Ndugu
Wananchi;
Naomba nianze kwa
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na kunipa fursa ya kuzungumza
nanyi kwa kupitia utaratibu wetu huu mzuri wa kila mwisho wa mwezi. Leo ninayo
mambo matatu ninayopenda kuzungumza nanyi.
Ziara ya Rais wa China
Nchini Tanzania
Ndugu
wananchi;
Jambo la kwanza ni ziara ya
Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China aliyoifanya nchini kwetu
kati ya tarehe 24 na 25 Machi, 2013. Lengo la ziara yake ilikuwa kuimarisha
uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya China na Tanzania. Napenda kuchukua
nafasi hii kuwashukuru wakazi wa Dar es Salaam kwa kumpokea vizuri mgeni wetu na
ujumbe wake. Wameondoka wakiwa na kumbukumbu nzuri ya nchi yetu na watu
wake.
Kwa niaba yenu, nimepokea
salamu za shukrani kutoka kwa Rais Xi Jinping akielezea kufurahishwa na mapokezi
mazuri tuliyowapatia. Naomba tuendelee kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa
wageni wetu wengine mashuhuri watakaotutembelea siku za
usoni.
Nami pia, nimemshukuru sana
Mheshimiwa Xi Jinping kwa kukubali mwaliko wangu na kufanya ziara ya kihistoria
na yenye mafanikio makubwa kwa nchi yetu. Ameifanyia nchi yetu jambo la heshima
kubwa na kumbukumbu isiyosahaulika. Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Barani
Afrika kuitembelea, tena siku kumi tu baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi
yake. Na, kubwa zaidi ni kutumia fursa ya ziara yake hapa nchini kutangazia
dunia Sera ya China kwa Afrika katika kipindi cha uongozi
wake.
Tumefarijika sana kusikia
kuwa uhusiano na Afrika bado unapewa kipaumbele cha juu na viongozi wapya wa
China. Pia, kuwa China itaendelea kukuza biashara na uwekezaji na kuongeza
misaada ya maendeleo kwa Afrika ikiwemo kutoa nafasi 18,000 za mafunzo kwa
vijana wa Kiafrika. Kama mtakumbuka nchi zetu mbili zilitiliana saini mikataka
16 ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali. Misaada ya maendekeo kwa maeneo
yetu ya kipaumbele nayo imejumuishwa.
Ndugu
Wananchi;
Rais Xi Jinping alielezea
na kusisitiza dhamira yake na ya Serikali na Chama cha Kikomunisti cha China ya
kudumisha na kukuza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na China. Kama
mjuavyo uhusiano huo ulianzishwa mwaka 1964 na waasisi wa nchi zetu, yaani
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania na
Mwenyekiti Mao Zedong aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa China na Waziri Mkuu wake Chou
En Lai.
Rais wa China aliahidi kuwa
nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika medani ya kimataifa na
kuchangia katika jitihada zetu za kujiletea maendeleo kwa kuongeza misaada ya
maendeleo. Katika miaka 49 ya uhusiano na ushirikiano na China nchi yetu
imepata misaada mingi ya maendeleo ikiwemo Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa
Mwalimu Nyerere ambao ulizinduliwa na Rais Xi Jinping wakati wa ziara
yake.
Ndugu
wananchi;
Kuna miradi kadhaa mikubwa
inayoendelea kutekelezwa nchini, Bara na Zanzibar, kwa msaada wa Serikali ya
China. Wakati wa ziara yake, Rais Xi Jinping iliahidi kuendelea kutusaidia
miradi mingine ya maendeleo kama tulivyoomba wakati wa mazungumzo yetu licha ya
ile ambayo ilitiwa saini siku ile.
Ajali ya Kuporomoka Jengo
la Ghorofa
Jijini Dar es
Salaam
Ndugu
Wananchi;
Jambo la pili ninalotaka
kuzungumzia ni ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa
katika jiji la Dar es Salaam. Ajali hiyo iliyotokea juzi tarehe 29 Machi, 2013
imeleta msiba na simanzi kubwa nchini. Mpaka sasa maiti za ndugu zetu 30
zimepatikana. Watu 17 waliweza kuokolewa, wanne kati yao bado wanaendelea na
matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Wengine walitibiwa na
kuruhusiwa. Kazi ya kufukua eneo la ajali inaendelea na sasa inakaribia kufikia
ukingoni.
