Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali itaendelea
kukopa kwa ajili ya maendeleo, kwani haiwezi kuendesha taifa kwa kutegemea kodi
pekee.
Akiwa kwenye ziara ya
Mkoa wa Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alitembelea miradi mbalimbali ya
maendeleo, ikiwamo uzinduzi wa maabara ya kisasa ya Mamlaka ya Chakula na Dawa
Tanzania (TFDA) na Chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Veta
Kipawa
Alisema mikopo
inalipwa kwa kipindi kirefu na riba yake ni nafuu na kwamba, anashangazwa na
wanasiasa ambao alidai wengi ni wasomi ambao wamekuwa wakidanganya watu na
kuwatia hofu.
“Kumekuwa na siasa
nyingi kwamba tunadaiwa na kila Mtanzania anatakiwa alipe Sh400,000, mnadhani
tunakopa na kulipa kesho?” alihoji Rais Kikwete.
Akitoa mfano,
alisema daraja la Malagarasi limejengwa kwa mkopo na kwamba, riba yake ni
asilimia 0.02 na utalipwa kwa miaka 40.
“Hatuachi kukopa
ng’o, ukiacha wengine kama Kenya watakwenda watachukua na kupata maendeleo
halafu wewe unabaki hapohapo ulipo,” alisema.
Katika hatua
nyingine, Rais Kikwete amewaagiza watendaji wa Dar es Salaam kujenga hospitali
maalumu za uzazi na watoto, lengo likiwa ni kupunguza vifo vya mama na
mtoto.
Alisema
haiwezekani kila mara kutoa taarifa bila kuwapo kwa suluhisho la matatizo
yanayotolewa ufafanuzi.
Rais Kikwete
alisema katika kuboresha sekta ya afya na upatikanaji wa huduma, lazima
kuhakikisha zinajengwa hospitali maalumu za uzazi na watoto ili kupunguza
msongamano uliopo hivi sasa.
“Huwa najiuliza
ninyi madiwani mnapokutana katika vikao vyenu mnazungumza kitu gani, kugawa
viwanja?” alihoji Rais Kikwete huku watendaji mbalimbali wakiangua vicheko.
Post a Comment