* VIJANA HAWA WAFICHUA YALIYOFICHIKA CHADEMA,DR.SLAA APOROMOSHA MATUSI..SIRI YA KUMUUA ZITTO
WANASIASA wawili vijana
ambao wamekuwa katika vita ya maneno na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, kuhusu madai waliyoyatoa kuwa
anawindwa kuuawa, mwishoni mwa wiki iliyopita, walijitokeza katika ofisi za
Mtanzania Jumatano na kufunua siri na matukio ya utesaji raia na mauaji ya
kinyama ambayo yamekuwa yakitokea kwa nyakati tofauti kwenye shughuli za kisiasa
hapa nchini.
Wanasiasa hao, Juliana Shonza na Mtela
Mwampamba, ambao wamefanya mahojiano ya ana kwa ana na gazeti hili, walisema
madai waliyoyatoa awali kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbrod Slaa, alitajwa
na kada wa chama hicho, Ben Saanane, kuwa alimtuma amuwekee sumu Zitto kwa lengo
la kumuua ni ya kweli kwa sababu walimkamata akiwa nayo na alikiri jambo hilo na
kumuomba msamaha Zitto kwa kitendo hicho.
Walidai, mbali na tukio hilo ambalo baada ya
kuliibua limegusa hisia za wengi na kuzua mijadala mikali, yapo matukio mengine
ya mauaji na majaribio ya kuua, ambayo yamekuwa yakiratibiwa na Chadema kwa
lengo la kuwagombanisha wananchi na Serikali.
Shonza na Mwampamba walisema kuwa wapo tayari
kutoa ushuhuda wa matukio hayo mahali popote watakapohitajika na walipoulizwa ni
kwa nini baada ya kubaini kuwepo kwa vitendo hivyo, hawakutoa taarifa kwa vyombo
vya sheria au taasisi za ulinzi na usalama, walisema mlengwa mkuu katika matukio
hayo ambayo yalikuwa yakisababisha madhara kwa watu wengine hakuwa tayari siri
hiyo kuanikwa.
Akizungumza mbele ya jopo
la waandishi wa habari wa gazeti la Mtanzania Jumatano, Shonza alidai kuwa, yeye
na baadhi ya vijana wenzake waliokuwa wakiunda kundi Patriotic Movement,
walimnasa Saanane akiwa na sumu hiyo katika Hotel ya Lunch Time iliyoko Ubungo,
Dar es Salaam, ambao awali alidai kuwa ni dawa ya Panya, lakini alipobanwa
alieleza kuwa ilikuwa sumu ambayo hakuitaja jina na kwamba alipewa na Dk. Slaa
ili amuwekee Zitto kwa sababu alikuwa akimsumbua sana.
Alisema, sumu ingewekwa
kwenye kinywaji cha Zitto akiwa katika kikao hicho, lakini hatua yake ya
kutohudhuria ndiyo iliyomuokoa.
Shonza alisema, baada ya Saanane kukiri kuwa
alitumwa na Dk. Slaa kumuwekea Zitto sumu, walimtaarifu wakati akiwa Marekani na
aliporudi alikutana na kuwataka jambo hilo wasilifikishe polisi kwa sababu
lingekivuruga chama na kwamba kwa sababu alikwishawajua wabaya wake
atajilinda.
Alimtuhumu Zitto kwa kuficha ukweli na
kumwita kiongozi mwoga, huku akimuonya kuwa iwapo ataendelea na tabia ya
kukanusha ukweli atamuumbua hadharani kwa sababu anamjua
vizuri.
“Ameongea hayo kwa sababu ana tabia ya
kushindwa kuthibitisha kuwa ana uwezo wa kujiongoza yeye mwenyewe pamoja na
wengine. Mtu wa maslahi Zitto, anatafuta huruma ya Chadema baada ya kuona
amepukutika kisiasa kutokana na kukosa msimamo kiuongozi na hawezi tena kutetea
wanyonge, ni mtu mwoga.
Mnapokuwa kwenye mapambano yeye yuko tayari
kurudi nyuma, lakini huruma hiyo asitegemee kuipata Chadema, labda akubali
kushaurika na kubadilika kama kweli anataka kutetea maslahi ya wanyonge,”
alisema Shonza.
