Na: Albert Sanga
Miaka ya hivi karibuni dhana inayohusu ujasiriamali imeenea kwa kasi kubwa sana miongoni mwa wana jamii. Kwa sasa kila kona tunasikia ujasiriamali, makanisani , mitaani, vyuoni na katika mikutano ya kisiasa kunahubiriwa ujasiriamali. Hata hivyo kuna kibwagizo kinajirudia kila zinapotajwa changamoto za ujasiriamali; ukosefu wa mitaji!. Dhana ya ujasiriamali imepata kushika kasi kutokana na nchi yetu kujikuta inajisalimisha katika mfumo wa kibepari pasipo kupenda wala kutoa taarifa. Utandawazi umeyasababishia mataifa masikini kama Tanzania kurukia ubepari bila kuagana na...
nyonga zao. Nyonga ninazomaanisha hapa ni mifumo ya kiuchumi iliyokuwepo nap engine iliyobuniwa na wazalendo wa mataifa husika; Tanzania tukiwa na ujamaa wetu ulioasisiwa na mwalimu Julius Nyerere.
Inafaa sana watanzania wote kufahamu kuwa maisha ni magumu. Na ugumu wa maisha haujaanza jana wala miaka ya karibuni, bali tangu uwepo wa dunia hii maisha ni magumu. Wengi huwa hawataki kuukubali ukweli huu ‘kama ulivyo’.
Ndio maana utawasikia wakihuzuniaka, kung’ung’unika na kulalamika, kana kwamba waliambiwa maisha ni rahisi. Saa unapoukubali ukweli ya kuwa maisha ni magumu, ndio wakati ambao maisha hayawi magumu tena! Ndio! Kwa sababu ukijua maisha ni magumu ni lazima utaishi kwa nidhamu kubwa, na nidhamu ndio msingi namba moja wa kutatua matatizo yote katika maisha.
Ukiwa na nidhamu kidogo utatatua matatizo machache, na ukiwa na nidhamu nyingi utatatua matatizo mengi! Nidhamu inahusisha kufanya kazi kwa bidii, kuwapenda na kuwafikiria wengine, kuheshimu sheria za nchi na kila namna ya jema unalolijua.
Ukiona unalalamika kuwa maisha ni magumu, rejea katika fikra zako, huenda bado hakujafanyika mapinduzi! Ukiona unaukubali ukweli ya kuwa maisha ni magumu na wakati huo huo huna nidhamu ama una nidhamu chache, basi ujue kuwa hujaukubali ukweli wote wa maisha kuwa ni magumu, !
Ujasiriamali unawagusa watu wa kada na umri mbalimbali, vijana wazee na hata watoto. Kwa kuwa kundi la vijana [wasomi na wasio wasomi] ndio linaloongoza sana kwa kutegemewa kwa uzalishaji nitaongelea hilo. Ujasiriamali kwa ujumla ni dhana ambayo ili kukubalika kikamilifu kunahitajika mapinduzi makubwa sana ya fikra kwa vijana kuliko elimu ya kawaida. Fikra za kuwatazama wajasiriamali waliofanikiwa na kutoa visingizio kuhusu mafanikio yao ni fikra zenye matege na ukilema na hizo kamwe haziwezi kutufanya tukafanikisha kujikwamua kiuchumi.
Vijana ambao hawana elimu wanalalamika kuwa hawana elimu ndio maana maisha yao ni magumu ama yanasumbua, nao vijana ambao wanaelimu katika fani na viwango mbalimbali wanalalamika kuwa ajira hamna. Unapogusia suala la ujasiriamali katika kundi hili la vijana wenye elimu, utakisikia kilio ambacho kimekuwa kama wimbo sasa nacho ni “ukosefu wa mitaji”. Kwa ufupi ni kuwa vijana wenye elimu wanalia kutokana na ugumu wa maisha na vile vile vijana wasio na elimu wanalia. Wasio na elimu wanawatamani wenye elimu, na wenye elimu wanaitamani mitaji.
Kutokana na hali hii utagundua kuwa tatizo linaliwakabili vijana wengi wa Tanzania katika kujikwamua kiuchumi sio mitaji wala ukosefu wa elimu bali kuna tatizo la kifikra hapa. Ili kijana aweze kufanikiwa kubuni na kuanzisha mradi anatakiwa aamini kuwa kujiajiri kuna tija kubwa sawa sawa na kuajiriwa. Kwa sababu ni mara chache sana mtu anaweza kuwa tajiri kwa kutegemea mshahara wake!
Kwa bahati mbaya katika jamii kuna utamaduni uliojengeka sana katika jamii zetu wa kuamini sana kuajiriwa. Hata familia nyingi zinaposomesha watoto wao zinawasisitiza wasome kwa bidii ili wafaulu na kupata kazi zenye mishahara mikubwa. Utamaduni huu umefifisha hamasa na moyo wa kupenda kujiajiri miongoni mwa vijana wetu hasa waliopo katika mifumo ya kielimu..
