Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Kanda ya Afrika Mashariki nchini Tanzania (ILO)  Bw. Alexio Musindo akikagua kinywaji aina ya ‘paw paw wine’ na mkononi akiwa ameshika matunda aina ya ‘rozela’ yanayotumika kwa kutengenezea ‘juice’ wakati alilipotembelea kikundi cha Chimbuko kinachoundwa na watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Mjini Kyela mnamo tarehe 2, Aprili 2013 ili kujua maendeleo yao. Kikundi cha Chimbuko ni moja kati ya vikundi vya kijamii vinanvyonufaika na mradi wa UKIMWI kwa njia ya uwezeshaji Kiuchumi unaoratibiwa na ILO katika maeneo ipitayo njia kuu ya Tanzania – Zambia. (yaani Chalinze, Ilula, Mafinga, Makambako, Kyela na Tunduma). 
Mwenyekiti wa kikundi Cha Chimbuko Bi Sara Mwakinyuke akimwelezea Ndugu Alexio Musindo, Mkurugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki nchini Tanzania kuhusu matumizi ya bidhaa aina Rozela. Alifafanua pia miongoni mwa bidhaa wanazotengeneza ni pamoja na mmea wa asili aina ya mlonge ambapo alisema mlonge hutumika kama dawa inayotibu malaria. Kushoto kwake ni Afisa Mratibu Mkuu wa ILO nchini Tanzania Ndugu Anthony Rutabanzibwa aliyeongozana na Mukurugenzi wa ILO katika ziara hiyo.
Miongoni mwa vitu vilivyowashangaza maafisa wa ILO walipotembelea kikundi cha Chimbuko ni mmea wa Rozela na matunda yake kwani miongoni mwao hawajawahi kuona mmea huo bali matunda yake yakiwa tayari yameshahifadhiwa katika vifungashio. Sambamba nalo ni kitafunwa aina ya keki ya muhogo ambayo Mkurugenzi wa ILO kanda ya Afrika Mashariki alishangazwa baada ya kula keki hiyo namna ambavyo hata unga wa muhogo pia unaweza kutengenezwa keki na ikawa tamu kwelikweli!

Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani Kanda ya Afrika ya Mashariki nchini Tanzania Ndugu Alexio Musindo akiangalia bidhaa aina ya unga uitwao ‘SHIBE’ wenye mchanganyiko wa ulezi, soya lishe, mchele, karanga na mahindi unaosindikwa na kikundi cha chimbuko kama lishe bora inayoweza kutumiwa na watu wa rika zote wakiwemo wanaoishi na VVU na UKIMWI, wazee na watoto
Mwenyekiti wa vikundi cha Chimbuko Bi. Sara Mwakinyuke akimwelezea Ndugu Alexio Musindo, Mkururugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki nchini Tanzania juu ya changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika kujipatia kipato kupitia bidhaa wanazozalisha ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifungashio kwa ajili ya bidhaa wanazozalisha, kutoshiriki katika maonyesho ya Kitaifa ya biashara na ujasiriamali na kukosa elimu ya kutosha kuhusu uzalishaji wa bidhaa zao. Ndugu Alexio Musindo aliwaahidi kuwawezesha kupata vifungashio na Uongozi wa Halmashauri ya Kyela kupitia idara ya UKIMWI kuwaahidi kuwawezesha ili washiriki katika maonyesho ya saba saba mwaka 2013 yatakayofanyika mjini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kikundi cha wanawake wajasiriamali cha Faith kilichopo  Mjini mbeya Bi Helene Sanga akifafanua jambo baada ya kutembelewa na Ndugu Alexio Musindo, Mkururugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki nchini Tanzania mnamo tahere 2 Aprili 2013 kuhusu bidhaa wanazotengeneza aina ya BATIKI na changamoto wanazokumbana nazo ikiwemo ufinyu wa mtaji wa kikundi ili kuweza kuzalisha aina mbalimbali za BATIKI na kushiriki katika maonyesho ya kimataifa ya kibiashara. Kikundi cha Faith ni moja kati ya vikundi vya Kijamii na Vyama vya Ushirika mjini Kyela vinavyonufaika na mradi wa UKIMWI na uwezeshaji wa Kiuchumi unaoratibiwa na ILO.
 
