POLISI
saba kutoka wilayani Kasulu, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama
Kuu Kanda ya Tabora, iliyoanza kikao chake mjini Kigoma leo na kusomewa
mashitaka ya kuua kwa kukusudia. Mbele ya Jaji Sam Rumanyika, askari
Polisi hao walidaiwa kuwa Agosti 6, 2011 walimpiga
na kumuua kwa makusudi Festo Stephano, mkulima na mkazi wa Kijiji cha Rungwe mpya wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Waliopandishwa
kizimbani na kusomewa mashitaka yao ni pamoja na Baraka Hongdi, Koplo
Mawazo, Koplo Swahib, Koplo Charles, Koplo Shamsi, Koplo Jerry na Koplo
Amrani ambao kwa pamoja walikana mashitaka.
Baada
ya kukana mashitaka, kesi hiyo ilianza kusikilizwa kwa mashahidi wa
upande wa Jamhuri kuanza kutoa ushahidi wao, ambapo shahidi wa kwanza
katika kesi hiyo, Masumbuko Stephano, aliieleza Mahakama kwamba askari
hao walikusudia kufanya mauaji hayo.
Masumbuko
aliieleza Mahakama kwamba siku ya tukio, alikamatwa pamoja na marehemu
na mgambo wa kijiji, na kuwekwa katika mahabusu ndogo katika Ofisi ya
Mtendaji wa Kata.
Alidai
baada ya kufika, askari hao walianza kuwapiga kwa kutumia vitako vya
bunduki, fimbo na chupa za bia, hali iliyosababisha wapatwe na maumivu
makali.
Shahidi
huyo alidai kuwa baada ya kupigwa na kukaribia kupoteza fahamu, polisi
hao waliwavua nguo, wakawafunika na turubai ndani ya gari ambapo baadaye
walinunua magunia ya mkaa na kuwakandamiza na magunia hayo.
Shahidi
wa pili katika kesi hiyo, Andrea Sama, alidai kwamba askari hao
walikusudia kufanya mauaji siku hiyo, kwani licha ya kutoa kipigo pia
waliwavua nguo na kuwaingiza miti kwenye sehemu zao za haja kubwa.
“Mheshimiwa
Jaji kwa kweli nilishuhudia vitendo vya askari hao kwa macho yangu, na
nilishindwa kuamini kama jambo hilo linafanyika kwenye ardhi ya Tanzania
au tuko nchi nyingine, maana unyama uliofanywa na askari polisi hao
huwezi kudhani kama ni walinzi wa amani katika nchi hii,” alidai Sama.
Kesi
hiyo itaendelea kusikilizwa mfululizo hadi kutolewa hukumu, ambapo
mwanasheria mwandamizi wa Serikali, Juvelin Rugaihuruza, alidai kuwa
upande wa Jamhuri ambao ndiyo mlalamikaji, unatarajia kuwa na mashahidi
12 na vielelezo viwili.
Washitakiwa
hao wanatetewa na Mwanasheria, Method Kabuguzi, kutoka Kampuni ya
Uwakili ya Kigoma Law Chamber and Advocate ya mjini Kigoma.
Post a Comment