Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba na Katibu wa Tume Bw. Assaa Rashid.(Na Mwandishi Wetu).
 
Tume ya Mabadiliko ya Katiba inapenda kuwakumbusha wananchi wote wanaopenda kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kuwa siku ya mwisho ya kuwasilisha maombi hayo kwa Maofisa Watendaji wa Mitaa na Wilaya kwa Tanzania Bara na Masheha kwa Zanzibar ni siku ya Jumatano, tarehe 20 Machi mwaka huu (2013).
Wananchi wanaopenda kuwa Wajumbe wa Mabaraza hayo wawasilishe maombi yao yakiwa na taarifa zifuatazo: Majina Kamili; Jinsi; Umri; Eneo analoishi kwenye Kijiji/Mtaa; Kiwango cha Elimu; na Kazi yake.
Mwombaji anatakiwa kuwa na sifa zifuatazo: Awe ni Raia wa Tanzania na awe na umri wa miaka 18 au zaidi na awe na uwezo wa kusoma na kuandika. Sifa nyingine ni pamoja na kuwa mkazi wa kudumu wa kijiji, mtaa au shehia husika na awe ni mtu mwenye hekima, busara na uadilifu na pia awe mtu mwenye uwezo wa kujieleza na kupambanua mambo.
Kuhusu ukazi wa kudumu
Kuhusu ukazi wa kudumu, Tume inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa mkazi wa kudumu ni mwananchi yeyote anayeishi katika mtaa au kijiji husika na sio lazima awe anamiliki nyumba katika mtaa au kijiji hicho.
Aidha, Tume inapenda kuwafahamiusha wananchi walioomba kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kuhakiki majina katika orodha ya majina ya waombaji wote itakayobandikwa katika eneo la wazi au mbao za matangazo katika Mtaa, Kijiji au Shehia husika kwa siku saba kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 28 mwezi machi mwaka huu (2013).
Tarehe za uchaguzi wa Wajumbe ngazi ya Mtaa na Kijiji
Aidha, Tume inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa imefanya mabadiliko madogo katika mwongozo wake katika tarehe za vikao vya mitaa na vijiji vitakavyowachagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba. Kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na Tume mwezi uliopita, vikao hivi vilipaswa kufanyika kati ya tarehe 30 mwezi Machi mwaka huu (2013) na tarehe 3 Aprili mwaka huu (2013).
Kwa mujibu wa mabadiliko mapya, vikao hivyo sasa vitafanyika kati ya tarehe 30 Machi mwaka huu (2013) hadi tarehe 5 Aprili mwaka huu (2013). Kwa msingi huu kila kijiji au mtaa kitachagua tarehe atika vikao hivyo, wananchi watapiga kura za siri kuwachagua wananchi wanne kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
Kufuatia mabadiliko haya, Vikao Maalum vya Kamati za Maendeleo za Kata vya kuwachagua wajumbe wanne kutoka miongoni mwa wananchi waliochaguliwa na vijiji na mitaa navyo vimesogezwa mbele na sasa vitafanyika kati ya tarehe 7 Aprili mwaka huu (2013) na tarehe 10 Aprili mwaka huu (2013). Awali, vikao hivi vilipangwa kufanyika kati ya tarehe 5 Aprili mwaka huu (2013) na tarehe 9 Aprili mwaka huu (2013).
Tume inawaomba wananchi kushiriki na kuendesha mchakato wa kuwapata Wajumbe kwa amani na utulivu na kuzingatia mwongozo uliotolewa na Tume.
Imetolewa na:
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Dar es Salaam
Machi 18, 2013