Ndugu
Wananchi;
Mimi na viongozi wenzangu
tulipata nafasi ya kwenda kuangalia eneo la ajali. Hali niliyoiona pale
imenihuzunisha sana. Lazima nikiri, hata hivyo, kwamba nimeridhishwa sana na
juhudi kubwa za uokoaji zilizokuwa zinafanywa na wanajeshi wetu wakishirikiana
na taasisi, mashirika binafsi na wananchi. Napenda kutumia nafasi kutoa
shukrani maalum kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Saidi Meck Sadick kwa
uongozi wake madhubuti. Pia nampongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ndugu Raymond
Mushi, na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ndugu Suleiman Kova
pamoja na Maafisa na askari wa JWTZ, na wale wote walioshiriki na wanaoendelea
kushiriki katika juhudi za uokoaji.
Nawapongeza pia madaktari
na wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali nyinginezo kwa
jitihada zao za kuokoa maisha ya waliojeruhiwa. Nawapa pole wale wote waliofiwa
na wapendwa, ndugu na jamaa zao katika ajali hii. Nawaomba wawe na moyo wa
subira huku sote tukiungana nao kuwaombea marehemu wetu wapate mapumziko mema
peponi. Kwa waliojeruhiwa, tunawaombea wapone upesi.
Ndugu
Wananchi;
Maneno mengi yanasemwa
kuhusu chanzo cha ajali ile. Alimradi kila mtu ana dhana yake. Niliagiza
vyombo na mamlaka husika wachukue hatua zipasazo kuchunguza sababu za ghorofa
hilo kuanguka na watakaothibitika kusababisha maafa hayo wachukuliwe hatua
zipasazo. Wa kushtakiwa Mahakamani washitakiwe na wa kufutiwa leseni za kufanya
shughuli za ujenzi au taaluma zao wafutiwe bila ajizi. Jambo la msingi la
kusisitiza ni kuwa mamlaka zinazohusika na usimamizi wa ujenzi lazima zitimize
ipasavyo wajibu wake. Naamini kama mamlaka hizo zingetimiza ipasavyo wajibu
wake ajali hii ingeepukika. Halmashauri za miji na wilaya zina wajibu maalum
kwenye ujenzi katika maeneo yao. Watimize wajibu wao. Yaliyotokea Dar es
Salaam yawe fundisho kwa wote.
Ndugu
Wananchi;
Ni matumaini yangu kuwa
Bodi ya Usajili wa Wakandarasi na Bodi ya Usajili wa Wahandisi itakamilisha
mapema uchunguzi wake ili ukweli ujulikane. Bodi ya Usajili wa Wasanifu
Majengo na Wakadiriaji Majenzi na Baraza la Taifa la Ujenzi nao washirikishwe
kwa ukamilifu ili ukweli upatikane na hatua stahiki zichukuliwe. Pia naomba
washauri namna bora ya kukomesha ajali za aina hiyo siku za
usoni.
Uhusiano wa Wakristo na
Waislamu
Ndugu
Wananchi;
Jambo la tatu ninalopenda
kuzungumza nanyi leo ni uhusiano wa Waislamu na Wakristo nchini. Jambo hili
nimeshalizungumzia mara kadhaa siku za nyuma, lakini nalazimika kulisemea tena
kutokana na hali ilivyo sasa. Tumefikia mahali ambapo kama viongozi na waumini
wa dini hizi kubwa mbili hawatakubali kubadili muelekeo wa sasa, tunakoelekea ni
kubaya. Nchi yetu nzuri tutaivuruga na sifa yake ya miaka mingi ya Waislamu na
Wakristo kuishi pamoja kidugu, kwa upendo, ushirikiano na kuvumiliana
itatoweka. Tanzania itaacha kuwa kisiwa cha amani na kuingia katika orodha ya
nchi zenye migogoro na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Ndugu
Wananchi;
Nyaraka na kauli kali kali
zinazotolewa na viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu zinanishawishi kuamini
haya niyasemayo. Nyaraka na kauli hizo zina mambo mawili makuu. Kwanza, kwamba
kila upande unatuhumu, kushutumu na kulaumu upande mwingine kwa kufanya vitendo
viovu dhidi ya dini yake. Kauli na mihadhara ya kudhalilisha dini za wengine,
kunajisi vitabu vitakatifu, kuchoma moto nyumba za ibada, mzozo kuhusu nani
achinje na kuuawa kwa viongozi wa dini ni baadhi ya mambo yanayotolewa
mifano.
