Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Dkt. Salhia Muhsin Ali akitoa maelezo mbele ya Kikao cha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Wanafunzi wanaosoma mafunzo ya Udaktari katika Chuo cha Afya waliopo Wawi Kisiwani Pemba.
Picha juu na chini ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wanafunzi 12 wa Chuo cha Afya wanaosomea fani ya Udaktari waliopo Kisiwani Pemba.
Rais wa Wanafunzi wa chuo cha afya waliopo Kisiwani Pemba Ali Omar Khalifa akitoa baadhi ya changamoto zinazowakabili wanafunzi wa chuo cha afya waliopo Kisiwani Pemba.
Mwalimu Mkuu wa Wanafunzi wa Chuo cha Afya waliopo Pemba Dr. Maria Makdalema akielezea furaha yake kutokana na umahiri wa wanafunzi wake mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipowatembelea kwenye makazi yao Wawi Pemba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Mwalimu Mkuu wa Wanafunzi wa chuo cha Afya waliopo Kisiwani Pemba Dkt. Maria Makdalema. Pembeni yao ni Afisa Mdhamini Wizara ya AfYA Pemba Mkasha Hija Mkasha na Mkurugenzi Idara ya Tiba Zanzibar Dkt Salhia Muhsin Ali. (Picha na Hassan Issa wa – OMPR)– ZNZ.
*****
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari kumgharamia mwanafunzi yeyote atakayeamua kujiongezea taaluma ya fani yoyote ya Udaktari Bingwa kwa lengo la kuipunguzia Zanzibar uhaba wa Madaktari.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wakufunzi pamoja na Wanafunzi wa chuo cha afya wanaosomea fani ya Udaktari chini ya Wataalamu wa Cuba waliopo Wawi chake chake Pemba.
Balozi Seif amesema uwamuzi huo wa serikali umelenga kukidhi Mpango wake uliojipangia wa kuimarisha huduma za Afya katika kila umbali wa Kilomita Tano katika Visiwa vya Zanzibar.
Amesema Serikali katika kukabiliana na upungufu wa Madaktari bingwa wa fani tofauti imetowa fursa hiyo ili Daktari mwenyewe awe huru kuamua kuongeza ujuzi zaidi katika Nchi na fani aiwezayo huku akilenga kuja kuisaidia Jamii yake mara amalizapo mafunzo hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewapongeza Wanafunzi hao kwa ushiriki wao wa mafunzo hayo ya miaka saba na kuelezea matumaini yake kwamba wamalizapo mafunzo hayo ni kutoa huduma kwa kuzingatia maadili ya Udaktari.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaangalia na kuimarisha mazingira ya walimu pamoja na wanafunzi hao ili waweze kufanikisha lengo lililokusudiwa chuoni hapo.
Wakitoa baadhi ya changamoto zinazowakabili Wanafunzi hao wa Udaktari walisema upungufu wa vifaa limekuwa tatizo sugu linalorejesha nyuma mafunzo yao ya kila siku.
Wameiomba Serikali kupitia Wizara ya afya kuyafanyia kazi matatizo hayo likiwemo pia tatizo la mtandao wa Internet kwa wakufunzi wao sambamba na usafiri kwa wanaokwenda na kurudi kwenye mazoezi hasa wakati wa usiku.
Post a Comment