Khan na baada ya hapo, Rais Kikwete atakwenda Kasri la
Luxemburg kukutana na kuzungumza na Rais wa Bunge la Seneti la Ufaransa,
Mheshimiwa Jean Pierre Bel.
Usiku wa Jumatatu,
RaisKikwete atakula chakula cha usiku na Rais wa zamani wa Ufaransa, Mheshimiwa
Valery Giscard d’Estaing ambaye ni Mwenyekiti wa Tanzania Wildlife Conservation
Foundation.
Jumanne, Rais Kikwete
atakuwa na siku nyingine yenye shughuli nyingi ambako miongoni mwa mambo mengine
atakutana na kufanya mazungumzo na mabalozi wa Afrika wanaowakilisha nchi zao
katikaUfaransa, na atakutana na Mheshimiwa Abdou Diouf, Katibu Mkuu wa Umoja wa
Kimataifa wa Nchi Zinazongumza Lugha ya Kifaransa na Rais wa zamani wa
Senegal.
Rais Kikwete pia atashiriki
majadiliano kuhusu masuala ya kimataifa yaliyoandaliwa na Taasisi ya Mahusiano
ya Kimataifa ya Ufaransa – Institute Francais Des Relations International (IFRI)
na atakutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya
Kimataifa la Ufaransa (AFD).
Rais Kikwete ataondoka
nchini Ufaransa Jumatano, Januari 23, 2013, kwenda Uswisi ambako atatembelea
Makao Makuu ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mjini Zurich na baadaye kwenda
Davos kuhudhuria mkutano wa mwaka huu wa Shirika la Uchumi Duniani – World
Economic Forum (WEF).
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
19 Januari,
2013


Post a Comment