Na Mwandishi
Wetu
Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imetoa mwongozo wa jinsi ya kuwapata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba
yatakayoendeshwa na Tume na kujadili rasimu ya Katiba kuanzia mwezi Juni mwaka
huu na kuwataka wananchi wanaopenda kuwa wajumbe kuwasilisha majina yao kwa
Maafisa Watendaji wa Vijiji au Mitaa kwa Tanzania Bara na kwa Sheha kwa Zanzibar
kati ya tarehe 08 hadi 20 mwezi Machi mwaka huu
(2013).
Kutolewa kwa mwongozo huu
kunafuatia kuchapishwa kwa rasimu yake mwanzoni mwa mwezi huu ili kupokea maoni
ya wadau mbalimbali kabla ya kuuboresha. Wadau mbalimbali zikiwemo asasi za
kiraia na vyama vya siasa vilitoa maoni yao.
Kwa mujibu wa mwongozo huo
ambao umechapishwa katika magazeti mbalimbali ya leo (Feb. 27, 2013), baada ya
kuwasilisha majina yao, orodha ya majina yote itawekwa kwenye maeneo ya wazi na
mbao za matangazo katika Ofisi za Vijiji au Mitaa kwa Tanzania Bara na maeneo ya
wazi kwenye Shehia kwa Zanzibar kati ya tarehe 22 hadi 28 Machi mwaka
huu.
“Kwa Tanzania Bara, Vikao vya
Vijiji au Mitaa vya kuwachagua kwa kuwapigia kura za siri wananchi wanne kuwa
Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba vifanyike kati ya tarehe 30 Machi 2013 hadi 03
Aprili, 2013,” inasomeka sehemu ya 7 ya mwongozo huo ambao pia unapatikana
katika tovuti ya Tume (www.katiba.go.tz).
Kwa upande wa Tanzania Bara,
mwongozo huo unaongeza, kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata cha
kuwachagua wajumbe wanne kutoka miongoni mwa Wananchi waliopigiwa kura na
Mikutano Mikuu ya Vijiji au Mitaa kitafanyika kati ya tarehe 05 mwezi Aprili
2013 hadi 09 Aprili mwaka huu (2013).
“Kwa Tanzania Bara, majina ya
Wajumbe wanne waliochaguliwa na Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata,
yawasilishwe kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa husika kati ya
tarehe 13 Aprili, 2013 hadi 17 Aprili, 2013,” imeongeza sehemu ya mwongozo
huo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa
mwongozo huo, mchakato huo wa kuwapata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kwa mkoa wa
Dar es Salaam umepangiwa tarehe tofauti.
“Kwa mkoa wa Dar es Salaam,
Vikao vya Mitaa vya kuwapigia kura ya kuwapendekeza wajumbe wanane wa Mabaraza
ya Katiba ya Wilaya vifanyike kati ya tarehe 30 Machi, 2013 hadi 03 Aprili,
2013,” inasomeka sehemu ya mwongozo huo na kuongeza:
“Vikao Maalum vya Kamati za
Maendeleo za Kata vya kuwachagua wajumbe wanane kutoka miongoni mwa wananchi
waliopigiwa kura na Mikutano Mikuu ya Mitaa vifanyike kati ya tarehe 05 Aprili,
2013 hadi 09 Aprili, 2013,” imefafanua Tume katika mwongozo
wake.
Kwa mujibu wa Tume hiyo, Majina ya Wajumbe
wanane waliochaguliwa na Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata, yatapaswa
kuwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa husika kati ya
tarehe 13 Aprili 2013 hadi 17 Aprili, 2013.
Kuhusu
Zanzibar
Kuhusu Zanzibar, Tume kupitia
mwongozo wake, imeagiza kuwa Vikao vya Shehia vya kuwachagua kwa kuwapigia kura
za siri Wananchi watatu kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya vifanyike
kati ya tarehe 30 mwezi ujao (Machi, 2013) hadi mwezi tarehe 03 Aprili mwaka huu
(2013).
“Majina ya Wajumbe watatu,
waliochaguliwa na Mikutano ya Shehia, yawasilishwe kwa Mkurugenzi wa Baraza la
Manispaa, Katibu wa Halmashauri ya Mji au Wilaya ilipo Shehia hiyo kati ya
tarehe 13 Aprili 2013 hadi 17 Aprili, 2013,” imesema Tume kupitia mwongozo huo
na kufafanua zaidi:
“Majina ya watu wote
waliochaguliwa kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, pamoja na majina ya
Madiwani wote wa Mamlaka ya Serikali za Mtaa husika yawasilishwe kwa Katibu wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kutumia Fomu maalum iliyoandaliwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kwa madhumuni hayo kwa njia ya nakala tete (soft
Copy) na nakala
mango (hard
copy) kati ya tarehe 25 Aprili 2013 hadi 30 Aprili, 2013,” imefafanua
Tume.
Mabaraza ya Katiba
yatakayoundwa kwa mujibu wa mwongozo huo yataendeshwa katika kila wilaya na
halmashauri ya Mji na Manispaa kuanzia mwezi Juni hadi Agosti mwaka huu. Katika
mikutano hiyo ya mabaraza, Tume itawasilisha rasimu ya Katiba iliyotokana na
maoni ya wananchi pamoja na kutoa ufafanuzi wa hoja zitakazojitokeza. Baada ya
mikutano ya Mabaraza ya Katiba, Tume itawasilisha rasimu ya Katiba katika Bunge
Maalum.
Post a Comment