Makamu Wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal ameiwakilisha Tanzania katika Mkutano wa Umoja wa
Afrika unaojadili namna ya kumaliza Baa la Njaa katika nchi za Afrika.
Mkutano huo wa siku moja umefanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia
Jumatatu Julai Mosi, 2013 ambapo nchi washiriki wamekumbusha kuhusu
Azimio la Maputo walilolitoa miaka 10 iliyopita yaani mwaka 2003, azimio
lililolenga kukabiliana na Njaa na Utapiamlo.
Azimio
hilo lililenga kuzitaka nchi za Afrika kukabiliana na Baa la Njaa
sambamba na kuhakikisha kuwa wananchi wa Bara hili, si tu kwamba
wanapata uhakika wa chakula, bali kula chakula bora chenye virutubisho
vinavyohitajika katika kulinda afya za binadamu na hivyo kuwa na uwezo
wa kukabiliana na magonjwa. Pia azimio hilo lilizitaka nchi wanachama wa
Umoja wa Afrika kuhakikisha zinatanua bajeti zake za Kilimo ili zifikia
asilimia 10 ya Bajeti Kuu na pia kukifanya Kilimo kuchangia kwa
asimilia 6 katika ukuaji wa uchumi wa nchi za Afrika.
Katika
mkutano huo, Mheshimiwa Makamu wa Rais alieleza kuwa Tanzania
inashirikiana bega kwa bega na nchi za Afrika katika kuhakikisha kuwa
Bara hili linakabiliana vilivyo na baa la njaa na hivyo kutokomeza Baa
hilo kama nchi hizo zilivyokubaliana katika mkutano uliofanyika Maputo
mwaka 2003 uliopendekeza pia kuwa nchi za Afrika ziwe zimefanikiwa
kukabiliana na Baa la Njaa na Utapiamlo ifikapo mwaka 2025.
Katika
maelezo yake, Mheshimiwa Makamu wa Rais alifafanua kuwa Tanzania
imepiga hatua katika kilimo kupitia mpango wa Kilimo Kwanza na pia
mpango wa kukuza uzalishaji kwa kutumia kanda maalum maarufu kama SAGGOT
(unaojumuisha mikoa iliyo na uwezo wa kuzalisha chakula kwa wingi)
umeanza kukubalika na kuwa mpango wa nchi nyingi za Afrika. Hata hivyo
Mheshimiwa Makamu wa Rais alifafanua pia kuwa, ukuzaji wa Kilimo
unapaswa kuambatana na sekta nyingine kama Nishati, Miundombinu, Viwanda
na Biashara.
Umuhimu
wa kukuza sekta hizo unatokana na ukweli kuwa, zinachangia kukuza
kilimo, kukifanya kuwa na tija na pia kutoa unafuu wa uzalishaji kwa
wakulima. Tena kwa kukuza sekta hizo, Afrika inaweza kupiga hatua kubwa
kwani tatizo la uzalishaji halitokani na upungufu wa uzalishaji tu, bali
hata pale panapokuwa na uzalishaji mkubwa, kuna maeneo ambayo mazao
yameshindwa kulifikia soko ama kufikishwa kwa watu wenye mahitaji.
Awali
akichagia katika mkutano huo, Rais Mstaafu wa Brazil Lula da Silva
alisema njaa ni jambo la kijamii, linalochangiwa kwa kiasi kikubwa na
binadamu wenyewe hasa pale mtaji na kipato kinapobakia kuwa katika
mikono ya wachache wakati wengi wakiambulia patupu.
Rais
Lula pia alimnukuu Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere na kusema; “kama mnataka maendeleo lazima mshirikishe wananchi
wote.” Kwa kutumia nukuu hii, Rais Lula anasisitiza kuwa, Afrika
inapaswa kuwa na mipango inayoshirikisha wananchi ili iwasaidie kukua
kiuchumi na kukabiliana na matatizo yanayowakabili katika maisha yao.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika Dkt. Nkosazana Zuma
alisema barani Afrika kuna changamoto kubwa inayowakabili akina mama na
moja ni kubwa ni kukosa fursa ya kumiliki ardhi hali inayofanya
uzalishaji kuwa duni. “Jambo hili linaweza kubadilishwa na sisi,
tunaweza kubadili tamaduni zetu kwa kuwa tunatambua mchango mkubwa wa
akina mama katika Kilimo. Hata hivyo, kama hatutafanya mabadiliko akina
mama watabakia nyuma na bara la Afrika litazidi kukabiliana na Baa la
Njaa,” alisema.
Naye
Rais Mstaafu wa Nigeria Olesegun Obasanjo aliueleza mkutano huo kuwa,
zipo tamaduni barani Afrika ambazo zinawabagua wanawake japokuwa ndio
wazalishaji zaidi. Pia akaongeza kuwa, wanawake wasitumike katika
shughuli za kisiasa tu bali wawezeshwe ili kufanikisha azma ya Afrika
kukabiliana na njaa.
Makamu
wa Rais katika mkutano huo ameambatana na Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika Injinia Christopher Chiza pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mahadhi Juma Maalim. Katika Mkutano huo
pia viongozi mbalimbali wamehudhuria akiwemo Rais Mstaafu wa Brazil Lula
da Silva, Rais Mstaafu wa Nigeria Olesegun Obasanjo, Rais Mstaafu wa
Ghana John Kuofor. Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni
Mkurugenzi wa Shirika la Chakula Duniani, Jose Graziano da Silva,
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika Dkt. Nkosazana Zuma, Rais wa Sudan,
Benin na wawakilishi wa nchi mbalimbali ambazo ni wajumbe wa Umoja wa
Afrika.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Ethiopia Julai 02, 2013
Post a Comment