Aidha, Shonza alimshambulia pia Saanane kwa
kudai anakataa ukweli anaojua, kwa sababu tukio la kukamatwa kwake akiwa na sumu
lilitokea akiwa mbele ya zaidi ya mtu mmoja na kusisitiza kuwa kada huyo wa
Chadema anatumika na viongozi wa juu wa chama hicho kuwashughulikia baadhi ya
wanachama wasiotakiwa.
Katika hili, Shonza alidai zaidi kuwa Saanane
ni mtu hatari kwa sababu ndiye aliyeanzisha kundi la PM7, ambalo lilikuwa na
lengo la kumpindua Mbowe kutoka kwenye wadhfa wake wa uenyekiti, lakini baadaye
aliwageuka wenzake na kusababisha kufukuzwa katika chama.
“Saanane alikuwa anatumika kutuingiza mkenge.
Alianzisha kile alichokiita mapinduzi, Patriotic Movement (PM7), lengo lilikuwa
Pindua Mbowe, sisi hatukujua.
Tulikuwa saba katika PM7, Saanane alifanikiwa
kutuchezea akili na alikuja na 'nick names' (majina bandia) yake. Mimi akaniita
Benanzir Bhuto, Mchange akaitwa Mdude, Mwampamba- Joseph Kony, Zitto- Dogo kama
tulivyozoea kumuita na yeye mwenyewe akajiita Cobra, wapo na wengine sikumbuki
vizuri majina yao hapa.
Sisi vijana wakati mwingine tunatumika
vibaya, sisi hatukujua ana ajenda yake, tulivyoshtuka akatukana na ndiyo
yakatokea hayo yaliyotokea,” anazidi kueleza Shonza.
Mwampamba
Kwa upande wake Mwampamba ambaye aliandamana
na Shonza katika ofisi za Mtanzania Jumatano, alidai kushangazwa na hatua ya
Zitto kukanusha kauli ya Shonza iliyokuwa ikieleza namna Saanane alivyokamatwa
akiwa na sumu aliyokuwa ametumwa kumuwekea Zitto.
Alisisitiza kuwa, Zitto anajua mipango
inayopangwa ndani ya Chadema kwa ajili ya kummaliza na alimtaka aache tabia ya
kufunika kombe ili mwanaharamu apite, kwa sababu inaweza kuwa na athari mbaya
kwake.
“Zitto anajua mpango mzima wa kutaka
kumalizwa kwa sumu na Ben Saanane, baada ya kutumwa na Dk. Slaa kwa sababu
tulimwambia na alithibitisha mwenyewe pale Saanane alipomuomba msamaha, sisi
ndiyo tulimbana Saanane hadi akaeleza ukweli wa mipango yao ya
mauaji.
“Leo namshangaa anavyojikomba eti haamini
kuwa anaweza kuuawa na hao jamaa. Lakini kwa Ben Saanane, namtaka atambue kuwa
Ludovick alipokamatwa alikanwa na Dk. Slaa wakati ndiye alikuwa kijana wake
mpenzi, sasa na yeye ipo siku atakimbiwa.
“Zitto anatakiwa aache tabia ya kufunika
funika mambo, ajue nimemwokoa sana katika mambo mengi, mfano mauaji ya Morogoro
yaliyopangwa na Chadema yalimlenga Zitto, alikuwa atolewe kafara. Yule muuza
magazeti aliyepigwa risasi Morogoro akafa, siku hiyo ilikuwa afe Zitto,” alidai
Mwampamba.
Alipoulizwa ni kwanini viongozi wa Chadema
wanataka kumuua Zitto, alisema ni kwa sababu ya uhusiano mbaya baina yake na
vigogo hao ambao chanzo chake ni hatua ya kutaka kugombea urais na kutomuunga
mkono Dk. Slaa katika harakati zake za kuwania urais mwaka
2010.
“Zitto hana uhusiano mzuri na viongozi wa juu
wa Chadema. Nia yake ya kutaka kugombea urais hawaipendi, inawaudhi sana na
amekuwa akitofautiana nao kwa mambo mengi, anajua kuwa anawindwa ndiyo maana
hata oparesheni za M4C hashiriki.
