LICHA ya kuwepo
kwa shule za msingi na sekondari kwa Mkoa wa Kilimanjaro ambazo kwa
kiasi fulani zinakidhi mahitaji, bado kuna changamoto kadha wa kadha
ambazo zinaathiri maendeleo ya kitaaluma kwa baadhi ya maeneo. Wilaya ya
Rombo ambayo ni moja ya wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa
maeneo yanayokabiliwa na changamoto za kipekee kitaaluma hasa elimu ya
sekondari.
Wilaya hii imefanikiwa kuwa na shule nyingi za
sekondari hasa zile za Serikali licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa
katika uendeshaji wa shule hizi. Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wadau
wa elimu wilayani Rombo, kuna jumla ya shule za Sekondari 48; yaani
shule zinazomilikiwa na Serikali 41 huku zile za binafsi zikiwa saba tu.
Tofauti na maeneo mengine ya Tanzania idadi kubwa ya
wazazi wilayani Rombo wana mwamko wa kuwapeleka watoto wao shule kupata
elimu ya sekondari mara baada ya elimu ya msingi. Hatua hii pekee ya
kumpeleka sekondari mtoto ni kutambua umuhimu wa elimu kiasi fulani kwa
mtoto. Wapo pia wanaojitahidi na hata kulipa michango na mahitaji kwa
wakati japo si wote.
Lakini kumpeleka mtoto shule na kutomfuatilia
anafanya nini wakati gani na hata anaporudi nyumbani baada ya shule
haitoshi. Uchunguzi mdogo uliofanyika katika baadhi ya maeneo ya mpakani
mwa Tanzania na Kenya katika ndani ya Wilaya ya Rombo, yakiwemo maeneo
ya Holili, Tarakea na Rongai imebaini licha ya baadhi ya wazazi kuwa na
mwamko wa kuwapeleka sekondari watoto wao hawafuatilii maendeleo yao
kabisa.
Hali hii imesababisha wanafunzi hao kujihusisha na
shughuli nyingine zaidi ya elimu za kutafuta fedha (biashara). Maeneo
haya yapo mpakani sehemu ambazo zinashughuli nyingi za kibiashara na
kazi ndogo ndogo za kufanya. Uchunguzi umebaini wapo wanafunzi ambao
hufanyabiashara na kazi za vibarua ndogo ndogo huku wakiendelea na shule
jambo ambalo linaathiri maendeleo yao kitaaluma na eneo zima.
Wapo wanafunzi wa sekondari ambao hufanya kazi za
kuendesha pikipiki za abiria maarufu kama bodaboda mpakani na huku
wakiendelea na shule, wapo pia ambao hufanya vibarua vya kubeba mizigo
na hata kulimishwa kwenye mashamba hasa eneo la Kenya na kulipwa ujira
wa siku. Shughuli hizi za utafutaji kipato zinapowanogea wengine huacha
kabisa shule na kuendelea za shughuli za utafutaji kipato.
Wasichana wao hukimbilia kufanya kazi za ndani hasa
kwa wenyeji wa Kenya na pia kufanya kazi za uuzaji vinywaji baa. Mji wa
Loitokitoki uliopo mpakani kabla ya kuingia nchini Kenya ndio wenye
idadi kubwa ya biashara na shughuli kama hizi ambazo hufanywa na
wasichana wengine wakiwa wamekimbia shuleni ama baada ya darasa la saba
bila kujali kama amechanguliwa kuendelea au kuishia mnjiani kutokana na
uangalizi mdogo ki-malezi.
Ramadhan Ally ni mmoja wa wakazi wa Tarakea wilayani
Rombo, anasema baadhi ya wanafunzi huamua kujiingiza kwenye shughuli za
utafutaji kipato kutokana na usimamizi mdogo wa wazazi/walezi wao.
"Wapo wazazi ambao wamewaacha watoto wao chini ya uangalizi wa bibi au
babu wao wapo 'busy' kibiashara nchini Kenya, wapo wazazi wengine
huwashirikisha watoto wao kufanya vibarua vya mpakani ili kukuza kipato
cha familia...sasa hali kama hii inamfanya mtoto asione umuhimu wa shule
na wakati mwingine baadae uamua kuacha kabisa shule," anasema Ally.
Anaongeza kuwa wapo baadhi ya wazazi hawawatimizii
mahitaji ya shule watoto wao hivyo watoto kuamua kutafuta chochote
wenyewe. Hili huwenda likawa na ukweli, uchunguzi uliofanyika katika
sekondari za Tanya, Nduweni, Ngaleko, Urauri na Mbomai umebaini muitikio
wa ulipaji wa ada na michango mingine kwa wazazi/walezi ni mdogo sana
kwa wazazi. Kiujumla madeni ni mengi dhidi ya wanafunzi.
Venance Mramba ni Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Sekondari
ya Nduweni, katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya anakiri
mwamko mdogo wa waza/walezi kwa ulipaji ada na michango mingine shuleni
hapo. "...Ukweli hapa madeni ya wanafunzi ni mengi ikiwemo ada na
michango mingine...," anasema Mramba.