Na, pili kwamba kila upande
unailamu Serikali kwa kupendelea upande mwingine. Wakristo wanalaumu kwamba
mihadhara ya kudhalilisha Ukristo inaendeshwa na Serikali haichukui hatua.
Aidha, Wakristo wanateswa na viongozi wao kuuawa na Waislamu, lakini Serikali
haichukui hatua. Kwa ajili hiyo wanadai kuwa Serikali imeshindwa kulinda uhai
wa raia wake. Wanasema pia kwamba Serikali inapendelea upande wa
Waislamu.
Ndugu
Wananchi;
Waislamu nao wanadai kuwa
kitabu chao kitakatifu, yaani Quran Tukufu, kinadhalilishwa kwa kuchanwa,
kuchomwa moto na kukojolewa na Wakristo na Serikali haichukui hatua yo yote ya
maana. Waislamu wananyanyaswa katika nchi yao, wanakamatwa ovyo, hawapewi fursa
sawa na kwamba Serikali inawapendelea Wakristo. Wanasema nchi inaendeshwa kwa
mfumo wa Kikristo. Mimi binafsi wananishutumu kuwa napendelea kushiriki zaidi
kwenye shughuli za Wakristo kuliko za Waislamu kama vile harambee za kujenga
Makanisa na shule za Makanisa. Naambiwa kuwa mwepesi kushiriki maziko ya
Maaskofu kuliko Masheikh wanapofariki. Ipo Misikiti mitatu hapa Dar es Salaam
wamenisomea itikafu nife. Katika itikafu hiyo wamewajumuisha Inspekta Jenerali
wa Polisi, Said Mwema na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam,
Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ndugu Suleiman Kova.
Ndugu
Wananchi;
Napenda kuwahakikishia
Watanzania wenzangu kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza, hatupendelei upande wo
wote. Hatufurahishwi na kitendo cha mtu kudhalilisha dini ya mwenzake ndiyo
maana wapo wahadhiri wa dini ya Kiislamu na wahubiri wa dini ya Kikristo
wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa nyakati mbalimbali. Vyombo vya usalama
vinatambua wajibu wake huo na kama haifanyiki ni ulegevu wa mtu tu katika
kutimiza wajibu wao na siyo kwamba ni sera na maelekezo yangu au ya Serikali.
Mtakumbuka kuwa mara kadhaa nimewakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya na wakuu wa
vyombo vya usalama kuacha ajizi katika kutimiza wajibu wao kwenye suala
hili.
Ndugu
Wananchi;
Mimi binafsi sibagui,
hushiriki shughuli za Waislamu na Wakristo kila ninapoalikwa labda nikose nafasi
kwa sababu nyinginezo. Nimeshafanya shughuli nyingi za Waislamu kama vile
Maulid ya Mtume Muhamad S.A.W., safari za Hija, ujenzi wa misikiti na madrasa na
mengineyo mengi. Nimeshashiriki mazishi ya Masheikh kama nifanyavyo kwa
Maaskofu na watu mbalimbali Waislamu na Wakristo. Pale ambapo sikushiriki
mazishi ya Sheikh au Askofu itakuwa ni kwa sababu ya kubanwa na shughuli
nyingine ambazo lazima nifanye mimi, au taarifa ilikuwa ya muda mfupi. Kwa
upande wa Waislamu desturi yetu ya kuzika mara mtu anapofariki huwa kikwazo
kwangu kushiriki hasa ikiwa ni nje ya Dar es Salaam kwa sababu ya taratibu za
kumsafirisha Rais kutoka mahali pamoja kwenda pengine siyo nyepesi. Wakristo
hawana utaratibu huo, huwa wanaweza kusubiri hivyo huniwia rahisi
kushiriki.
