Na Ban Ki-moon
Safari ya maili elfu moja huanza na hatua ya kwanza, lakini kuanzia wiki hii tutaanza safari ya siku elfu moja kuelekea kwenye hatma mpya.
Mnamo tarehe 5 Aprili, dunia itaingia kwenye wakati muhimu katika msukumo mkubwa zaidi katika historia na uliofanikiwa sana wa kuondoa umaskini – alama hii ya siku 1000 kabla ya tarehe ya mwisho ya kufikia shabaha ya Malengo ya Milenia ya Maendeleo.
Malengo hayo halisi nane yaliwekwa mwaka 2000, wakati ambapo viongozi wengi zaidi kuliko walivyowahi kukutanika katika Umoja wa Mataifa walikubaliana kupunguza umaskini na njaa kwa kiwango cha nusu, kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na maradhi, kutatua upungufu wa maji salama na usafi, kupanua elimu na kufungua milango ya fursa kwa wasichana na wanawake.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa viongozi kutoa ahadi nono zenye kuleta matumaini makubwa. Watu wenye mtazamo hasi walitarajia kwamba mpango wa MDG ungetupiliwa mbali katikati ya njia kwa sababu ulionekana kama wa kinadharia zaidi. Badala yake, Malengo yamesaidia katika kupanga vipaumbele vya ulimwengu na kitaifa, vimechochea uchukuaji hatua, na vimesaidia kuleta matokeo makubwa.
Katika miaka kumi na mbili iliyopita, zaidi ya watu milioni 600 wameondoka kwenye lindi zito la umaskini – ambayo ni sawa na kupunguza tatizo kwa kiwango cha nusu. Idadi kubwa iliyovunja rekodi ya watoto wanaopata elimu ya msingi – ambapo idadi ya wasichana na wavulana iko karibu sawa, kwa mara ya kwanza. Vifo vya mama na mtoto vimepunguzwa. Uwekezaji unaolenga kukabili malaria, VVU/UKIMWI na kifua kikuu umeokoa mamilioni ya maisha, na Bara la Afrika limepunguza vifo vinavyotokana na UKIMWI kwa theluthi moja katika miaka sita iliyopita.
Vilevile kuna Malengo na shabaha pale tunapohitaji kufanya maendeleo zaidi. Watoto wengi zaidi bado wanapoteza maisha wakati wa kuzaliwa, wakati ambapo njia za kuokoa maisha hayo zipo. Jamii nyingi bado zinaishi katika mazingira yenye matatizo ya usafi, jambo linalofanya maji yasiyo salama kuwa tishio kubwa kwa uhai. Katika maeneo mengi ulimwenguni, yale yaliyo tajiri na yaliyo maskini pia, tofauti ya kipato inazidi kuwa kubwa sana. Watu wengi mno wanabaki nyuma.
Ili kuongeza kasi ya uchukuaji hatua, jamii ya kimataifa haina budi kuchukua hatua nne muhimu sasa.
Kwanza, kuongeza mafanikio kupitia uwekezaji wa kimkakati na wenye shabaha maalumu wakati huohuo kuhakikisha kwamba kila uwekezaji una matokeo mengi, ili kutia nguvu zaidi matokeo katika maeneo mengine yote: wafanyakazi wa afya ya jamii milioni moja katika Bara la Afrika wahudumie maeneo yasiyofikika kwa urahisi na kuwasaidia akina mama na watoto wasipoteze maisha kutokana na magonjwa ambayo yanazuilika au kutibika kwa urahisi; kuongeza uwekezaji katika usafi; kuhakikisha upatikanaji wa huduma za msingi za afya kwa wote, ikiwa ni pamoja na huduma za dharura za uzazi; na usambazaji wa kutosha wa dawa za kupunguza makali ya VVU na kuzuia malaria.
Kuhakikisha kuwepo kwa usawa katika kupata elimu, huduma za afya, lishe, fursa za kiuchumi kwa wanawake na wasichana na kwamba jambo hili ni miongoni mwa vitoa misukumo vikubwa vya maendeleo katika Malengo yote.
Pili, tuweke mkazo katika nchi zilizo maskini na zilizo hatarini zaidi, ambazo ndiyo zina jumla ya watu bilioni 1.5. Nchi hizi mara nyingi zimegubikwa na njaa, mapigano, uongozi dhaifu, na viwango vya juu ya makundi yanayotenda jinai, ambapo kwa kiasi kikubwa zinajikuta zinashindwa kuendelea licha ya kujaribu kufanya jitihada kubwa. Zilizo nyingi bado hazijafikia hata moja ya Malengo ya Milenia ya Maendeleo. Kwa kuwekeza kwenye maeneo kama yale ya Sahel, Pembe ya Afrika, Asia ya Kati, tunaweza kuhamasisha mzunguko wenye tija zaidi wa maendeleo ya kiuchumi, usalama wa watu na kujenga amani.
Tatu, hatuna budi kutimiza ahadi za fedha. Ni vigumu sana kuendana na bajeti huku kukiwa na kundi kubwa la maskini na watu walio hatarini zaidi. Kimaadili, ni jambo lisilokubalika na halitamsaidia si mhisani wala mpokeaji. Licha ya kuwa katika kipindi cha kubana matumizi, nchi nyingi zimekuwa za kupigiwa mfano kwa kutimiza yale waliyoahidi. Wahisani wapya kutoka katika mataifa yanayoibukia pia wamekuwa wakijitokeza. Tunapaswa kupongeza juhudi hizi na kuhimiza nyingi zaidi zifanyike.
Nne, alama ya siku-1000 inapaswa kuwa wito wa kutaka kuanzishwa kwa vuguvugu la kiulimwengu kuanzia serikali hadi katika ngazi za chini, ambapo kila upande umekuwa muhimu sana kufikia mafanikio. Ni vema pia tutumie kikamilifu fursa kamili ya kiteknolojia na vyombo vya habari vya kiraia – fursa ambazo hazikuwepo wakati Malengo ya Maendeleo ya Milenia yalipokuwa yakiandaliwa muda mfupi kabla ya kuingia karne mpya.
Malengo ya Milenia ya Maendeleo yamethibitisha kwamba shabaha lengefu za maendeleo ya ulimwengu zinaweza kuleta tofauti kubwa ya maana. Zinaweza kuhamasisha, kuunganisha na kujenga ari. Zinaweza kuchochea ubunifu na kuleta mabadiliko ulimwenguni.
Mafanikio katika siku 1000 zifuatazo, siyo tu kwamba zitakuza ubora wa maisha ya mamilioni ya watu, bali pia itaongeza kasi wakati tunapopanga nini kifuatie baada ya mwaka 2015 na changamoto za kufanya maendeleo yawe endelevu.
Bado kutakuwa na mambo mengi ambayo bado hayajakamilika. Lakini tunapotazama kizazi kijacho cha malengo ya maendeleo yaliyo endelevu, tunapata ari kwa kujua kwamba Malengo ya Milenia ya Maendeleo yameonyesha kwamba, panapokuwa na utashi wa kisiasa, kukomesha umaskini uliokithiri ni jambo linalowezekana na limo ndani ya uwezo wetu.
Tuzitumie vema siku hizi 1,000 na kutumia vizuri ahadi yetu ile ya Milenia.
Ban Ki-moon ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Post a Comment