Victus Kiwango ni Mkuu wa Sekondari ya Tanya iliyopo
wilayani Rombo maeneo ya mpakani, anakiri pia mwamko mdogo wa wazazi
kuchangia ada na michango mingine katika shule yake, anaongeza kuwa wapo
wanaodiriki kusema kuwa uwezo wao kiuchumi ni mdogo wa ulipaji ada na
michango mingine.
Hata hivyo kwa upande wake Mwalimu Mkuu Msaidizi wa
Sekondari ya Holili, Benson Samizi iliyopo eneo la Wilaya ya Rombo
mpakani anabainisha kuwa mwitikio wa wazazi kufuatilia maendeleo ya
watoto wao shuleni hapo ni mdogo kabisa. Anasema hata wanapo itisha
mkutano wa wazazi shuleni hapo mwitikio huwa ni mdogo pia, wazazi wengi
huagiza wawakilishi baada ya kuja wao wenyewe.
"...Changamoto nyingine shuleni kwetu ni u-'busy' wa
wazazi na biashara zao. Naamini wazazi wengi hapa hawafuatilii
maendeleo ya watoto wao shuleni, mzazi utakuta unamuita kumshirikisha
jambo kwa maendeleo ya manae lakini anatuma mwakilishi, majukumu yao
kiusimamizi kwa mtoto anayatupa kwa mwalimu...sasa mwalimu hawezi
kufanya kila kitu bila ushirikiano na mzazi," anasema Samizi.
"Binafsi nilijaribu kufanya utafiti mdogo shuleni
kwetu wa kuangalia ni kwa kiasi gani wazazi wanafuatilia maendeleo ya
mtoto shuleni...lakini huwezi amini kwa mwaka mzima walikuja wazazi
wawili tu wenyewe kuulizia maendeleo ya watoto wao, hapa unaweza
kuangalia ni namna gani watu hawa wapo 'busy' na shughuli zao zaidi ya
maendeleo ya mtoto shuleni. Hata ukiitisha kikao cha wazazi hawafiki
robo tatu ya wanafunzi wanaokuja shuleni," anasema mwalimu Samizi.
Aidha anakiri uwepo wa wanafunzi ambao hurubuniwa na
kujiingiza katika shughuli nyingine nje ya masomo na wengine kuacha
shule. Anasema kuwa kwa mwaka 2013 shule hiyo ilipewa jumla ya wanafunzi
wa kidato cha kwanza 140 lakini walioripoti ni wanafunzi 85 tu, huku
wengine 30 kupelekwa katika shule za binafsi. idadi iliyosalia
hawajulikani walipo hadi sasa. Anaongeza kuwa kuanzia mwaka 2011 hadi
Mai 2013 jumla ya wanafunzi 7 walitiwa mimba na kesi zao kushughulikiwa
katika hatua anuai.
Sim Msami Silayo ni Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya
Urauri iliyopo maeneo ya mpakani Wilaya ya Rombo, anasema tangu nyakati
za ukoloni kulikuwa na kasumba ya wanafunzi kwenda kufanya vibarua
maeneo ya mpakani anasema hali hii imeendelea mpaka leo. Anasema zipo
baadhi ya familia zinautaratibu wa kwenda kufanya vibarua kwa makundi
hivyo kuwaathiri baadhi ya wanafunzi.
Anasema kwa taarifa ambazo wanazo wapo baadhi ya
mabinti hukimbia shule na kwenda kufanya kazi za uuzaji vinywaji baa na
wengine kazi za majumbani hali ambayo uongozi wa shule umekuwa
ukiendelea kupambana kukabiliana na changamoto hiyo.
Wakati hali iko hivyo wanafunzi kama Thabit Kayanda
(si jina lake halisi) japokuwa ni mmoja wa wanafunzi wilayani Rombo
wanamtazamo tofauti. "...Unapoona mzazi yupo 'busy' na biashara zake
kiasi hata cha kutokutimizia mahitaji yako ya shule lazima uanze
kujitengenezea maisha yako mwenyewe hivyo mtu unajikuta unaingia katika
biashara au shughuli zingine kujipatia fedha. Na kama unafanya na
kufanikiwa (kupata fedha) unajikuta unaona hakuna haja ya kuendelea na
shule...kumbuka kila mmoja anasoma ili aje kupata fedha za kuendesha
maisha yake, kama unaanza kufanikiwa chochote hakuna haja ya kuendelea
na shule," ni maneno ya Kayanda na mtazamo tofauti.
Hata hivyo mtazamo wa wanafunzi kama Kayanda na
changamoto nyingine zilizopo wilayani Rombo haziondoi umuhimu wa elimu
kwa kila mtoto. Hivyo kila mmoja na kila upande unakila sababu ya
kuhakikisha unatimiza wajibu wake na elimu kupewa kipaumbele maeneo yote
bila kujali changamoto zilizopo.
Post a Comment