Jumuiya ya Wafanyabiashara
wa Kariakoo wameahidi kuendelea kutafuta suluhu kwa njia ya mazungumzo na
serikali juu ya mgogoro wa makontena ambayo yamezuiliwa bandarini, kitendo
ambacho kimeathiri biashara zao kwa mda mrefu sasa kwani wemeshindwa kufanya
biashara ndani na nchi jirani kwa takriban zaidi ya wiki
tatu.
Tamko hili lililotolewa na
Jumuiya Hii wiki iliopita, limeeleza kuwa tayari wametuma maombi kwa wizara
husika na idara za serikali za mapato ili kuwepo na mkutano utakaoweza kutizama
jinsi ya kutatua mgogoro wa makontena zaidi ya 400 ambayo yamezuiliwa
bandarini.
Katika tamko hilo imeelezwa
kuhusu dhamira yao ya kukutana na Waziri wa Fedha na Uchumi, Waziri wa Viwanda
na Uwongozi wa TRA pamoja na vyombo vingine husika ili kujadili na kutafuta
ufumbuzi wa kile wanachodai ni ongezeko la kodi.
Wanasisitiza kuwa kuwepo
kwa pande zote hizi kwenye mkutano kutawezesha kufikia
ufumbuzi.
Jambo lililopelekea kufikia
uamuzi huu wa kukutana na viongozi ni kile walichokiita kutekwa nyara kwa kikao
cha awali kilichofanyika na Waziri wa Fedha ambapo Chama cha Mawakala wa
bandarini kilifunika nafasi hiyo kwa kujadili matatizo yao wenyewe bila ya
kujali kero inayowakabili wafanyabiashara ambao tayari wameanza kupata hasara
kutokana na makotena yao kukwama.
Wafanyabiashara
wamelalamika juu ya mawakala kuingia katika malumbano yao binafsi juu ya
ushindani wa kibiashara badala ya kutafuta suluhisho la makontena yalio na
bidhaa za wafanyabiashara hawa wadogo wadogo.
Hata hivyo tamko la
wafanyabiashara limeweka wazi kuridhika kwao na maelekezo yaliyotelewa na Waziri
wa Fedha na maafisa wa TRA juu ya kukubali kwao kufanya kikao haraka na
wafanyabiashara hawa.
Wafanyabiashara pia
wametakiwa kujaza fomu upya ambazo zitaeleza upya aina za bidhaa walizoleta
nchini na vielezo kamili vya bidhaa hizo ili vifanyiwe uhakiki
upya.
Pia wamehakikishiwa kuwa
hawatatozwa faini kwa makosa yoyote yatayobainika baada ya kuhakiki fomu zao
upya, iwapo zitakuwa na dosari.
Jumuiya hiyo pia imesema
kwamba iwapo kulikuwa na ukwepaji wa kodi basi badala ya TRA kuwaadhibu wao
nivema wangechukua hatua dhidi ya wale wote waliokwenda
kinyume.
Katika malalamiko yao
wanadai kuwa ushuru wa forodha (Import duty) na VAT zimeongeka mara mbili bila
ya wao kupewa taarifa.
Pia wanadai kuwa TRA
haikufuata utaratibu katika kuongeza kodi.Wanadai pia wafanyabiashara
wanalalamika juu ya HS Code ambayo inatumika kuonyesha aina ya bidhaa mbali
mbali na ushuru wake kwa madai ya kuwa imechakachuliwa.
Lakini wafanyabiashara
wameendelea kusisitiza kuwa wao ni wananchi wenye kutii sharia za nchi na wako
tayari kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili katika meza ya
mazungumzo.
Wameelezea jinsi
walivyoanza kupoteza wateja wao mara baada ya mizigo yao kuzuiliwa bandarini,
ikiwa ni pamoja na usumbufu mkubwa kwa wateja wao ambao wanatoka katika nchi za
Afrika mashariki na nyinginezo.
Wamesema hivi sasa kuna
uwezekano wa wateja wao kuhama na kufanya biashara nchi nyingine jambo ambalo
litaipotezea taifa kiwango kikubwa cha pato la taifa.
Wafanyabiashara hao wanadai
kuwa tayari wapo wenzao ambao wamekufa kutokana na kutetereka kwa biashara zao
baada ya kuambiwa walipe kodi kubwa ambayo imewaletea mshituko mkubwa hadi
kufikia kupoteza maisha.
Kwa mujibu wa takwimu
zilizotolewa na jumuiya, tayari mali ya mabilioni imekwama na gharama za
kuukomboa zinaongezeka.
Post a Comment