Rais Mohammed Mursi wa Misri amesema anaunga mkono wito wa raia wa Syria wanaotaka rais Bashar al-Assad (Pichani) ahukumiwe katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu.
Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Marekani CNN, Rais Mursi pia ametabiri kwamba waasi wataweza kuipindua serikali ya Bashar al-Assad katika vita vinavyoendelea nchini Syria.
Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani imetupilia mbali mpango wa amani uliopendekezwa na Assad katika hotuba yake, na kurudia wito wa kumtaka aondoke madarakani.
Wito kama huo wa kumtaka ajiuzulu pia ulitolewa na Umoja wa Ulaya, huku Umoja wa Mataifa ukisema kwamba vita vinavyoendelea kwa miezi 21 nchini Syria vimeangamiza maisha ya watu zaidi ya 60,000.
Wakati huo huo Rais Mohammed Mursi wa Misri amepokea viapo vya mawaziri wapya kumi.
Inaripotiwa kwamba rais huyo anayo matumaini kwamba kuingizwa kwa mawaziri hao katika serikali yake kutaimarisha imani juu ya uchumi wa Misri, huku mazungumzo na Shirika la Fedha Ulimwenguni IMF, kuhusu mkopo yakikaribia.
Uchumi wa Misri umekuwa ukiporomoka tangu mwaka 2011, lilipoanza vuguvugu lililomtimua madarakani rais wa zamani Hosni Mubarak.