Wazazi mkoani Lindi
wametakiwa kusimamia elimu ya watoto wao kwa kuhakikisha kuwa wanaenda shule,
wanakagua madaftari yao na kuwarekebisha pale ambapo wamekosea kwa kufanya
hivyo watafaulu vizuri katika masomo na kufanikiwa kimaisha kwani elimu ni
msingi wa maendeleo.
Wito huo umetolewa jana na
mke wa Rais Mama Salma Kikwete kwenye kilele cha sherehe za maadhimisho ya miaka
36 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizofanyika kimkoa katika kata ya
Rondo wilaya ya Lindi vijijini.
Mama Kikwete ambaye pia ni
Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM taifa toka wilaya ya Lindi mjini alisema kuwa
maendeleo ya elimu si mazuri katika mkoa huo hivyo basi kina baba washirikiane
na wake zao kuhakikisha kuwa watoto wanahudhuria shule na kufanya vizuri katika
masomo yao.
“Ninyi watoto nawasihi
msome kwa bidii mkumbuke kuwa huu si wakati wa mtoto kukatisha masomo kwa ajili
ya kupata ujauzito kwani mkiwa na elimu kutakuwa na uhakika wa kupatikana kwa
wataalamu mbalimbali katika mkoa huu na kutatua tatizo la kutokuwa na wataalamu
ambalo limedumu kwa muda mrefu”, alisema Mama Kikwete.
Aidha Mjumbe huyo wa
Halmashauri kuu ya CCM taifa aliwataka wanawake kutosubiri nafasi za upendeleo
za viti maalum bali wagombee nafasi mbalimbali za uongozi ndani na nje ya chama
ili wafike katika ngazi ya maamuzi na kuachana na fikira kuwa wao hawawezi
kumwaga sera wakati wa uchaguzi.
Alimalizia kwa kuwataka
wakazi wa mkoa huo kudumisha amani, upendo na utulivu, kufanya kazi kwa
bidiii, maarifa na kujituma, wakulima walime kilimo cha kisasa ambacho
kitawafanya wavune mazao mengi zaidi pia wafanyakazi watumie muda wa kazi
kufanya kazi na kuwahudumia wananchi.
Mama Kikwete pia alifungua
jengo la ofisi ya CCM lenye thamani ya shilingi milioni 35 ambalo limejengwa na
Mbunge wa jimbo la Mtama ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa Benard Membe.
Waziri Membe alisema kuwa
jengo hilo lina vyumba sita ambavyo ni ofisi za jumuia zote za chama hicho
ambazo ni Vijana, Wanawake, Wazazi, pia kuna ofisi za Mbunge, Mjumbe wa NEC na
chumba cha mikutano.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa CCM wa mkoa huo Ally Mtupa aliwataka wanachama wa chama hicho kuwa na
mahusiano mazuri baina yao na viongozi wanaowaongoza. Wakisikia jambo wasiwe na
papara ya kukimbilia kuandamana bali wafanye upelelezi kwanza na wakishabaini
ukweli ndipo wachukue hatua.
Mtupa alisema, “Hivi sasa
kuna watu wanapita mitaani na kupotosha ukweli kuwa Serikali yetu haijaleta
maendeleo, wamesahau kuwa wanatembea katika barabara na kutibiwa katika
Hospitali zilizojenga na CCM, tunawaomba watu hawa wawaheshimu viongozi
wanaotawala kwani hata vitabu vya dini vinasisitiza umuhimu wa kuwatii viongozi
waliopewa mamlaka ya kutawala”.
Sherehe hizo zilienda
sambamba na mchango wa matembezi ya mshikamono ambapo zaidi ya shilingi milioni
mbili zilipatikana, ufunguzi wa ofisi za CCM, ufanyaji wa usafi wa mazingira ,
kuwatembelea wagonjwa mahospitalini, utoaji wa kadi kwa wanachama wapya ambapo
wanachama wa kawaida 286 , jumuia ya wazazi 63 na kutoka vyama vya upinzani 23
walipewa kadi.
Post a Comment