Jeshi la Polisi mkoani Kagera limefanikiwa kuwaua majambazi saba wakati wa mapambano makali ya kurushiana risasi na Askari wa Jeshi la Polisi wakati majambazi hao walipokuwa katika harakati za kuvamia mgodi wa Tulawaka ambapo baada ya kupekuliwa walikutwa na bunduki mbili za kivita aina ya SMG, mabomu matatu ya kurusha kwa mkono, risasi 156, magazine tano, simu mbili pamoja na fedha za Burundi franc 800.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi wa Polisi Philip Kalagi alisema tukio hilo lilitokea tarehe kumi mwezi huu majira ya saa tatu na nusu usiku katika kijiji cha Mavota wilayani Biharamulo.
Kamanda Kalagi alisema kati ya majambazi hao, watano wanasadikiwa kuwa ni raia wa Burundi na mmoja wao ametambulika kwa jina la Minani Luzamba (46) mkazi wa Rwambarage nchini Burundi.
Aidha alisema raia wawili uraia wao bado unachunguzwa ingawa wamekutwa na vitambulisho vya Tanzania vya kupigia kura vilivyotolewa mkoani Kigoma na maiti zao zimehifadhiwa katika Hospitali ya wilaya ya Biharamulo.
Alisema kazi hiyo ilifanikiwa kwa kushirikiana na kikosi kazi cha taifa cha kuzuia uhalifu pamoja na taarifa za raia wema ambapo amewaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za kuwezesha kukamatwa kwa watu wanaojihusisha na uhalifu mkoani Kagera.
Post a Comment