Dar es Salaam. Wanafunzi 30,063 waliopata
daraja sifuri katika matokeo yaliyopita, wameula baada ya kupandishwa hadi
daraja la nne kutokana na ukokotoaji upya wa matokeo ya mtihani wa kidato cha
nne yaliyofanywa na Baraza la Mitihani la Taifa (Nacte) na kutangazwa
jana.
Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa
Marekebisho hayo yalifanyika baada ya kufutwa
kwa matokeo ya awali yaliyotangazwa Februari 18, mwaka huu.
Kufutwa kwa matokeo hayo, ilikuwa ni
utekelezaji wa sehemu ya mapendekezo ya Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu Mizengo
Pinda, baada ya wanafunzi 240,909 kupata daraja sifuri kwenye matokeo
yaliyotangazwa mara ya kwanza.
Akitangaza matokeo hayo jana, Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema sasa watakaokuwa na sifuri ni
210,846 sawa na asilimia 56.92 wakati wavulana wakiwa ni 104,259 na wasichana
106,587.
Hiyo ina maana kuwa sasa ufaulu umepanda na
kuwa asilimia 43.08 badala ya ule wa kwanza ambao ulikuwa asilimia 34.5.
Dk Kawambwa alisema kutokana na ukokotoaji mpya
wa matokeo ya sasa, idadi ya wanafunzi waliofaulu mtihani huo kwa daraja la
kwanza mpaka la nne imeongezeka na kufikia wanafunzi 159,747 kutoka
126,847.
Wanafunzi waliopata daraja la kwanza ni 3,242
wavulana wakiwa ni 2,179 na wasichana 1,063 ikiwa ni asilimia 0.88 ya matokeo
yote, daraja la pili ni 10,355 sawa na asilimia 2.8 wavulana wakiwa 7,267 na
wasichana 3,088.
Waliopata daraja la tatu ni 21,752 sawa na
asilimddia 5.87 wavulana wakiwa 14,979 na wasichana 6,773, daraja la nne ni
124,260 sawa na asilimia 33.54 .
Tofauti na matokeo yaliyofutwa, ambayo
watahiniwa waliopata daraja la kwanza walikuwa ni 1,641, wavulana wakiwa 1,073
na wasichana 568, daraja la pili ni 6,453, wavulana wakiwa 4,456 na wasichana
1997.
Waliopata daraja la tatu walikuwa 15,426,
wavulana 10,813 na wasichana 4,613, waliopata daraja la nne 103,327, wavulana
64,344 na wasichana 38,983 huku waliopata sifuri wakiwa 240,903, wavulana
120,664 na wasichana 120,239.
Dk Kawambwa alieleza watahiniwa waliosajiliwa
kufanya mtihani huo walikuwa ni 480,029 na waliofanya ni 458,139 sawa na
asilimia 95.44.
Alisema kuwa watahiniwa wa shule waliosajiliwa
kufanya mtihani huo walikuwa ni 411,225 na waliofanya ni 397,138 sawa na
asilimia 96.57 huku wa kujitegemea wakiwa ni 68,804 na waliofanya ni 61,001.
MWANANCHI
Post a Comment