VIONGOZI waliokuwa serikalini wakati wa mkataba wa kuzalisha umeme
wa dharula wa Richmond bado wanaendelea kung’ang’aniwa kwenye kashifa
ya kushiriki kwenye ufisadi wa mkataba huo.
Wanaotajwa kushiriki kikamilifu, ni Edward Lowassa aliyekuwa waziri
mkuu. Wengine waliokuwa mawaziri kwa nyakati tofauti katika wizara ya
nishati na madini, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi.
Taarifa zinasema mipango ya siri ndani ya serikali ndiyo ilifanikisha mradi wa kifisadi wa Richmond/Dowans.
“Siyo bure,” ameeleza mwanasheria mmoja jijini Dar es Salaam. “Walikuwa wanawekeza; na sasa wanavuna kwa kuchekelea.”
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya serikali, mambo kadhaa
yalifanywa na serikali “kwa makusudi; bila shaka kwa manufaa ya
baadaye.”
Kwanza, kupinga na kukataa maamuzi halali ya bodi ya tenda ya
TANESCO ambayo ilikataa maelezo na vitambulisho vya Richmond vya
kuombea mkataba wa kuzalisha umeme nchini.
Bodi ya TANESCO ilikatataa maombi ya Richmond mara tatu. Baada ya
kuonyesa ujasiri huo, ndipo serikali ilinyakua madaraka ya Bodi na
kuyatumia ilivyotaka kwa kuipa mkataba Richmond.
Pili, Serikali iliamuru na kushinikza TANESCO kukubali mkataba kati yake na kampuni ambayo tayari waliishaikatalia mara tatu.
Tatu, Serikali ilivunja sheria yake yenyewe (Sheria ya Ununuzi ya
umma ya mwaka 2004) kwa kukalia nafasi ya muhitaji anayepaswa kuamua
iwapo kinachohitajika kununuliwa kina manufaa kwake na kinahitajika kwa
wakati huo.
Nne, serikali kwa ushirikiano na wanasheria ilikubali suala la
uvunjwaji wa sheria ya ununuzi wa bidhaa lijadiliwe katika mahakama ya
usuluhishi ya kigeni badala ya kwanza kumaliza sula hilo katika mahakama
za Tanzania.
Hii ndiyo maana hukumu ya Jaji Emilian Mushi wa mahakama kuu,
kanda ya Dar es Salaam, inasema mawakili wa TANESCO na serikali
waliruhusu, kinyume cha utaratibu, mahakama ya upatanishi ya kimataifa
(ICC) kutafsiri sheria za Tanzania.
Anasema hatua ya mawakili hao, ndiyo sababu ya mahakama yake
“kufungwa mikono” kwenye shauri lililofunguwa na asasi za kiraia kupinga
malipo ya Sh. 111 bilioni kwa kampuni ya Dowans.
“Katika suala hili,” anasema Jaji Mushi, “hoja muhimu ya kisheria
iliyostahili kuletwa hapa mahakamani, ni juu ya hatua ya serikali
kuipora bodi ya zabuni ya TANESCO, kazi ya kutafuta mzabuni, badala yake
kazi hiyo ikafanywa na serikali yenyewe.
Anasema kitendo hicho kilipaswa kujadiliwa na kufanyiwa maamuzi na
mahakama za hapa nchini kwanza, kabla ya shauri hilo kusikilizwa
kwenye mahakama ya usuluhishi.
Jaji anasema na kurejea taratibu kuwa “tathimini ya utoaji zabuni
hufanywa na bodi ya zabuni ya TANESCO, sio serikali wala wizara ya
nishati na madini.”
Hayo yamo katika hukumu ya Jaji Mushi ya kurasa 89 ambayo gazeti hili linayo.
Kwa mujibu wa sheria ya manunuzi ya umma, kifungu cha 31, siyo
serikali wala wizara ya nishati na madini, aliyekuwa na mamlaka ya kutoa
zabuni ya kufua umeme.
Anasema kwa kuzingatia sheria hiyo, mahakama yake imehuzunishwa na kitendo cha serikali kujipa mamlaka yasiyoihusu.
Hatua ya serikali kuipora kazi ya kutoa zabuni bodi ya Tenda ya
TANESCO ilikwenda sambasamba na kurejeshwa kundini kampuni ya Richmond,
ambayo bodi ya tenda ya TANESCO tayari ilishaindoa.
Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja huku baadhi ya walioshiriki
kuangamiza nchi kwenye mkataba huo wakihaha kujisafisha; huku Jaji
Mushi akisema, “Kama siyo serikali kujiingiza katika mchakato wa zabuni,
kusingekuwa na kashifa.
Jaji Mushi anasema, “Jambo la kushangaza ni pale terehe 4 Aprili
2006, serikali ilipoitaka TANESCO kuziita kampuni nane ambazo awali
ziliomba kupewa zabuni na kuzifanyia tathmini upya ikiwamo Richmond,
ambayo tayari ilithibitika kutokuwa na uwezo wa kutekeleza mradi huo.”
Mara baada ya serikali kupora mamlaka ya bodi ya zabuni, 30 Machi
2006, iliamua kutangaza upya zabuni hiyo kwa njia ya “International
shopping procurement.”
