Dar
es Salaam. Ikulu imetoa kauli inayopingana na ile ya Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu hatima ya Mkurugenzi wa Kitengo cha
Itifaki cha wizara hiyo Anthony Itatiro, ambaye anatuhumiwa pamoja na maofisa
wengine wa wizara hiyo kupanga njama ya kuchota Sh3 bilioni baada ya kubuni
safari feki ya Rais.
Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Sefue aliliambia gazeti hili jana kuwa Serikali imeshachukua hatua
za kinidhamu dhidi ya Itatiro kwa kumvua hadhi ya ubalozi na kutenguliwa na
nafasi yake ya ukurugenzi wa Itifaki.
Hata hivyo, kauli ya
Sefue ambaye ndiye Mkuu wa Utumishi serikalini, inapingana na ile iliyotolewa
juzi na Naibu Waziri katika wizara hiyo, Juma Mahadhi ambaye alikaririwa akisema
kwamba Itatiro bado yuko kazini na kwamba suala lake lilikuwa likisubiri uamuzi
wa Rais Jakaya Kikwete.
Mahadhi
alitoa kauli hiyo alipobanwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje,
Edward Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli aliyehoji hatima ya tuhuma hizo
wakati wa kikao cha kamati hiyo.
Hata hivyo, jana Sefue
akizungumza na Mwananchi alisema: “Uteuzi wake umetenguliwa baada ya kutokea
hilo tatizo, hatua ya kinidhamu tuliyomchukulia ni kumwondoa katika nafasi hiyo
pia hata ule wadhifa wake wa ubalozi pia tumemwondolea.”
Sefue alisema nafasi ya
Mkuu wa Itifaki iliyokuwa ikishikiliwa na Itatiro hivi sasa anakaimu mtu
aliyemtaja kuwa ni Andi Mwandemba na kwamba hatua hizo zimechukuliwa mwaka huu,
lakini akasema hakumbuki tarehe.
Alipoulizwa hatua zaidi
ambazo atachukuliwa kigogo huyo alijibu; “Itatiro atatafutiwa kazi nyingine
ambayo ni ya chini zaidi kuliko aliyokuwa nayo awali, yaani cheo cha chini
kuliko alichokuwa nacho.”
Sefue alieleza kuwa
utaratibu uko wazi kwamba linapogundulika jambo ambalo siyo la kawaida hatua za
kinidhamu ni lazima zichukuliwe.
“Inapogundulika kuwa
mambo hayaendi vizuri hatua za kinidhamu lazima zichukuliwe ili iwe funzo kwa
wengine,” aliongeza Sefue, ambaye ni Balozi wa zamani wa Tanzania kwenye Umoja
wa Mataifa.
Alipoulizwa kama ni
hatua stahili kwa kumvua wadhifa mtu anayehusishwa katika njama za kutaka
kuchota kiasi cha Sh3 bilioni, alijibu kuwa hiyo ni hatua ya kinidhamu na pia ni
fundisho kwa wengine.
Kauli
ya Mahadhi
Lowassa, ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu, alimhoji
Mahadhi kuhusu jaribio la wizi lililofanywa na maofisa wa wizara yake baada ya
kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Mambo ya Nje kilichofanyika kwenye Ofisi
ndogo ya Bunge jijini Dar es Salaam juzi.
Mahadhi alisema
wizara ilichukuahatua dhidi ya maofisa wa ngazi za chini wakati suala la Itatiro
lilikuwa mikononi mwa Rais Kikwete kutokana na wadhifa
wake.
Naibu waziri huyo alidai
walichukua hatua hiyo kufuatia ushauri waliopewa na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mkaguzi wa Ndani walioendesha uchunguzi wa
njama hiyo.
Post a Comment