Ndugu
Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa
Serikali yetu haijashindwa kulinda usalama wa raia wake au viongozi wa dini na
nyumba za ibada. Kama ingekuwa hivyo, tungeshuhudia mauaji ya raia, viongozi wa
dini na matukio ya kuchomwa nyumba za ibada yakiwa mengi hapa nchini. Lakini
hivyo sivyo. Nawasihi sana ndugu zangu Wakristo na Waislamu kuwa tusiyachakulie
matukio ya kuuawa kwa Mchungaji Mathayo Kachila kule Buseresere, Geita, na Padri
Evaristus Mushi kule Zanzibar, au kumwagiwa tindikali Sheikh Fadhili Soroga,
Naibu Mufti wa Zanizbar, kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda na kuchomwa moto
kwa Makanisa Zanzibar na Mbagala, Dar es Salaam kuwa ni kielelezo na ushahidi wa
Serikali kushindwa kutimiza wajibu wake.
Kila tukio lina mazingira
yake, hakuna ushahidi wa vyombo vya Serikali kuzembea. Hakuna ushahidi wa
matukio hayo kuunganika. Mpaka sasa hatujapata ushahidi wa kuwepo kikundi cha
Waislamu wanaopanga kuua viongozi wa Kikristo na kuchoma moto Makanisa hapa
nchini.
Ndugu
Wananchi;
Kifo cha Mchungaji Mathayo
Kachila wa Buseresere ni matokeo ya vurugu zilizosababishwa na mzozo kati ya
Wakristo na Waislamu kuhusu kama nyama iliyochinjwa na Wakristo Kanisani nayo
iuzwe kwenye bucha iliyopo pale kijijini ambayo kwa mazoea huuzwa nyama
iliyochinjwa na Waislamu. Katika ugomvi na vurumai hizo ndipo watu kadhaa wa
pande zote walijeruhiwa na Mchungaji kupoteza maisha. Si tukio unaloweza
kulihusisha na mengineyo nchini. Ni la pale pale Buseresere na limeanzishwa na
kuhusisha Wakristo na Waislamu wa Buseresere kwa sababu
zao.
Hivi kama kusingekuwepo na
mzozo wa nyama ile kuuzwa katika bucha ile kuumizana kule na mauaji yale
yangetokea? Kabla ya mzozo ule Wakristo na Waislamu wa Buseresere hawakuwa na
ugomvi baina yao. Walikuwa wanaishi kidugu na kushirikiana katika shughuli zao
za kujitafutia riziki huku kila mmoja akimuabudu Mungu kwa misingi ya dini
yake. Hivyo kutumia tukio hilo kutoa wito kwa Wakristo wote kuwa kuuawa kwa
Mchungaji Kachila ni sawa na kuuawa kwa Wakristo wote nchini kulikofanywa na
Waislamu ni kulikuza tatizo isivyostahili. Busara ituongoze kutafuta njia ya
kuwapatanisha Wakristo na Waislamu wa Buseresere wazungumze, waelewane na
waendelee kuishi pamoja kama ilivyokuwa awali. Hata mzozo wa kuchinja wanaweza
kuumaliza. Mbona bucha za kitimoto zipo na watu hawajapigana. Kutumia mzozo wa
Buseresere kueneza chuki kati ya Wakristo na Waislamu nchi nzima si sawa.
Hatuwatendei haki Watanzania.
Ndugu
Wananchi;
Kuuawa kwa Padri
Evaristus Mushi wa Zanzibar ni tukio linalojitegemea halina uhusiano kabisa na
lile la Buseresere, Geita. Hapakuwa na mzozo kuhusu nani achinje. Bado
uchunguzi wake unaendelea na tumehusisha vyombo vya upelelezi vya nje
vishirikiane na vyetu kufanya uchunguzi. Tumefanya hivyo kwa sababu ya ugumu
uliopatikana katika uchunguzi wa matukio ya kabla yake. Yaani ile la kupigwa
risasi na kujeruhiwa kwa Padri Ambrose Mkenda na kumwagiwa tindikali kwa Naibu
Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhili Soroga. Bado hakuna mafanikio ya kutia moyo.
Na bado tunajiuliza kama matukio hayo matatu yanahusiana. Je, Makanisa kuchomwa
moto kule Zanzibar nako kuna uhusiano wowote na matukio yale matatu? Uchunguzi
unaoendelea unaweza kufumbua fumbo hilo.
