Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa
---
Katika wiki za hapa karibuni kumekuwa na mijadala na
mazungumzo mengi kuhusu mikakati ya maendeleo ya mikoa ya Kusini hususan Mkoa wa
Mtwara. Mazungumzo hayo yamekuwa na lugha kali na yameambatana, hatimaye, na
maandamano na mikutano ya hadhara. Kiini chake ni matumizi ya gesi
iliyogunduliwa mkoani kwa ajili ya miradi au mipango ya maendeleo ya mkoa huo,
mipango iliyopo mbioni kutekelezwa au inayotarajia kutekelezwa. Mwenendo wa
mazungumzo, maandamano na mikutano ya hadhara imeelekea kuashiria shari na
kuvunjika kwa amani.
Aidha vituko na kauli hizo zimekaribia kujenga
kutokuelewana kati ya Viongozi wa Vyama vya Siasa na Serikali, kati ya wanachama
wa vyama vya siasa na viongozi wao, kati ya wananchi na viongozi wa
Serikali.Mtafaruku huu haufai kuachwa uendeleee na kutishia usalama. Mipango ya
maendeleo siyo Siri. Mikakati na mbinu za Utekelezaji wake siyo Siri. Maelezo
yake mazuri yanaweza kutolewa yakadhihirisha namna na kasi ambayo raslimali
zitawanufaisha wananchi wa eneo zilizomo na Taifa zima.Utekelezaji wa miradi
unategemea masharti kadhaa, k.m. Uwapo wa mitaji na teknolojia.Lakini pia
mwekezaji, awe Serikali au Sekta binafsi, atataka iwepo hali ya utulivu na
usalama wa watu, hali na mali.Hayo yatadaiwa na wawekezaji wa ndani na wa nje.
Vurugu, fujo, vitisho havivutii uwekezaji.
Nikiwa Mwana Mtwara na raia mwema mpenda nchi,
nimefadhaishwa sana na matukio haya ya siku za karibuni Mtwara.Kwa sababu hiyo
natoa wito kwa wadau wote wa maendeleo ya Mtwara kusitisha harakati hizi na
maandamano na mihadhara na badala yake wajipange KUKAA PAMOJA katika meza
moja, kupitia historia,kutathmini mipango, kuchambua kwa kina mikakati ya
utekelezaji wake,na hatimaye kufikia muafaka wa Ujia wa maendeleo. Fujo,
vitisho, kupimana nguvu na malumbano kamwe si masharti ya maendeleo. Mazungumzo
yataboresha sera, ya uwekezaji ya mkoa na nchi.
Linalowezekana leo lisingoje kesho.
Benjamin William Mkapa
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania
Post a Comment