Hebu tumtafakari kijana anayesema kuwa amekosa mtaji ndio maana ni masikini. Ni dhahiri kuwa wengi wa vijana mara kwa mara huwa wanabahatika kupata, shilingi elfu ishirini mifukoni mwao. Kijana akitumia ubunifu, kwa mfano anaweza kununua kuku wawili wa kienyejji wa kufugwa, kila mmoja shilingi elfu saba, jumla wawili ni elfu kumi na nne.
Hawa wakifugwa kwa miezi mine wanaweza kutotoa kuku kumi. Baada ya mwaka mmoja kuku wanaweza kufikia sitini! Kuku sitini ukiwauza kwa shilingi elfu saba kila mmoja anakuwa na zaidi ya laki nne. Tayari huyu anakuwa ameanza safari ya kujikwamua na umasikini!
Vijana wa Tanzania ambao wanapambana na ugumu wa maisha wanahitaji sana kupokea semina, shuhuda na uzoefu kutoka kwa wajasiriamali wa kitanzania ambao wamefanikiwa. Kama semina, warsha na makongamano yatakuwa yakitumia dhana pekee za vitabuni tutarudi kule kule katika mfumo tegemezi, ambao unaonekana sio halisi bali ni wa kujibia mitihani. Tunawahitaji wajasiriamali vijana kuandika vitabu vinavyoeleza namna walivyofanikiwa ili kutia hamasa na kubadilisha fikra za vijana wengine ambao wanasua sua kujikita katika ujasiriamali kwa visingizio vya kukosa elimu na kukosa mitaji.
Ujasiriamali unahusisha kujenga fikra madhubuti za kujitegemea na kutegemewa. Kwanza ni kuwa akili ya mtu inapanuka na kuwaza zaidi na zaidi kutegemea na mahitaji yaliyopo katika fikra. Ukiwaza kupata fedha kidogo ya kujikimu ubunifu wa akili yako utajikita katika upatikanaji wa fedha hiyo kidogo! Ukiwaza kuwa na fedha nyingi akili yako inapanuka kuwaza namna ya kupata fedha nyingi. Lengo langu hapa si kusisitiza vijana kuwa na fedha nyingi, isipokuwa ni kuweka hamasa kwa vijana kuhusu ujasiriamali na namna ya kujikwamua kiuchumi.
Ni vema vijana wote wafahamu ya kuwa “fedha ni mawazo”. Kama fedha ni mawazo basi kujikwamua kiuchumi ni mawazo pia. Kama ni suala la kuwaza, kwa nini asiye na elimu asiwaze? Kama ujasiriamali unaanza na mawazo, kwa nini wenye elimu walilie mitaji? Sikatai kuwa mitaji ni suala la msingi katika ujasiriamali, lakini ifahamike kuwa uthubutu wa kuanza na kujaribu wazo hata kwa sehemu ndogo ndio msingi wa mafanikio ya mjasiriamali yeyote.
Nchi ya Tanzania ina ajira na fursa nyingi sana za kiuchumi za kumtosha hata mtoto atakayezaliwa kesho! Sioni sababu ya muhitimu wa darasa la saba kukosa ajira, kwa nini muhitimu wa kidato cha nne na sita wakose kitu cha kufanya chenye kuwakwamua kiuchumi katika nchi tajiri kama Tanzania? Kwa wale ambao ni wahitimu wa vyuo vya kati na vya elimu ya juu sioni haja ya kuwaandikia kwa sababu inatosha sana kwao kutengeneza ajira kwa wengine.
Tatizo jingine linalowasibu vijana wengi wa Tanzania hata wanashindwa kupoka (Seizing) fursa za kijasiriamali na fikra potofu za kutaka kuanza na mafanikio. Kama ni kijana msomi anawaza kuanza na kampuni lenye mtaji wa mamilioni. Yatatoka wapi mamilioni bila kuanza na kudogo? Kwa wale ambao hawana elimu kubwa wengi wamevia kimawazo kwa kuota kuokota fedha ama kuokota elimu.
Kama ulikosa elimu haupaswi kulalamika wala kung’ung’unika kwa sababu huko ni kupoteza muda bado unayo nafasi kubwa sana ya kufanikiwa. Fikra za kupata vya bure bila kuhangaika ndio zinapelekea watanzania wengi kujiingiza katika michezo mingi ya ‘kibahati nasibu’ kwa matarajio kuwa watatoka! Cha ajabu ni kuwa michezo mingi inayohusu bahati nasibu ama mingineyo inawapotezea fedha badala ya kuwasaidia, hapa yanahitajika mapinduzi ya kifikra.
Maisha bora na ya uhakika kwa vijana yanawezekana sana ikiwa kutafanyika mageuzi makubwa katika sekta binafsi, ujasiriamali. Na ili ujasiriamali ufanikiwe na kufanywa na vijana kwa uhakika ni lazima vijana wote wakubali kufanya mapinduzi ya fikra zao za kitegemezi. Tukisema ujasiriamali hatumaanishi ujasiriamali wa kujikwamua wewe kijana peke yako, bali tunagusa pia katika utanuzi wa fikra za kuanzisha makampuni, huduma na bidhaa mbalimbali zenye ubunifu mpya kwa kuvitumia vipaji kikamilifu
Watanzania tunahitaji ushindi wa kiujasiriamali!
stepwiseexpert@gmail.com
, 0719 127 901
Post a Comment