“Mimi nilikuwa Chadema na nilikuwa karibu
sana na Zitto, najua nini kilikuwa kinaendelea juu yake na najua baadhi ya mambo
ya Chadema. Ninaijua mipango ya mauaji ya Chadema. Zitto aliwahi kuwekewa sumu
Bagamoyo wakati wabunge wa chama hicho walipokuwa kwenye mkutano wao
huko.
“Alinusurika kufa. Alipona baada ya sumu hiyo
kutolewa mwilini mwake. Waliiflashi.” Alidai Mwampamba.
Alidai kuwa Zitto alipata kunusurika katika
ajali ya gari wakati akitokea Bagamoyo kuelekea Iringa, baada ya gari alilokuwa
akitumia kulegezwa nati zinazofunga tairi. Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada
ya Zitto na Mbowe kutupiana maneno makali kwenye
mkutano
Kauli ya
Saanane
Akizungumza na Mtanzania
Jumatano jana kupitia simu yake ya kiganjani, Saanane alisema madai yaliyotolewa
na Shonza na Mwampamba dhidi yake siyo ya kweli, kwa sababu wanayodai kuwa
walimkamata akiwa na sumu, hakuwa nao.
Alisema kwa mujibu wa
kumbukumbu zake, siku ya Desemba 5, mwaka jana, alikuwa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, akikutana na wanaharakati na baadaye jioni alikwenda
harusini.
Hata hivyo, alipoulizwa
iwapo alipata kukutana na Shonza na Mwampamba katika Hotel ya Lunch Time,
Saanane alisema amepata kukutana nao mara kadhaa kwa ajili ya kupanga mikakati
ya PM7, ambayo alishiriki kuianzisha lakini aliachana nao baada ya kubaini
walikuwa wakiitumia kwa malengo mabaya.
Mtanzania Jumatano
lilipombana Saanane aeleze mikakati waliyokuwa wakiipanga yeye na wenzake katika
PM7, alisema ilikuwa ya siri na vikao vyao vilikuwa vya siri kutokana na hofu ya
kufikiriwa vibaya na viongozi wa chama iwapo wangebainika wanajihusisha na kundi
hilo.
Alipoulizwa kama
anafahamiana na Zitto na wapi amekwishakutana naye, alisema anamfahamu na
amekuwa akikutana mara kwa mara huku akishangaa tamko lake kwenye mitandao ya
kijamii lilikokuwa likieleza kuwa, hamfahamu na hata akimuona anaweza kupishana
naye.
Hata hivyo, baadaye Saanane
aliomba anuani ya barua pepe ya Mhariri wa gazeti hili na kumtumia barua ya
kumtaka amuombe radhi kwa kuandika habari ya uongo iliyokuwa ikieleza madai ya
masharika wake wanaomuhusisha na tuhuma za kutumwa kumuwekea sumu Zitto, pasipo
kumtafuta Zitto mwenyewe kuzungumza hata neno
moja
Vituko vya Dk.
Slaa
Dk. Slaa alipotafutwa kwa
simu yake ya kiganjani na kuulizwa kuhusu madai hayo, alianza kuporomosha matusi
mazito huku akilituhumu gazeti hili kutoa nafasi ya kuandika habari zinazowagusa
viongozi wa Chadema badala ya kuandika habari za
maendeleo.
“Sina muda wa kujibu
maswali hayo… hayana msingi…tuhuma hizo hazijadiliwi kwenye magazeti……ni masuala
ya kijinga…pumbavu kabisa. Acheni upumbavu bwana. Nina mambo mengi ya msingi ya
kitaifa ya kushughulikia kuliko haya madai ya kipumbavu.” Aling’aka Dk.
Slaa.
Hata gazeti hili
lilipomsihi awe mtulivu ili aweze kutoa ushirikiano, aliendelea kufoka huku
akiporomosha matusi zaidi kabla halijaagana naye na kukata
simu.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe simu yake iliita muda wote bila majibu na hata
Zitto.
CHANZO:MTANZANIA
GAZETI
Post a Comment