Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo
na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Ikulu jijini Dar es
salaam leo
Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete katika picha ya pamoja
na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Ikulu jijini Dar es
salaam leo. Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano) Mhe Steven
Wassira.Picha na IKULU
----
Viongozi wa dini wamewataka waumini kote nchini kulinda
amani na umoja uliopo ili nchi isije ikaingia kwenye mgawanyiko wa kidini na
kuleta machafuko hapa Tanzania.
Wito huo umetolewa na viongozi wa dini leo Ikulu ya
Dar-Es-Salaam mara baada ya kikao cha pamoja baina ya viongozi wa dini na Rais
Jakaya Kikwete.
Viongozi hao wa dini wamefika leo wakiongozwa na Askofu
Tarcisius Ngalalekumtwa, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania (TEC).
Viongozi wengine wametokea Baraza la Kikristo Tanzania
(CCT) Seventh Day Advertist (SDA) na Baraza la Pentekoste Tanzania
(PCT).
Mkutano huo umeanza kwa Askofu Ngalalekumtwa kusoma
tamko lao la pamoja kwa Rais Kikwete ambalo ndilo limetoa muongozo wa mazungumzo
hayo ya leo ambayo yamehusu Amani na Usalama wa Taifa na migogoro ya kidini
ndani ya jamii.
Mkutano wa viongozi wa dini ya Kikristo Tanzania ni
mojawapo ya jitihada za Rais Kikwete kutafuta muafaka na kutafuta utatuzi wa
hali ya sintofahamu ambayo inanyemelea nchi yetu katika kipindi
hiki.
“Nataka tuzungumze ni namna gani tunaweza kutoka kwenye
hali hii na tunakwendaje mbele zaidi na kuhakikisha nchi yetu bado inakua ya
amani na umoja kama ilivyozoeleka” Rais amesema na kutoa nafasi kwa viongozi wa
dini kutoa maoni yao.
Viongozi hao wa dini wamemueleza Rais Kikwete kuwa
wanaunga mkono jitihada zake za kutafuta amani na kwa pamoja wamekubaliana
uandaliwe mkutano wa pamoja baina ya viongozi wa dini zote ambapo masuala ya
amani na umoja wa nchi utajadiliwa kwa kirefu.
Katika kikao cha leo pande zote zimekubaliana kuwa kuna
changamoto zilizoko sasa zinahitaji kutatuliwa haraka iwezekanavyo ili kuepusha
nchi kutumbukia katika mgogoro mkubwa zaidi, na pia kukubaliana kuwa pande zote,
kwa maana ya serikali na taasisi za dini, zinawajibu mkubwa wa kuhakikisha amani
inadumu.
Kabla ya kikao cha leo , Rais amewahi kukutana na
viongozi wa dini ya kiislamu na kikristo mmoja mmoja ambapo alikua akitafuta
maoni na ushauri wa pande zote kabla ya pande zote hazijakaa pamoja na kuwa na
msimamo wa pamoja.
Kikao cha leo kimehitimisha jitihada hizo na
kinachofuata ni mkutano mmoja ambapo Rais Kikwete atakutana na viongozi wa dini
zote kwa pamoja hivi karibuni.
Imetolewa
na:
Premi Kibanga
Mwandishi wa Habari wa Rais,Msaidizi
Ikulu-DSM
23 Aprili,2013
Premi Kibanga
Mwandishi wa Habari wa Rais,Msaidizi
Ikulu-DSM
23 Aprili,2013
Post a Comment