Tiketi
kwa ajili ya pambano la kimataifa la kirafiki kati ya Tanzania (Taifa
Stars) na Cameroon (Indomitable Lions) zinaanza kuuzwa kesho (Febaruari 5
mwaka huu) katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Viingilio
katika pambano hilo litakalochezwa Jumatano (Februari 6 mwaka huu)
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 jioni ni sh. 5,000 (viti
vya kijani), sh. 7,000 (viti vya bluu), sh. 10,000 (viti vya rangi ya
chungwa), sh. 15,000 VIP C, sh. 20,000 VIP B na sh. 30,000 VIP A.
Vituo
vitakavyouzwa tiketi hizo kuanzia saa 2 asubuhi ni Shule ya Sekondari
Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa
Samora/Ohio, Oilcom Ubungo, Dar Live Mbagala na kituo cha mafuta
Buguruni.
Vilevile tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mechi, na milango itafunguliwa saa 8 kamili mchana.
Wakati
huo huo, kundi la kwanza na la pili la wachezaji wa Cameroon tayari
limetua jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi dhidi ya Tanzania (Taifa
Stars) itakayochezwa keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Cameroon
chini ya Kocha Jean Paul Akono itafanya mazoezi kesho saa 11 jioni
Uwanja wa Taifa. Nayo Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium
Lager yenyewe itafanya mazoezi Uwanja wa Taifa leo saa 11 jioni.
12,984 WASHUHUDIA SIMBA, JKT RUVU ZIKITOKA SARE
Watazamaji
12,984 walikata tiketi kushuhudia mechi ya namba 99 ya Ligi Kuu ya
Vodacom iliyochezwa jana (Februari 3 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Viingilio
katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh.
20,000 ambapo jumla ya sh. 73,532,000 zilipatikana. Kila klabu ilipata
mgawo wa sh. 17,443,752.45 ambapo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
iliyolipwa ni sh. 11,216,745.76.
Mgawo
mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 8,869,704.64,
tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 5,321,822.78, Kamati ya Ligi
sh. 5,321,822.78, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh.
2,660,911.39 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA)
sh. 2,069,597.75.
UCHAGUZI FRAT SASA KUFANYIKA FEB 14
Uchaguzi
wa viongozi wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT)
uliokwama kufanyika mara mbili, sasa utafanyika Februari 14 mwaka huu
mjini Morogoro.
Wajumbe
wa Mkutano Mkuu wa FRAT wanatakiwa kufika Morogoro siku moja kabla ya
tarehe ya uchaguzi. Pia wapiga kura na wagombea wanatakiwa kulipia ada
za uanachama kwa mwaka 2013 kabla ya uchaguzi.
Wagombea
ni Army Sentimea na Said Nassoro (uenyekiti) wakati wanaoomba nafasi ya
Makamu Mwenyekiti ni Juma Chaponda, Juma Mpuya na Tifika Kambimtoni.
Abdallah
Mitole, Charles Ndagala na Hamis Kisiwa wanawania ukatibu mkuu, nafasi
ya Mhazini inagombewa na Jovin Ndimbo. Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni Kamwaga Tambwe wakati
nafasi ya uwakilishi wanawake yupo Isabela Kapera.
Wagombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Emmanuel Chaula na Samson Mkotya.
Post a Comment