*WAITAKA TFF KUTOA SABABU KWANINI WABADILISHE MWAMUZI WA KIPUTE CHA WATANI WA JADI GHAFLA!
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe Dar es salaam
WEKUNDU
wa Msimbazi Simba “Taifa Kubwa” wameshangaa na maamuzi ya ghafla ya
shirikisho la soka nchini Tanzania TFF kufanya maamuzi ya kubadilisha
mwamuzi wa kati atakayechezesha kipute cha jumamosi cha watani wa jadi
katika dimba maridhawa la taifa jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Usajili ya Simba, mjumbe wa kamati ya utendaji ya klabu
hiyo na mratibu wa timu katika mashindano, Kaptein Zacharia Hans Poppe
ameimabia FULLSHANGWE kuwa wamegundua kuwepo kwa njama za watani wao wa jadi kutokana na mabadiliko hayo yaliyofanywa bila kukaa na timu husika.
“Yanga
wana mchecheto na timu ya vijana ya Simba, wana wasiwasi kubwa sana na
ndio maana wameanza njama. Toka wiki iliyopita walitaka kubadilishia
mwamuzi tofauti na Israel Nkongo aliyepangwa toka mwanzo”. Alisema
Poppe.
Poppe
amesema viongozi wa kamati ya utendaji ya Simba wanakutana kujadili
suala hilo na wamewataka wanahabari kuwabana TFF kueleza sababu za
kufanya mabadiliko hayo bila taarifa.
Kiongozi huyo alihoji kama Nkongo siku hiyo atakuwa na dharura au atakuwa mgonjwa siku ya jumamosi?
“Sisi
habari hizi tumeziona kwenye mitandao, nasikia waandishi waliuliza
katika mkutano wa TFF kwanini wamebadilishe mwamuzi, lakini TFF
wametuma habari kuwa mwamuzi atakuwa Saanya kutoka Morogoro, watoe
sababu za msimgi kwanini wamefanya hivyo.”. Alisema
Saanya
kutoka mji kasoro bahari Morogoro ndiye ameteuliwa kuchezesha pambano
la watani wa jadi, Simba na Yanga SC siku ya jumamosi huku akisaidiwa
na Samuel Mpenzu wa Arusha, Jesse Erasmo kutoka Morogoro, wakati
mwamuzi msaidizi atakuwa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam.
Kamisaa
wa mechi hiyo atakuwa Emmanuel Kavenga kutoka Mbeya wakati mtathmini wa
waamuzi atakuwa ni Leslie Liunda wa Dar es Salaam.
Mashabiki
watalipa Sh. 5,000 kwa lugha ya mitaani “Buku Tano” kikiwa kiingilio
cha chini zaidi katika sehemu ya viti vya Rangi ya Bluu.
Viti vya rangi ya kijani itakuwa sh. Elfu saba (7000/=), wakati viti vya rangi ya chunga itakuwa sh. Elfu kumi (1000).
Kwa wale wenye pesa zao viingilio vitakuwa ni Sh. 15,000 kwa VIP C, Sh. 20,000 kwa VIP B na Sh. 30,000 kwa VIP A.
Ofisa
Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura Mgoyo
alisema kuwa viingilio hivyo ni sawa na viingilio vya mchezo wa mzunguko
wa kwanza wa ligi hiyo baina ya klabu hizo Oktoba 3 mwaka jana ambapo
zilitoka sare ya 1-1.
Wambura alisema tiketi zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo, yaani Ijumaa wiki hii katika vituo mbalimbali vitakavyotajwa.
Yanga
wanakumbuka kipigo cha 5-0 msimu wa mwaka jana na kinawazunguka zaidi
vichwani na wanahitaji kulipa kisasi msimu huu ambapo tayari ni
mabingwa, wakati Simba wana hasira ya kupoteza nafasi ya ubingwa na
mshindi wa pili msimu huu.
Simba kwa sasa inawatumia vijana zaidi wakati Yanga inawatumia mafaza wote na vijana wake.
Tusubiri
nini kitatokea siku ya jumamosi uwanja taifa jijini Dar es salaam,
majira ya saa kumi kamili jioni kwa saa za Afrika Mshariki.
Yanga
wameweka kambi yao kisiwani Pemba katika hoteli ya Samail mkabala na
benki ya PBZ, wakifanya mazoezi Uwanja wa Gombani wakati Simba wameweka
kambi maeneo ya Mbweni JKT Zanzibar wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa
Mao Dze Tung.
Post a Comment