Katibu wa Kikundi cha Mshikamano wajasiriamali mjini Kyela mkoani Mbeya Bw. Nazar Mwaipasi akifafanua kuhusu maendeleo ya kikundi ikiwa ni pamoja na kuanzisha SACCOS punde baada ya kutembelewa na Ndugu Alexio Musindo, Mkururugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki nchini Tanzania mnamo tahere 2 Aprili 2013.Bw. Nazar aliongeza kuwa kikundi cha Mshikamano kinachoundwa na wanawake na vijana wa kike na kiume wanaojihusisha na biashara binafsi na usindikaji wa vyakula kama mafuta ya mawese, samaki, mapishi na biashara ya mchele, kiliundwa baada ya mafunzo ya ujasiriamali na UKIMWI yaliyotolewa kwa wanawake na vijana kupitia mradi wa UKIMWI na uwezeshaji wa Kiuchumi wa ILO. 
Moja kati ya maeneo ya uzalishaji wa kinywaji kiitwacho ‘wine’ katika kikundi cha Chimbuko alipotembelea Ndugu Alexio Musindo, Mkururugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki nchini Tanzania mnamo tahere 2 Aprili 2013. Ndugu Musindo aliwaeleza wanawake wa Kikundi cha Chimbuko kuwa malengo ya shirika la kazi Duniani katika kuwasaidia wanawake wajasiriamali yatawezekana tu pale ambapo Serikali itakuwa na Sera thabiti za kuwasaidia kuwalinda na kuwawezesha kiuchumi ndipo tutakapopata uzalishaji utakaowawezesha kimapato na kuwekwa sheria zitakazowalinda kijamii.
Mkururugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki nchini Tanzania Ndugu Alexio Musindo (wa pili kushoto)akinunua baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wanaoishi na VVU Chimbuko mjini Kyela baada ya kutembelea katika jengo wanalouzia bidhaa zao mapema tarehe 2 Aprili 2013 ili kujua maendeleo ya mradi wa UKIMWI unaoratibiwa na ILO katika wilaya ya Kyela. Kutoka kulia ni Afisa Maendeleo Mkuu wa Wilaya ya Kyela ndugu Omari Mungi, Afisa Mratibu Mkuu wa ILO nchini Tanzania ndugu Anthony Rutabanzibwa, na Mratibu Msaidizi wa Mradi wa UKIMWI ILO nchini Bi. Getrude Sima (kushoto). 
Hili ni jengo linalomilikiwa na Kikundi cha Chimbuko katika Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya na ndilo eneo wanalouzia bidhaa zao mahali ambapo mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani nchini ndugu Musindo alipata fursa ya kutembelea mnamo tarehe April 2, 2013. Wito wa Chimbuko kuomba wahisani ikiwemo serikali kuwaboreshea mazingira yao ya kazi ili waweze kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokidhi mahitaji na kupata ushindani mzuri katika soko kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kuongeza kipato, ajira na kuondokana na umasikini. 
Mkururugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki nchini, Ndugu Alexio Musindo akipeana mkono na Meneja wa Kimbalu SACCOS ndugu Aggrey Mwambije alipotembelea ofisini hapo mnamo tarehe 2 Aprili 2013 kujua maendeleo ya wanaonufaika na mradi wa UKIMWI na uwezeshaji Kiuchumi unaoratibiwa na ILO. Kimbalu SACCOS ipo mpakani mwa Tanzania na Malawi (Kasumulu)katika wilaya ya Kyela na wanachama wake wananufaika na mradi huo. 
Wakionekana wenye nyuso za furaha ni wanachama wa Kimbalu SACCOS katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani nchini Tanzania ndugu Alexio Musindo punde baada ya kupata taarifa ya mafanikio ya mradi mnamo tarehe 2 Aprili 2013. Kimbalu SACCOS in waelimisha rika mahiri 21 waliopata elimu ya UKIMWI kupitia mradi wa ILO wa UKIMWI.
 
Mkurugenzi wa ILO nchini Tanzania akinong’ona jambo na Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Mji Mdogo Tunduma Bi. Deonisia Kafuka wakielekea katika ziara ya kutembelea vikundi vya kijamii vinanvyonufaika na mradi wa ILO wa UKIMWI na uwezeshaji wa Kiuchumi mnamo tarehe 2 Aprili 2013. Katika ziara hii Ndugu Musindo pia alipata fursa ya kufanya kikao na viongozi wa serikali wa Halmashauri ambapo alipata kuelezwa kuwa Tunduma ni mji unaokuwa kwa kasi kibiashara na pia tatizo la utumikishwaji wa watoto ni kubwa hivyo kutoa wito kwa ILO na UNICEF waangalie jinsi gani wanaweza kusaidia kutatua tatizo hili.
Wanawake wa Kikundi cha Amani ‘A’ kinachojishughulisha na shughuli za usindikaji wa vyakula, ufumaji wa mashuka na mikeka na kilimo pia waliweza kutembelewa na Mkurugenzi wa ILO nchini Tanzania. Wakinamama hawa walipata wasaaa wa kumwelezea Mkurugenzi wa ILO nchini kuhusu maendeleo wanayopata kupitia shughuli zao sambamba na kupata mafunzo ya ujasiriamali kutoka ILO kupitia waelimishaji wake. Pia waliweza kubainisha changamaoto zinazowakabili kama upungufu wa vifaa vya uzalishaji zikiwemo cherehani na mitaji midogo. Mkurugenzi wa ILO nchini aliwaahidi kuwa ILO itazidi kuwasaidia ili waweze kuondokana na hali ya umasikini na athari zitokanazo na UKIMWI.
Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani nchini ndugu Alexio Musindo akiwa katika moja ya kiwanda cha ufumaji cha wana kikundi wa Amani ‘A’ mjini Tunduma baada ya kuwatembelea mnamo tarehe 2 Aprili 2013. Kikundi hiki ni moja ya vikundi vilivyopokea elimu ya ujasiriamali na UKIMWI inayotoelewa na ILO chini ya Mradi wa UKIMWI.
 
Hizi ni baadhi ya mashine mbili za ushonaji (vyerehani) zinazomilikiwa na kikundi cha Amani ‘A’ mjini Tunduma.
Mkurugenzi wa ILO pia alipata nafasi ya kuonana na viongozi na baadhi ya wanachama wa SACCOS ya Lulu Tunduma ambayo pia inanufaika na elimu ya mradi wa ILO wa UKIMWI. Tunduma Lulu SACCOS ina jumla ya waelimisha rika mahiri 9 waliopata mafunzo kupitia mradi huu ambao huendeleza mafunzo kwa wanachama wao.