Kuna watu wanadhani
yanahusiana na kwa sababu nzuri. Lakini inabaki kuwa ni dhana ya kibinadamu
mpaka ukweli halisi utakapobainika. Bado kazi ya uchunguzi inaendelea kufanywa
na vyombo vya usalama vya nchi yetu wakishirikiana na wenzao wa nje. Katika
mazingira hayo, ni mapema mno kumnyooshea kidole mtu ye yote na kuilaumu
Serikali ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Serikali siyo
mshirika katika mauaji hayo, na haina sababu ya kufanya hivyo. Ndiyo maana
tunahangaika usiku na mchana kupata jawabu.
Ndugu
Wananchi;
Hali kadhalika tukio la
Makanisa ya Mbagala, Dar Es Salaam kuvamiwa, kubomolewa, mali kuibiwa na
kuchomwa moto tarehe 12 Oktoba, 2012 nalo lina mazingira yake maalum. Chanzo
chake ni mzozo uliotokana na tukio la kusikitisha la kijana mmoja Mkristo
kukojolea Kitabu Kitakatifu cha Waislamu, yaani Quran Tukufu. Pamoja na maelezo
kuwa walikuwa na ubishi wa kitoto na kijana mwenzake, lakini kitendo hicho
kiliwakasirisha Waislamu. Kijana huyo alifikishwa kituo cha Polisi. Baadhi ya
Waislamu wenye msimamo mkali walifika kituoni hapo wakidai wapewe huyo kijana
wamuadhibu wao. Jeshi la Polisi lilikataa. Kukatokea mzozo kati ya waumini hao
na Polisi na baada ya kushindwa walichokitaka baadhi yao walipotoka pale,
wakaenda kufanya uhalifu wa kuvunja, kuiba na kuchoma moto
Makanisa.
Ndugu
Wananchi;
Baada ya tukio la Mbagala
hapajakuwepo na tukio la kuchomwa Kanisa mahali popote kwa upande wa Bara.
Aidha, hapajawahi kuwepo tishio lililothibitika la watu kutaka kuchoma Kanisa
popote. Lakini maneno ya vitisho vya kuchoma Makanisa yako mengi hasa kupitia
mitandao ya simu za mkononi. Kila ujumbe wa namna hiyo ulipofikishwa kwenye
vyombo vya usalama uchunguzi umefanywa na hata hatua za tahadhari kuchukuliwa
lakini hakuna hata taarifa moja iliyothibitika kuwa na chembe ya ukweli. Hata
dalili hazijakuwepo.
Tulichojifunza ni kuwa
ujumbe na vitisho vya aina mbalimbali hupelekwa kote, kwa Wakristo na Waislamu.
Upo unaowalenga Wakristo ukiwaambia wenzao Waislamu wanapanga kuwadhuru. Na upo
wanaopelekewa Waislamu wakiambiwa Wakristo wanao mipango mibaya dhidi yao.
Watanzania wenzangu nawaomba mtanabahi na mjue kuwa wapo watu wanacheza mchezo
mchafu wa kuwagonganisha na kutaka kuwagombanisha Wakristo na Waislamu kwa
sababu wanazozijua wao na kwa faida yao. Wanapandikiza chuki kwa lengo la
kutaka Wakristo na Waislamu wagombane. Wanapandikiza chuki baina ya Serikali na
waumini wa dini zetu kuu mbili ili ionekane Serikali imewatelekeza raia wake.
Ni mchezo mbaya, tusikubali kucheza ngoma tusiyoijua. Hivi ndugu zangu mmekaa
chini na kujiuliza kumetokea nini kipya hata leo kuwa na mhemko kama huu kati ya
Wakristo na Waislamu na kutishia kuleta vita baina nchini
kote?
Ndugu
Wananchi;
Serikali haijapuuzia kila
palipotokea matukio ya uhalifu. Watu 76 wanaotuhumiwa kuharibu na kuchoma moto
Makanisa kule Mbagala na kufanya fujo kituo cha Polisi wamekamatwa na kesi zao
zinaendelea Mahakamani. Kwa upande wa tukio la Buseresere lililosababisha kifo
cha Mchungaji Mathayo Kachila, watu 17, wakiwemo waumini wa dini ya Kikristo na
Kiislamu walikamatwa na kesi zao zinaendelea. Wapo walioshitakiwa kwa mauaji na
wapo walioshitakiwa kwa kufanya vurugu. Jeshi la Polisi bado linawatafuta watu
wengine waliohusika na uhalifu huo ili na wao wakamatwe. Kwa upande wa Zanzibar,
watu 10 wanaotuhumiwa kuchoma Makanisa wamekamatwa na kesi zao zinaendelea.
