Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa uzinduzi wa Jumuiya ya Akiba, Mikopo na
Maendeleo Dodoma (Jamimado) katika viwanja vya Kumbukumbu ya Mwalimu
Nyerere.
Lowassa anayetajwa kuwa miongoni mwa wagombea urais mwaka 2015 kupitia CCM,
ambaye amekuwa akiandamwa kwa kufanya siasa kwenye makanisa, alisema amekuwa
akifanya kazi kubwa ya kuchangia masuala ya maendeleo katika vikundi mbalimbali
kwa lengo la kuwakwamua katika umasikini.
“Najua mmenipa heshima ya kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Jumuiya ya
Jumimado kwa kuwa mnajua ninachokifanya kwingine. Sina fedha, lakini nina
ushawishi mkubwa kwa watu na wengi wananiunga mkono,” alisema.
Aliwataka wanajumuiya hiyo kujipanga ili wafanye harambee waweze kupata fedha
zaidi ya sh milioni 500 na kwamba hilo linawezekana.
“Nataka tukifanya harambee iwe babu kubwa ili kila mtu ajue tumefanya nini,
na nilitamani tufanye harambee hiyo kabla ya mwisho wa mwaka huu. Unajua
ukiwawezesha akina mama umeliwezesha taifa na utakuwa umeondoa umasikini,”
alisema.
Lowassa alisema ameamua kutoa sh milioni 10 kwa ajili ya maandalizi ya
harambee itakayokuwa na tija pamoja na kuutunisha mfuko wa jumuiya hiyo.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Aksa Lemwayi katika risala yake alimmwagia sifa
lukuki Lowassa kuwa wanamtambua ni baba wa kupinga umasikini katika maeno
mbalimbali hapa nchini.
“Tunatambua jinsi anavyosimamia na kutekeleza maamuzi yake katika shughuli za
kimaendeleo, amekuwa ni kiongozi wa aina yake katika kutambua na kuthamini
shughuli za maendeleo katika jamii,” alisema.
Aliongeza kuwa Lowassa amekuwa ni kiongozi anayepigana kufa au kupona
kuhakikisha jamii inaondoka kwenye lindi la umasikini.
Lemwayi alisema wanajisikia furaha na ufahari kumualika Lowassa kwenye
uzinduzi wa jumuiya hiyo.
Alisema kuwa jumuiya hiyo kwa sasa inakabiliwa na changamoto za kukosekana
kwa usafiri kwa wanachama wanaotoka maeneo mbalimbali nje ya mji.
Alibainisha kukosekana kwa usafiri kunafanya shughuli za jumuiya hiyo ikiwemo
vikao vya mara kwa mara kushindwa kutofanyika au kufanyika kwa wakati
usiostahili.
Lemwanyi aliziomba taasisi za kifedha zipanue mitandao katika kutoa mikopo
yenye riba nafuu ili kuwawezesha Watanzania wengi kujikwamua katika dimbwi la
umasikini ambao kwa sasa ni kilio kikubwa kwa wananchi wengi.
na Danson Kaijage, Dodoma - TANZANIA DAIMA
Post a Comment