Dar es Salaam. Kauli
ya Serikali iliyotolewa bungeni juu ya kufutwa kwa matokeo ya mtihani
wa kidato cha nne na sababu za kufeli kwa wanafunzi wengi, imeibua utata
baada ya taarifa kadhaa kuonyesha kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi ilibariki mabadiliko ya mfumo mpya wa kupanga madaraja.
Taarifa
ya Serikali iliyosomwa bungeni Mei 3, mwaka huu na Waziri wa Nchi Ofisi
ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi(Pichani) ilisema
Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), lilifanya mabadiliko ya mfumo bila
kushirikisha wadau.
“Baraza
la Taifa la Mitihani lilikuwa linachakata alama za mwisho kwa kutumia
mfumo ambao ulikuwa unabadilika kwa kutegemeana na hali ya ufaulu wa
mwanafunzi... lakini mwaka 2012 lilitumia mfumo mpya wa kuwa na viwango
maalumu vya kutunuku (fixed grade ranges).”
“Tume
imebaini kwamba, pamoja na mfumo huo kuandaliwa kwa nia nzuri,
utaratibu huo mpya haukufanyiwa utafiti na maandalizi ya kutosha kabla
ya kutumika.
“Baraza
la Taifa la Mitihani limeelekezwa kuzingatia kuwa pamoja na kwamba
sheria ya kuanzishwa kwake inawaruhusu kufanya marekebisho ya mchakato
wa mtihani, lakini marekebisho yoyote ya kubadilisha utaratibu wa
kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya matokeo ya mtihani lazima
yahusishe wadau wote wanaohusika na mitalaa, ufundishaji na mitihani.”
Kwa
mujibu wa vielelezo vilivyochapishwa na Gazeti la Wiki la Jamhuri,
mfumo huo ulipitishwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi.
Nyaraka
hizo zinaonyesha kuwa, kikao kilichokutana na kujadili mapendekezo ya
Necta ya kubadili mfumo huo kiliongozwa na Waziri wa Elimu, Dk Shukuru
Kawambwa na Katibu wake alikuwa Naibu Waziri wa Elimu, Philip Mulugo.
Muhtasari
wa kikao hicho unaonyesha wajumbe wa mkutano huo walikuwa ni pamoja na
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Selestine Gesimba, Kamishna wa Elimu,
Profesa Eustell Bhalalusesa, Paulina K Mkonongo, Marystella Wassena,
T.E. Temu, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi
(Nacte), Dk Primus Nkwera, Bunyanzu Ntmabi, H.A Lihawa wote wakiwa
wajumbe kwa upande wa Wizara.
Kutoka
Necta wajumbe walikuwa ni Dk C.E Msonde, Katibu Mtendaji wa Baraza
hilo, Dk Joyce Ndalichako, Mwenyekiti wa Bodi ya Necta, Profesa Rwekaza
Mukandara pamoja na Profesa Sifuni Mchome, ambaye ni Katibu Mtendaji wa
Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).
Aidha,
Gesimba alimwandikia barua Katibu Mtendaji wa Necta yenye kumbukumbu
namba CAC.109/437/01N Desemba 12 mwaka jana akiliagiza kutumia mfumo
mpya wa kukokotoa alama za mitihani ya kidato cha nne na sita.
“Tafadhali
rejea kikao kilichofanyika tarehe 10/12/2012 katika ukumbi wa mikutano
wa wizara kuhusu somo tajwa hapo juu (Maagizo ya kuhusu utaratibu wa
matumizi ya viwango vya ufaulu katika mitihani ya kidato cha nne na
sita).
“Viwango
vya ufaulu vilivyopendekezwa na Baraza la Mitihani la Tanzania vitumike
kwa mitihani ya Kidato cha Nne 2012 na Kidato cha Sita kwa mwaka 2012
tu.
“Viwango
vya kutunuku (grade rage) vifanyiwe kazi zaidi ili kupunguza au kuondoa
mrundikano (bunching) wa alama katika kundi moja.”
“Necta
ifanye utafiti kuhusu matumizi ya alama za maendeleo kwa O level
(kidato cha kwanza mpaka cha sita) na A Level (kidato cha tano na sita)
na kutoa mapendekezo mapya ya matumizi ya alama za maendeleo (continuous
assessment).”
“Utekelezaji
wa maagizo haya ufanyike mapema ili mapendekezo yaliyowasilishwa yaweze
kuanza kutumika katika Mwaka wa Fedha 2013/2014.”
Mbali
na barua hiyo, Profesa Bhalalusesa aliandika barua kwa Katibu Mtendaji
wa Necta, Novemba 14, mwaka huu kuhusu utaratibu wa matumizi ya alama za
maendeleo ya mtihani na viwango vya ufaulu katika mitihani ya taifa.
“Rejea
kichwa cha habari hapo juu na barua yako yenye kumbu Na. MTS.
1/29/VOL.XII/61 ya tarehe 20/09/2012. Kutokana na maelezo ya barua yako,
Wizara imeridhia mapendekezo ya uwiano wa alama za maendeleo ya
wanafunzi (CA) na alama za mtihani wa mwisho kubadilishwa kutoka alama
50:50 na kuwa 30:70.”
“Wizara inaridhia pia alama 15 zitokane na mtihani wa kidato cha pili kwa wanafunzi wa kidato cha nne.”
“Aidha,
wizara inataka mlete mchanganuo wa jinsi alama 15 zilizobakia
zitakavyopatikana ili kuleta uelewa wa pamoja. Vivyo hivyo, mchanganue
utaratibu wa mgawanyo wa alama za maendeleo ya mwanafunzi wa kidato cha
sita,” ilisema.
Akizungumza
jana, Dk Kawambwa alisema hawezi kuzungumza chochote na badala yake
atafutwe Mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza Kushuka kwa Kiwango cha Ufaulu
wa Mtihani huo, Profesa Sifuni Mchome kwa kuwa kwa sasa masuala yote
yapo chini yake.
“Naomba
nisi-comment (nisizungumze) chochote kwa sasa, muulizeni Profesa Mchome
kwa kuwa sasa hivi mambo yote yapo chini ya tume, nikizungumza
nitawaudhi,” alisema.
Hata
hivyo, jana Profesa Mchome ambaye pia alikuwa mjumbe wa kikao
kilichopitisha mapendekezo hayo ya awali, hakupatikana kuzungumzia madai
hayo lakini juzi akizungumza na mwandishi wetu alisema tume yake
ilibaini kuwa Necta na wizara walikubaliana mwaka jana kuanza kutumia
kanuni hiyo na utekelezaji wake ukaanza mwaka jana jambo ambalo halikuwa
sawa.
Alisema
mabadiliko makubwa kama hayo yalipaswa kuchukua angalau miaka minne ili
watoto waandaliwe kuanzia kidato cha kwanza na waje wapimwe wanapofika
kidato cha nne.
“Vyote
hivi ni vyombo vya Serikali (Necta na Wizara ya Elimu) kwa hiyo
kujikosoa siyo tatizo, sisi tumeona hilo ni tatizo na tukapendekeza
hivyo na Serikali ikaamua kujikosoa,” alisema.
Alisema
kuwa baada ya mabadiliko yanayoweza kufanyika bila kushirikisha
wataalamu wengi lakini suala la alama za mtihani kwa kuwa tayari matokeo
yake yameonekana baada ya kujaribiwa, ni vyema wadau wakashirikishwa
zaidi
Post a Comment