Bado hajakamatwa mtu kwa tukio la mwisho la kuchoma Kanisa baada ya kuuawa Padri
Evaristus Mushi. Uchunguzi unaendelea.
Ndugu
Wananchi;
Kwa upande wa kujeruhiwa
kwa Padre Mkenda, bado uchunguzi haujakamilika pamoja na kuwapo taarifa kadhaa
zinazoendelea kufanyiwa kazi. Kuhusu uchunguzi wa mauaji ya Padre Mushi, baada
ya jitihada kubwa kufanyika ikiwa ni pamoja na kushirikisha nchi zilizobobea
katika uchunguzi wa makosa ya aina hii, hatua ya kutia moyo imefikiwa. Mtu
mmoja amekamatwa na wengine wanaendelea kutafutwa.
Ndugu
Wananchi;
Kwa upande wa kanda na
vituo vya redio nako pia Serikali imechukua hatua. Watu kadhaa wamekamatwa na
kufikishwa Mahakamani katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kurekodi na
kusambaza kanda zinazochochea chuki na vurugu za kidini. Wapo Waislamu na
Wakristo. Wapo watu wengine ambao wanaendelea kutafutwa. Zipo taarifa kuwa
baadhi yao wamekimbilia nchi za nje. Jeshi la Polisi limeomba msaada wa Polisi
wa Kimataifa, yaani Interpol, kusaidia kuwatafuta na kuwarejesha nchini. Vituo
viwili vya radio yaani Kwa Neema FM cha Sengereme na Radio Imani cha Morogoro
vimefungiwa kwa muda wa miezi sita. Baada ya muda huo kupita, Kamati ya Maudhui
ya Mamlaka ya Mawasiliano itaamua ipasavyo.
Ndugu
Wananchi;
Nimeyaeleza haya kwa kirefu
kuwahakikishia kuwa Serikali inajali usalama wa raia wake wa mali zao na amani
na utulivu wa nchi yetu. Kamwe hatujashindwa kulinda raia wa nchi wa yetu na
yapo mambo mengi yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika kuhakikisha kuwa
Watanzania wa dini zote, makabila yote, rangi zote na mahali po pote walipo wako
salama. Tunataka kuona watu wanaendelea kuishi kwa amani, upendo, ushirikiano
na mshikamano kama tulivyokuwa tunaishi siku zote. Tunapenda kuona Watanzania
wanaepuka mambo yanayowabagua na kusisitiza yale yanayowaunganisha. Tujiepushe
kuyapa kipaumbele yale yanayotugawa.
Ndugu
Wananchi;
Athari za mzozo kuhusu
kuchinja kule Geita iwe fundisho kwetu sote. Tuazimie sote kuwa yaliyopita si
ndwele, tugange yajayo. Hebu tufikirie maisha yetu Watanzania yatakuwaje kwenye
shughuli za kijamii kama vile sherehe, harusi, ngoma na misiba iwapo tutaanza
kuwa na chakula tofauti kwa Waislamu na Wakristo. Fikiria itakuwaje kwenye
hospitali, shule na vyuo pawe na majiko mawili au labda hata mabwalo mawili ya
chakula kwa Waislamu na Wakristo. Jeshini nako kuwe na majiko na mabwalo ya
Waislamu na Wakristo. Hali iwe hivyo hivyo kwenye migahawa na maeneo mengine
yenye huduma ya chakula.
Ndugu zangu, tunataka
kuipeleka wapi nchi yetu? Tunataka kujenga nchi ya namna gani? Mimi naamini
tukifanya hivyo huo utakuwa ndiyo mwanzo wa kubaguana kwa kila kitu na kila
jambo na kuligawa taifa kwa namna ambayo hatutakuwa wamoja tena. Huko
tunakoelekea siko, ni kubaya. Tubadilike, na wakati ni huu. Viongozi wa dini
waongoze njia wawaepushe waumini wao na taifa letu na janga
hili.
