Spika wa Bunge Anne Makinda juzi usiku alifunga mjadala wa
Bajeti Kuu ya Serikali, huku akiwaonya wabunge kwa kunukuu baadhi ya
vifungu vya Kanuni za Kudumu za Bunge inayoashiria kuwa ikiwa
hawatopitisha bajeti hiyo Rais atalivunja Bunge.
Akiahirisha kikao cha 53 cha Mkutano wa 11 wa
Bunge unaoendelea mjini Dodoma juzi usiku, Spika Makinda alitaja Kanuni
ya 107 (1) na (2) ambayo hutumika kukidhi matakwa ya Ibara ya 90 (2)(b)
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayohusu Rais kulivunja
Bunge.
Kanuni hiyo ya 107.(1) inaeleza: “Mjadala kuhusu
Hotuba ya Bajeti ya Serikali utakapomalizika, Spika atalihoji Bunge ili
litoe uamuzi wake wa kupitisha au kutokupitisha Bajeti ya Serikali ili
kukidhi matakwa ya Ibara ya 90(2) (b) ya Katiba.”
Akinukuu kifungu hicho cha Katiba, Makinda
alisema: “Rais hawezi kulivunja Bunge, isipokuwa kama Bunge litakataa
kupitisha bajeti.”
Mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka
2013/14 umejadiliwa kwa siku nne kuanzia Jumatatu wiki hii ambapo
Makinda alisema kuwa wote walioomba kuchangia walifanya hivyo
wamekwisha.
“Nafunga mjadala wa Bajeti ya Serikali Kuu leo, wote walioomba na waliokuwepo wamekwisha,” alisema Spika
Makinda.
Makinda.
Hata hivyo, wakichangia hotuba hiyo, wabunge wengi
walionyesha kupinga bajeti hiyo katika maeneo mbalimbali ikiwamo
misamaha ya kodi, ongezeko la kodi katika mafuta ya petrol na kodi ya
umiliki wa laini za simu (Simcard).
Wabunge pia walipinga bajeti hiyo wakitaka sekta
ya madini ichangie zaidi Pato la Taifa, kupitia na kurekebisha mikataba
ya madini.
Hali hiyo huenda inazua hofu kuwa huenda wabunge wengi wakaipinga kwa kuipigia kura ya hapana.
Kifungu cha 107(2) cha Kanuni za Kudumu za Bunge
inaelekeza kuwa uamuzi wa Bunge kupitisha au kutokupitisha Bajeti ya
Serikali utafanywa kwa kupiga kura ya wazi kwa kuita jina la mbunge
mmojammoja.
Jana Makinda alitangaza Jumatatu ijayo ya Juni 24
kuwa ndiyo siku ambapo wabunge watapiga kura kwa kuitwa majina
mmojammoja ili kupitisha Bajeti ya Serikali au la.
Hata hivyo, kurejea kwa wabunge wa Kambi Rasmi ya
Upinzani wa Chadema ambao hawakuchangia mjadala huo wa Bajeti Kuu ya
Serikali, hata kuwasilisha Bajeti Mbadala, kunaongeza hofu kuwa huenda
wabunge wote wa kambi hiyo wakaipinga.
Wabunge
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kuhusu kauli hiyo
ya Spika, baadhi ya Wabunge walikuwa na mtazamo tofauti huku baadhi
wakisema Bunge halijawa na meno ya kuisimamia Serikali.
Mbunge wa Lindi, Salum Barwany (CUF) alisema:
“Bunge halijawa na meno ya kuisimamia Serikali, kanuni iliyopo na
aliyoitaja Spika Makinda inakinzana na uamuzi wa Bunge; inaonekana kuwa
Bunge siyo sehemu ya kuisimamia Serikali.
Aliongeza kuwa hali hiyo ni athari ya Bunge kuwa
sehemu ya Serikali na kwamba ingawa wabunge wa upinzani wanaweza
kuikataa, lakini wale wa chama tawala CCM wanabanwa wakilazimishwa
kuiunga mkono.
Kwa upande wake Mbunge wa Nzega, Dk Hamisi
Kigwangalla (CCM) alisema: “Ingawa mimi sikuunga mkono bajeti katika
mchango wangu, wabunge wa chama tawala CCM, tunalazimika kupiga kura ya
ndiyo ili kuilinda dola inayoongozwa na chama chetu.
Alifafanua: “Huu ni utaratibu wa kawaida wa
mabunge yanayofuata mfumo wa Westminster, wa uelekeo wa itikadi, mfano
hapa tuna kambi ya rasmi moja ya upinzani na Serikali. Upinzani una haki
ya kukataa, lakini wabunge wote wa CCM lazima walinde dola.”
Naye Mbunge Sylvester Mabumba alisema hatua hiyo
ya Spika inawaandaa wabunge kupitisha bajeti hiyo, kwani kutokuipitisha
ni sawa na kuizuia Serikali isitekeleze mipango yake kwa mwaka ujao,
hivyo Katiba inaruhusu Rais kulivunja Bunge.
Hata hivyo, jana katika kile ninachoweza
kutafsiriwa kama ni kuwapiga mkwara wabunge wakati akiahirisha kikao cha
Bunge, Spika Anne Makinda alitaka wabunge wote kuwapo bungeni Jumatatu
ijayo kwa ajili ya kupiga kura akisema hata walio safarini ni lazima
warejee na kushiriki upigaji kura huo muhimu.
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment