MAHAKAMA ya Juu imekataa ombi la
Waziri Mkuu Raila Odinga wa CORD la kutaka ibatilishe uchaguzi wa Uhuru Kenyatta
wa muungano wa Jubilee kuwa rais. Hii ina maana kuwa Bw Kenyatta sasa ataapishwa
kuwa rais Aprili 9.
“Mahakama ya Juu imefikia uamuzi kwa kauli moja kuhusu
masuala manne yaliyoibuliwa kwenye kesi za uchaguzi. Uchaguzi ulifanyika kwa
njia huru na ya haki na kwa kufuata Katiba na Sheria,” alisema Jaji Mutunga
kabla ya kutangaza kuwa Uhuru Kenyatta na William Ruto walichaguliwa kwa njia
huru na ya haki kuwa Rais na Naibu Rais wateule.
“Kesi za Raila na AFRiCOG zimetupwa. Kila mtu ajilipie
gharama. Uamuzi wa kina utatolewa katika muda wa wiki mbili.”
Kuhusu kesi ya wanaharakati Dennis Itumbi na Moses
Kuria kuhusu kura zilizokataliwa, Jaji Mutunga alisema mahakama hiyo haina
mamlaka ya kutoa uamuzi.
Alihitimisha kwa kutoa wito kwa Wakenya wadumishe
amani.
“Mahakama imetekeleza jukumu lake. Jukumu sasa ni kwa
raia, viongozi wao, mashirika ya kijamii na wanahabari kuhakikisha umoja wa
Kenya unadumu,” alisema Jaji Mutunga.
RAILA AKUBALI KUSHINDWA, AMTAKIA UHURU KILA LA
HERI
WAZIRI Mkuu Raila Odinga amekubali kushindwa baada ya
Mahakama ya Juu kutupilia mbali kesi yake kupinga kupinga kuchaguliwa kwa Uhuru
Kenyatta. Bw Odinga amemtakia Rais Mteule kila la heri.
“Hatua yangu ya kwenda mahakamani ilikuwa ishara ya
imani yangu katika Mahakama. Haikuwa ni ya kisasi.
Tulijaribu kadiri ya uwezo wetu. Mawakili wetu
wakiongozwa na Oraro walikusanya na kuwasilisha ushahidi mwingi.
“Tunasikitika kwamba Mahakama ilikataa ushahidi kwa
msingi kuwa uliwasilishwa kwa kuchelewa au mahakama haikuwa na muda. Mwishowe,
Wakenya walipoteza nafasi ya kujua nini kilitendeka.”
“Mimi na Kalonzo hatuna majuto kwa kuwasilisha kesi
kortini. Ni matumaini yangu kwamba serikali ijayo itaheshimu Katiba na
kuitekeleza.
Namtakia Rais Mteule Uhuru Kenyatta na kundi lake kila
la kheri. Pia, maseneta, wabunge, wawakilishi wa wanawake na magavana ufanisi.
Tusigawanywe na mtukio haya. Natoa wito kwa Wakenya na wafuasi wangu wakumbuke
maneno ya Wimbo wa Taifa – “Haki iwe ngao na mlinzi.”
Source: http://www.wavuti.com
Post a Comment