Ndugu
Wananchi;
Bado narudia kusisitiza
umuhimu wa viongozi wa dini zetu kubwa mbili kukutana na kuizungumzia hali hii
na kuipatia ufumbuzi. Ni wao kuliko mtu mwingine ye yote wenye majawabu ya
matatizo haya. Ni masuala yanayohusu imani za dini na yanafanywa na viongozi wa
dini na wafuasi wao kwa jina la dini zao. Serikali ina wajibu wa kulinda amani.
Kazi yetu itakuwa rahisi kama waumini hawatafanya vitendo vitakavyosababisha
uvunjifu wa amani. Wa kuongoza waumini lipi jema na lipi baya ni viongozi wa
dini.
Ndugu
Wananchi;
Nimeshakutana na viongozi
kadhaa wa madhehebu na taasisi za dini za Kikristo na Kiislamu kuzungumza nao
kuhusu jambo hilo. Nimepata faraja kuona kuwa wote wanasikitishwa na mambo
yanayotokea hivi sasa na wameona busara ya viongozi wa dini kuzungumza ili
kuondoa tofauti zilizojitokeza. Wanakiri kuwa hali ilivyo sasa siyo ya kawaida
kwa Tanzania na Watanzania. Kuna upepo mbaya wa shetani unapita ambao viongozi
wa dini wana wajibu wa kuhakikisha kuwa hali ya hewa inasafishwa na kurejesha
nchi yetu na watu wake katika maisha tuliyoyazoea. Maisha ambayo waumini wa
dini tofauti wanaishi pamoja kwa udugu, upendo, ushirikiano na mshikamano kwa
misingi ya ubinadamu wao na Utanzania wao.
Waziri Mkuu, Mheshimiwa
Mizengo Pinda, ameshaeleza dhamira ya Serikali ya kuitisha mkutano wa viongozi
wa dini mapema mwezi ujao. Ni matumaini yangu kuwa wote watashiriki wenyewe
bila ya kutuma wawakilishi. Lazima tupate jawabu kwa maslahi ya taifa letu na
watu wake.
Ndugu
Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba
yangu napenda kutumia nafasi hii kuwaomba na kuwasihi waandishi wa habari
wasaidie kuliepusha taifa letu kuingia katika vita vya kidini. Waache
kushabikia taarifa zinazochochea na kujenga uhasama baina ya waumini wa dini
zetu. Nawaomba wapime athari za taarifa zao kabla ya kuziandika au
kuzitangaza. Wawe makini na maneno wanayotumia. Katika hali tuliyonayo sasa
lazima sote tuazimie kuondoa tofauti za kidini na kujenga umoja miongoni mwa
Watanzania wa dini zote. Wasipofanya hivyo, wataliingiza taifa katika mgogoro
mkubwa ambao hauna msingi kama ilivyotokea katika nchi jirani. Nawaomba
wamiliki wa vyombo vya habari kutambua kuwa wanao wajibu wa kuhakikisha vyombo
vyao havitumiki kuleta mifarakano kwa kuchochea uhasama baina ya Wakristo na
Waislamu.
Hitimisho
Ndugu
Wananchi;
Naomba kumaliza kuwa
kusisitiza kuwa wananchi wote kudumisha umoja na mshikamano wetu. Tuishi kwa
upendo, umoja, mshikamano na ushirikiano bila kujali tofauti ya dini zetu,
kabila, rangi au mahali atokako mtu. Hizo ndizo tunu za taifa letu la Tanzania
ambazo hatuna budi kuzienzi, kuzilinda na kuzidumisha. Narudia kuwahakikishia
kuwa Serikali haipendelei dini yo yote na wala haina mpango wa kushiriki
kuangamiza dini yo yote au waumini wao. Serikali kupitia vyombo vyake vya
usalama itaendelea kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia wake na mali zao kama
inavyofanya siku zote. Kama kuna mtu anaona kuwa maisha yake au mali zake zipo
hatarini, aende kutoa taarifa Polisi. Hatua zipasazo
zitachukuliwa.
Ndugu
Wananchi;
Mwisho nawatakia sikukuu
njema ya Pasaka. Tusherehekee kwa amani na utulivu. Tusherehekee
pamoja.
Mungu Ibariki
Afrika!
Mungu Ibariki
Tanzania!
Asanteni kwa
Kunisikiliza.
Post a Comment