Katibu
Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutubia wafuasi wa chama
hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika Matemwe, Mkoa wa Kaskazini
Unguja
Katibu
Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akimkabidhi Mwanachama mpya Kadi
ya Chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika Matemwe, Mkoa wa
Kaskazini Unguja
Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Katibu
Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amewataka
Wanachama na Wazanzibari kwa Ujumla kuendelea kushikamana katika kipindi
hiki cha kuitolea Maoni Rasimu ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ili lengo la Zanzibar kuwa na Mamlaka yake kamili liweze
kufikiwa.
Alisema
mshikamano ndio uliosaidia Rasimu hiyo kupunguza mambo ya Muungano
kutoka 22 hadi 7 na kwamba jitihada zinapaswa ziendelee katika kujenga
hoja ili Wizara ya mambo ya Nje, Bank Kuu na Sarafu, Vyama vya Siasa,
Uraia na Ushuru wa Bidhaa kutolewa katika Mambo ya Muungano.
Maalim
Seif aliyasema hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika
Matemwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja mwishoni mwa wiki.
Alisema
kwa maoni yake Tume ya mabadiliko ya katiba imefanya kazi kubwa ya
kukusanya na kuchambua maoni ya wananchi na hatimaye kupata rasimu ya
awali ya katiba ambayo imezingatia baadhi ya matakwa ya wazanzibari.
Alisema
pamoja na mambo mengine rasimu hiyo ya awali imezingatia kwa makini
uwepo wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imeundwa na nchi mbili
yaani Zanzibar na Tanzania Bara, na kwamba mara kwa mara Rasimu hiyo
imekuwa ikitaja washirika wa Muungano.
Mambo
mengine aliyoeleza kuyakubali katika rasimu hiyo ni pamoja na kutamka
wazi kuwa masuala ya Mafuta na gesi asilia, Mikopo na biashara za nje,
Ushuru wa forodha, pamoja na elimu ya juu na baraza la mitihani kutokuwa
katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
Hata
hivyo alisema kuna mambo kadhaa yanayohitajika kurekebishwa katika
rasimu hiyo ili kufikia lengo la kuwa na Zanzibar yenye mamlaka kamili.
Aliyataja
mambo hayo kuwa ni pamoja na jina la Muungano ambao kwa maoni yake
unapaswa kuitwa “Muungano wa Jamhuri za Tanzania”, tofauti na ilivyo
sasa “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”.
Mambo
mengine aliyoeleza kutoridhishwa nayo kwenye rasimu hiyo ni pamoja na
Mambo ya nje kubakia katika orodha ya mambo ya Muungano, sarafu na benki
kuu, uraia na uhamiaji pamoja na vyama vya siasa.
“Tunataka
Zanzibar iwe na uwezo wa kufanya mambo yake bila ya kuingiliwa, kwa
mfano iwe na uwezo wa kujiunga na Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika
(AU), pamoja na FIFA”, alieleza Maalim Seif.
Aidha
alisema baadhi ya vipengele vya rasimu hiyo havikutolewa maelezo ya
kutosha, hali inayowafanya wananchi kutoelewa mantiki halisi
iliyokusudiwa, na kuiomba tume ya Mabadiliko ya Katiba kuvitolea
ufafanuzi.
Miongoni
mwa vipengele hivyo ni Muundo wa Muungano ambapo amesema zilizoungana
tangu asili ni Tanganyika na Zanzibar, na kutaka Tume iweke wazi
washirika hao wa Muungano.
Hata
hivyo alisema rasimu hiyo bado ina kasoro nyingi ambazo zinapaswa
kujadiliwa zaidi katika mabaraza ya katiba, ili kupata rasimu ya pili
itakayokidhi matakwa ya wananchi, kabla ya rasimu hiyo kufikishwa katika
Bunge la katiba.
Maalim
Seif alifahamisha kuwa Chama cha Wananchi CUF kimeunda jopo la
wataalamu wa Sheria kwa ajili ya kuipitia na kuichambua rasimu ya katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyotolewa hivi karibuni.
Alisema
jopo hilo la wataalamu litakapokamilisha kazi yake, litakuwa na upeo
mkubwa wa kuushauri uongozi wa chama hicho, ili kiweze kutoa tamko rasmi
la Chama kuhusiana na rasimu hiyo ya katiba.
Alisema
bado wananchi wana fursa ya kuchangia katika rasimu hiyo kupitia
wawakilishi wao watakaoingia katika mabaraza ya katiba ambapo wananchi
watatoa uamuzi wa mwisho wakati wa kura ya maoni.
“Wananchi
ndio waamuzi wa mwisho wa mabadiliko ya katiba, kwani baadae mutapata
fursa ya kupiga kura ya maoni ya kuikubali au kuikataa rasimu ya mwisho
kabla ya kutiwa saini na kuwa katiba kamili”, alifafanua Maalim Seif.
Wakati
huo huo Maalim Seif aliwatahadharisha wananchi kutojihusisha na vitendo
vyovyote vya vurugu na uvunjifu wa amani katika kuendelea na mchakato
huo.
Kabla
ya mkutano huo, Maalim Seif alifungua barza ya CUF ijulikanayo kwa
jina la “msimamo” au “mtendeni Namba 2” katika kijiji cha Mfurumatonga,
yenye wanachama 200.
Kwenye
mkutano wa hadhara alikabidhi kadi za CUF 609 kwa wanachama wapya
walioamua kujiunga na chama hicho, huku 148 kati yao wakiwa wamerejesha
kadi za CCM.
Naye
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF Taifa, Salim
Bimani, aliwakumbusha wananchi kujisajili katika daftari la kudumu la
wapiga kura muda utakapofika.
Post a Comment