Ndugu zangu,
Jana niliandika, kuwa ili tufahamu zaidi urafiki uliokuwepo wa watatu hawa; Julius, Oscar na Rashid ni vema tufahamu jinsi walivyokutana;
Nyerere alikutana na Oscar Kambona wakati Kambona alipokuwa shuleni Tabora mwishoni mwa miaka ya 40. Inasemwa, kuwa Nyerere alimtangulia kiumri Oscar kwa kupishana miaka mitatu tu. Kule Tabora Nyerere alikutana pia na Rashid Kawawa, naye alimzidi kiumri kwa miaka mitatu hivi.
Hivyo basi, twaweza kusema, kuwa urafiki wa Julius, Oscar na Rashid ulianzia Tabora, na harakati zao za pamoja za mapambano ya kisiasa zilianzia huko huko Tabora. Endelea....
Julius Nyerere alikuwa Mkatoliki na hodari sana shuleni. Akafika mpaka Uingereza kimasomo. Aliporudi akafanya kazi ya ualimu pale Pugu. Alipoambiwa achague kati ya ualimu na siasa, Julius akachagua siasa.
Oscar naye alikuwa mwumini wa kanisa la Anglican na hodari sana shuleni. Naye akafika mpaka Uingereza kusomea sheria. Hakumaliza masomo yake, Nyerere alimshawishi akatishe masomo yake, arudi nyumbani kuimarisha TANU kwenye Uchaguzi uliokuwa mbele yao.
Rashid Kawawa, Mwislamu, alisoma mpaka Tabora. Hakufika Uingereza, lakini, alikuwa kiongozi mahiri wa vyama vya Wafanyakazi . Katika TANU alikuwa ni mpiganaji wa kuaminika. Rashid alikuwa maarufu mjini. Alipata hata kucheza filamu maarufu ya ’ Mwogo Mchungu’.
Watatu hawa walikuwa marafiki, hilo halina shaka. Na baada ya uhuru wa Tanganyika, Julius na Oscar walijenga nyumba zao pale kijijini Msasani kwenye pwani ya bahari. Naam. Walikuwa karibu sana kikazi na walichagua kuishi pamoja kama majirani.
Inasimuliwa, kuwa pale Msasani, nyakati za jioni, Oscar na Julius walipenda sana kutembea pamoja ufukweni mwa bahari. Walitembea wakijadiliana mambo mbali mbali. Bila shaka, wake zao, Maria na Flora, walitembeleana na hata kuombana chumvi.
Na ikafika wakati, Oscar na Julius hawakuonekana tena wakitembea pamoja ufukweni. Na pengine Maria na Flora hawakutembeleana na kuombana chumvi. Ikafika wakati pia, Oscar na familia yake wakafungasha mizigo yao na kuondoka nchini kupitia Namanga. Nyumba yao ikaja kupata mpangaji mpya; Milton Obote, rafiki mwingine wa Julius Nyerere. Obote alipinduliwa na Idi Amin. Akakimbilia Tanzania, kwa rafiki yake, Julius Nyerere.
Na mjini Dar es Salaam ukatawala uvumi zaidi kuliko ukweli wa kilichotokea. Ikasemwa, kuwa Kambona ametoroka akiwa na sanduku limejaa pesa. Na pesa yetu wakati ule ilikuwa na thamani sana. Fikiri sasa kama sanduku la Kambona kweli lilijaa manoti!
Na utotoni pale Ilala, nilipata kusikia uvumi, kuwa huko Ulaya, Kambona amekuwa tajiri mkubwa. Wengine wakasema alishinda Bahati Nasibu. Wengine wakasema ni fedha alizotoroka nazo.
Na kuna wakati ukaenea uvumi, kuwa kuna meli bandarini imezuiliwa kushusha shehena ya vitanda. Ni vitanda ambavyo Kambona alivituma Tanzania ili vitumike mahospitalini. Kwa vile ukweli hasa kuhusu ugomvi wa Kambarage na Kambona haukupata kusemwa, basi, uvumi ukaendelea kusambazwa. Hivyo basi, ’kimya kikuu’.
Simulizi hii ni jaribio pia la kuvunja ukimya wa juu ya nini kilitokea miaka hamsini iliyopita, na nini cha kujifunza. Itaendelea....
Credits: Mjengwablog
Post a Comment