Serikali imeshatoa jumla ya shilingi bilioni 61 kupitia Mpango wa Maendeleo ya Msingi nchini kwa ajili ya uendeshaji wa shule za msingi.
Kiwango cha fedha hizo kilitolewa na Serikali hadi kufikia Machi mwaka huu ikiwa ni sawa na asilimia 77 ya kiasi kilichopangwa kutolewa na serikali kwa ajili hiyo katika mwaka huu wa fedha 2012/2013.
Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa, Elimu, Mhe. Kassim Majaliwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Ngara Mh. Deogratias Ntukamazina aliyetaka kujua ni lini Serikali itarejesha mpango wa kutoa shilingi 10,000 kwa kila mwanafunzi kwa ajili ya uendeshaji wa shule badala ya shilingi 200 zinazotolewa kwa sasa.
Mh. Majaliwa amesema kuwa asilimia 40 ya fedha hizitatumika kwa ajili ya ununuzi wa vitabu na kuongeza kuwa serikali imedhamiria kuhkikisha kuwa kiasi cha shilingi 10,000 kwa mwanafunzi kinafikiwa kwa kuendelea kutoa fedha za uendeshaji kila robo ya mwaka.
Ameongeza kuwa fedha zote zilizotolewa na Serikali Kuu tayari zimeshatumwa katika Halmashauri zote nchini na kubainisha kuwa kwa Wilaya ya Ngara jumla ya shilingi milioni 473 zimeshapelekwa ambazo ni sawa na shilingi 6,932 kwa wanafunzi ambayo ni sawa na asilimia 69.
Aidha Mh. Majiliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kutoa kiasi kilichobaki cha wastani wa shilingi 3,000 kwa mwanafunzi kadiri ya makusanyo ya serikali yatakavyopatikana hadi kufikia mwaka wa fedha.
Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi Nchini ulianza kutekelezwa kuanzia mwaka 2002 ambapo awamu ya kwanza ilitekelezwa kuanzia mwaka 2002 hadi 2006 na awamu ya pili kuanzia mwaka 2007 hadi 2012.
Serikali imekuwa ikitekeleza mpango huu kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo.
Mhe, Majaliwa amelieleza Bunge kuwa mbali na asilimia 40 za uendeshaji wa Maendeleo ya Elimu ya kutoka fedha za Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi kwa ajili ya kununulia vitabu, Serikali imetenga fedha kutokana na fedha za chenji ya Rada kwa ajilinya kununulia vitabu na tayari shilingi bilioni 40 kutoka katika fedha hizo zimeshatumwa katika Halmashauri.
(Na Benedict Liwenga, Dodoma.)
Post a Comment