Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kinawasilisha na mawakili wake na asasi za
haki za binadamu kujua hatua za kisheria kuchukua dhidi ya askari wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa madai ya kutekwa na kuteswa Naibu Mkurugenzi wa
CUF Taifa, Shaweji Mketo, na viongozi wengine wa chama hicho Mkoa wa Mtwara.
Mpango huo ulitangazwa jana jijini Dar
es Salaam na Mwenyekiti wake wa Taifa, Profesa Ibrahimu Lipumba wakati akiongea
na waandishi wa habari.
Prof. Lipumba
alisema pia chama hicho kinawasiliana na mawakili hao kujua hatua za kisheria za
kuchukua dhidi ya Jeshi la Polisi kwa madai ya kuwabambikia kesi viongozi hao
ambao kimedai walikamatwa na kupigwa na askari wa JWTZ katika kambi yao ya
Naliendele.
Alisema pia wanawasiliana
na asasi za kiraia zinazoshughulikia haki za binadamu na haki za wanawake
kumsaidia kisaikolojia mwanamke anayedaiwa kubakwa na askari wa JWTZ mkoani humo
na kufikishwa mahakamani.
Lipumba
aliwataja viongozi wengine wa CUF waliodaiwa kutekwa na kuteswa kambini Juni 28,
mwaka huu kuwa ni Salum Mohamed ambaye ni Mwenyekiti wa CUF Mtwara Mjini,Ismail
Jamal Mwenyekiti wa CUF Mtwara vijijini.
Wengine ni Mwenyekiti wa Vijana Mtwara mjini, Ismail
Njalu, Katibu wa CUF Mtwara mjini, Said Kulaga na Kashindye Kalungwana ambaye ni
dereva wa jeshi hilo makao makuu.
Alidai viongozi hao baada ya kutekwa na askari wa JWTZ
walivuliwa nguo zote na kulazwa kifudifudi, kumwagiwa maji ya baridi na kupakwa
chumvi kisha kuanza kupigwa usiku kucha kwa kutumia mikanda ya jeshi, ngumi,
mateke na fimbo maalum za ngozi za wanyama na miti maalum.
Alisema viongozi hao wakiwa njia kurejea Mtwara Mjini
wakitokea Msimbati magari mawili ya jeshi yaliziba barabara baada ya kuliona
gari la CUF na wanajeshi walianza kuwashusha na kuwapiga kisha kuwarusha kwenye
karandinga lao.
Alisema baadaye
walipelekwa katika kambi ya Naliendele kabla ya kuachiwa saa 5:00 usiku na
kukabidhiwa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara.
“Kwa bahati mbaya Mketo alipigwa sana katika ubavu wake
wa kulia ambao amewahi kufanyiwa operesheni kubwa miezi kadhaa iliyopita,.
Alipoona anapigwa sana eneo hilo akaona awaombe askari wampige maeneo mengine
lakini eneo hilo wamhurumie, kusikia vile askari wale walimgeuza kwa nguvu na
kuanza kumpiga mateke ya nguvu zaidi katika eneo lile hadi alipoteza
fahamu,”alisema.
Alisema Mketo
alipozinduka Juni 28, mwaka huu alijikuta ana dripu na hakuelewa ni ya nini na
baadaye wanajeshi waliitoa.
Profesa Lipumba alisema tukio la
utesaji raia ndani ya kambi ya jeshi ikiliunganishwa na matukio mengine kama ya
utesaji wa Dk.Stephen Ulimboka , kutekwa nyara kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la
Wahariri (TEF), Absalom Kibanda, kulipuliwa bomu katika mkutano wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kunadhihirisha hatua za awali za kusambaratika
kwa dola.
Msemaji wa JWTZ, Kapambala
Mgawe, alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo zinazoelekezwa kwa askari wa jeshi lake,
alisema suala hilo linatiwa chumvi na wanasiasa kwasababu kiutaratibu anayetekwa
ni adui hivyo raia wa Tanzania hawezi kutekwa na wanajeshi.
Mgawe alisema tuhuma zinazoelekezwa kwa wanajeshi zina
lengo la kutaka kulichafua jeshi hilo ili lisifanye kazi yake kwasababu vipo
vipengele vya kisheria vinavyoruhusu askari wa JWTZ kuliingilia kati kudumisha
amani kunapotokea Jeshi la Polisi limezidiwa.
Alisema katika kipindi hiki ambacho kuna vurugu nyingi
zinajitokeza katika nchini jeshi litakapokuwa linachukua hatua ya kudhibiti
yatesemwa mengi ikiwamo askari kuhusishwa na vitendo vya
ubakaji
Loading...
Post a Comment