AFISA Usalama wa Taifa, Peter Patrick Tyenyi ,53, (pichani) ambaye maiti yake ilikutwa Mei 27, mwaka huu katika kisima cha maji masafi kilichopo maeneo ya ofisini kwao, Kijitonyama Makumbusho jijini Dar, kifo chake kimetajwa kuwa ni cha kimafia.
Chanzo chetu makini ndani ya familia ya marehemu kimedai kuwa wao wanaamini kuwa ndugu yao hakufa kifo cha kawaida isipokuwa kuna mkono wa mtu.
Wanafamilia hao wanadai kuwa kifo hicho ni cha kimafia kwa sababu kisima kilichokutwa mwili huwa siyo rahisi mtu kuingia bila kuonekana.
Habari zinasema siku hiyo ya kutoweka kwake, asubuhi afisa huyo alitoka nyumbani kwake maeneo ya Kijitonyama akiwa na afya njema.
Kiliendelea kusema kwamba mara baada ya afisa huyo kufika ofisini, walikaa kikao cha kazini na mara baada ya kumalizika hakuonekana tena.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa ofisa huyo alitafutwa kwa njia ya simu baada ya kutoonekana ofisini kwa saa kadhaa lakini zote zikawa hazipatikani.
Imeelezwa kuwa baadhi ya wafanyakazi wenzake waliingiwa na hofu kwa vile haikuwa kawaida yake kuondoka ofisini bila kuaga na hakuwa na tabia ya kuzima simu zake zote.
Habari zaidi zinaeleza kuwa kutoonekana kwa marehemu kwa saa kadhaa, kuliwafanya ndugu zake wapigiwe simu na maofisa wa idara ya usalama wa taifa kuulizwa na ikabidi wafike ofisini kwake ili kupata taarifa kamili.
Inasemekana kuwa mara baada ya ndugu hao kupewa taarifa hizo waliingiwa hofu, hali iliyowafanya waanze kutembelea baadhi ya hospitali za hapa Dar lakini hawakufanikiwa kupata taarifa zozote kuhusu ndugu yao huyo.
Wakati ndugu zake wanaendelea kumtafuta kwa siku za Jumanne na Jumatano, zikapatikana taarifa kuwa kuna mwili umeonekana katika kisima cha maji masafi kilichopo maeneo ya ofisini kwake.
Imedaiwa kuwa siku ya Alhamisi ambayo mwili ulionekana, maji yalikuwa yamekatika na mmoja wa wafanyakazi wa idara hiyo alikwenda kwenye kisima hicho ndipo alipouona mwili na kutoa taarifa kwa uongozi.
Imeelezwa kuwa baada ya uongozi kupata taarifa hizo, walienda kushuhudia na kuutambua kuwa ni wa Tyenyi.
Mwili huo ulikutwa ukiwa umeharibika na ulichukuliwa hadi Hospitali Kuu ya Jeshi la Wananchi Tanzania, Lugalo.
“Ndugu wa marehemu ilibidi wapewe taarifa ambapo walifika alipokua akifanyia kazi kisha kwenda Lugalo na kuutambua mwili,”kilisema chanzo hicho.
Mwili huo ulifanyiwa uchunguzi (post mortem) na wanandugu waliruhusiwa kuuchukua tayari kwa mazishi.
Muda wote kabla mwili haujasafirishwa kwenda Musoma kwa mazishi, msiba ulikuwa kwa mdogo wake aitwaye Julius Patrick, Kigamboni.
Kwa mujibu wa familia kupitia kwa Julius, mwili ulisafirishwa kwa ndege Jumamosi asubuhi ya wiki iliyopita na kuzikwa siku hiyohiyo jioni lakini majibu ya uchunguzi hayajapatikana.
Marehemu ameacha watoto watatu na maofisa wa polisi wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo lakini wakasema msemaji ni mkuu wao, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, ACP Charles Kenyela.
ACP Kenyela alipopigiwa simu alithibitisha kutokea tukio hilo.
“Ni kweli mwili wa marehemu ulikutwa kwenye kisima chao lakini upelelezi bado unaendelea,”alisema Kenyela
on Wednesday, June 5, 2013
Post a Comment