Jaji anasema, “…kwa kutathmini uhalisia na historia ya maombi
haya, ukweli ni kuwa jambo hili ni gumu na linaumiza sana. Ugumu wa
jambo hili ni kwamba, Richmond haikuwa na zana za kazi, wafanyakazi na
uzoefu wowote katika miradi kama hiyo.”
Anasema, “Ni jambo la kushangaza, serikali na mawikili wake
wanakubali jambo hili la kuvunjwa kwa sheria ya manunuzi ya umma kwa
kufanya lijadiliwe kwenye mahakama ya usuluhishi.”
“Hatua ya mawakili wa serikali kuridhia mawakili wa Uingereza
kujifungia kwenye hoteli ya Kilimanjaro-Kempinsk kutafasri sheria za
Tanzania, ndiyo msingi wa kesi iliyofunguliwa na wanaharakati kupinga
kusajiliwa kwa tuzo ya Dowans kugonga mwamba,” ameeleza mwanasheria
mmoja jijini Dar es Salaam.
Ushahidi ulioletwa mahakamani, anasema Jaji, umethibitisha kwamba
bodi ya zabuni ya TANESCO ilikataa kutekeleza maelekezo ya serikali ya
“kuziita tena kampuni ambazo awali hazikupitishwa ikiwamo Richmond.”
Katika uamuzi wake, Jaji Mushi ametupilia mbali maombi
yaliyowasilishwa tarehe 27 Augosti 2011 na Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) kupinga malipo kwa kampuni ya Dowans Holdings SA (Costa Rica)
na Dowans Tanzania Ltd.
Maombi hayo yalikuwa ni ya kupinga maamuzi yaliyotolewa na
mahakama ya kimataifa ya usuluhishi katika kitengo cha biashara ambayo
iliamuru makampuni ya Dowans kulipwa fidia ya Sh. 94 bilioni na TANESCO
kutokana na hatua ya kuvunja mkataba wake.
Baada ya kuvunjwa kwa mkataba huo, 14 Septemba 2008 kampuni ya
Dowans ilifungua shauri la madai katika mahakama ya kimataifa ya
usuluhishi wa migogoro ya kibiahara (ICC), kupinga kuvunjwa kwa mkataba
kati ya kampuni ya Richmond Development Company (LLC) na TANESCO.
Kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya mkataba wa TANESCO na Dowans wa 23
Juni 2006, pande hizo mbili zilikubaliana kutumia sheria za mahakama ya
ICC, pale panapotokea migogoro ya kisheria; kuheshimu maamuzi
yatakayotolewa na mahakama hiyo na maamuzi hayo ndiyo yatakuwa ya
mwisho.
Kulingana na kifungu cha 28 (6) cha kanuni ya mahakama hiyo,
maamuzi ambayo yatatolewa na mahakama hiyo yatakuwa ni ya mwisho na
yatazifunga pande hizo na hayatakatiwa rufaa.
Wakati hayo yakiendelea, MwanaHALISI limeelezwa kuna uwezekano
mkubwa wa Dowans kuwa tayari imeshalipwa sehemu ya fedha inayodai.
Kiasi kinachoelezwa kwamba kinaweza kuwa kimelipwa ni dola za
Marekani 5.1 milioni (karibu Sh. 8. bilioni) ambazo ziliwekwa dhamana
kwenye mahakama ya Uingereza.
Mwanasheria mashuhuri nchini, Tundu Lissu amesema, “Kama serikali
imeweka fedha hizo kama dhamana kwenye mahakama ya Uingereza, basi
hakuna kinachoweza kuwazuia Dowans kulipwa fedha hizo.”
Lissu alikuwa akijibu swali la mwandishi wa gazeti hili aliyetaka
kujua iwapo “fedha iliyowekwa dhamana na Tanessco yaweza sasa
kuchukuliwa na Dowans kwa kuwa shauri limemalizika mahakama kuu ya
Tanzania.”
Amesema, “Kama fedha hizo ziliwekwa kama dhamana, basi hakuna njia
ambayo TANESCO wanaweza kuzuia kuchukuliwa. Hapa labda kama kuna
shauri jingine limefunguliwa Uingereza. Lakini kama shauri lenyewe ndiyo
hilo la Dar es Salaam, mhh, hiyo hela kaka imeshakwenda.”
Mahakama ya ICC iliamua kutoa tuzo kwa Dowans kwa kigezo kwamba
pande hizo mbili zilijifunga kisheria kutatua matatizo ya kisheria
kupitia mpatanishi chini ya mahakama hiyo.
Kwa upande mwingine, Jaji Mushi anasema rekodi zilizopo
zinamuonyesha Rostam Aziz, mfanyabiashara na swahiba wa karibu wa Rais
Jakaya Kikwete kuwa “anahusika katika kampuni ya Richmond.”
Rostam alisafiri hadi Houston, Texas Marekani, tarehe 7 Oktoba
2006 kukutana na wawakilishi wa kampuni ya Richmond ambapo makubaliano
yalifanyika ya kuidhamini kampuni hiyo.
Ni Rostam Aziz, Jaji Mushi anasema aliyetumia madaraka yake
kushinikiza uhamishwaji wa mkataba kutoka Richmond kwenda Dowans;
jambo ambalo lilithibitishwa kwenye mahakama ya ICC na mmoja wa
mashahidi wa Dowans.
source: MwanaHalisi
VOA Express
2 hours ago
Post a Comment